Habari za Punde

Akinamama Zanzibar Wafanyiwa Uchunguzi wa Saratani ya Matiti Bila ya Malipo

Baadhi ya akinamama waliofika katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Zanzibar kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa maradhi ya saratani ya matiti wakipata maelekezo kutoka kwa mhudumu wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Ilala Afya Centre ya Dar es salaam Jaffer Dharsee (kulia) akibadilishana mawazo na viongozi wa Jumuiya ya watu wanaoishi na saratani Zanzibar  (ZCA) ambapo taasisi hizo mbili kwa kushirikiana na Wizara ya Afya zimeandaa kampeni hiyo.
Daktari Nalvis Dominguez Torres akimfanyia uchunguzi mama aliyefika katika hospitali ya mnazi mmoja kwa uchunguzi wa saratani ya maradhi ya matiti. 
Daktari bingwa wa uchunguzi wa maradhi ya saratani Zanzibar Msafiri Marijani akichukua sampuli kutoka kwa  mmoja wa akinamama waliofika Hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi wa saratani. 
Mkurugenzi wa Ilala Afya Centre ya Dar es salaam Jaffer Dharsee akitoa maelekezo kwa akinamama waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti katika kampeni iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa kituo hicho, Wizara ya Afya na ZCA.(Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.)

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar. 26.11.2016
Zaidi ya wanawake 500 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi hayo (ZCA), Ilala Afya Centre ya Dar es salaam na Wizara ya Afya Zanzibar.

Kampeni hiyo ya siku moja iliyofanyika Hospitali kuu ya Mnazimmoja iliwashirikisha akinamama wenye umri  kuanzia miaka 25 ilikuwa na lengo la kuweza kuwagundua mapema akinamama wenye tatizo la maradhi hayo ambayo dalili zake zinachelewa kujitokeza.

Daktari bingwa wa uchunguzi wa maradhi ya saratani Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa ZCA Dkt. Msafiri Marijani amesema kampeni hiyo ilihusisha uchunguzi wa  Utrasound na uchunguzi wa sindano na waliopatikana na dalili watafanyiwa vipimo ili kujua kama ni saratani ama matatizo mengine.

Dkt. Marijani amekumbusha kuwa saratani hadi hivi sasa haina tiba na kitu muhimu ni kuigundua mapema ili kuidhibiti kabla haijaleta athari kubwa hivyo amewashauri wananchi kupima afya zao mara kwa mara.

“Saratani ni maradhi yanayouwa watu wengi duniani kutokana na kuchelewa kugundulika mapema, kitu muhimu ni wananchi kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao,” alisisiti Dkt. Marijani.

Amesema Hosipitali zote za Wiala na vituo vingi vya Afya vya vijijini vinatoa huduma ya uchunguzi wa saratani hivyo amewashauri wananchi kuvitumia.

Kiongozi wa Jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi ya saratani Zanzibar  Bi. Zakia Mohd amesema kufuatia uchunguzi huo ambapo zaidi ya wanawake 100 wamebainika kuwa na dalili za saratani, wamegundua kuwa tatizo ni kubwa  kinyume na walivyo fikiria awali.

Amesema kutokana na hali hiyo ZCA itafikiria kununua chombo maalumu cha uchunguzi ‘mamography’ ambacho kinauwezo wa kugundua dalili za awali kabisa za maradhi hayo.

Ameongeza kuwa Jumuiya imeazimia kufanya uchunguzi mwengine wa saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya tenzi dume katika siku zijazo kwa vile ni miongoni mwa maradhi yanayowasumbuwa wananchi wengi wa Zanzibar.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.