Habari za Punde

Dk Shein atoa agizo zito Pemba: Ataka wananchi wa Ngomeni Mgelema wajengewe barabara ndani ya mwaka mmoja


Na Haji Nassor, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk: Ali Mohamed Shein, ameiagiza Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, kuhakikisha inaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kuyuni - Ngomeni wilaya ya Chakechake Pemba, katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Alisema wananchi wa Ngomeni ni sawa sawa na wananchi wengine wa Zanzibar, hivyo Serikali iwatumikie bila ya kujali itikadi zao, ikiwa ni pamoja na kuwajengea barabara ya kisasa.
Dk: Shein ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi hao, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba na kusema kuwa lazima wananchi hao wafikishiwe huduma zote muhimu.
Alisema hakuna sababu kwa wananchi wa eneo hilo ambao wanazalisha zao la taifa la karafuu kwa wingi kisha kuendelea kupata tabu ya usafiri hasa wa nchi kavu.
Rais huyo aliitaka wizara hiyo kuhakikisha ifikapo mwezi Novemba mwaka 2017, barabara hiyo imeshakamilika ujenzi wake kwa kiwango cha lami, ili wananchi wapate kusafirisha mazao na shughuli zao kwa ufanisi.
“Serikali yenu ipo kwa ajili ya kuwahudumia, sasa haipendezi na wala siamini, eneo hili la Ngomeni amabalo linazalisha karafuu kwa wingi na kisha wananchi wapate usumbufu’’,alifafanua.
Agizo hilo la rais wa Zanzibar lilikuja kufuatia risala fupi ya wananchi hao, iliosomwa na Ibrahim Zubeir Mmasiku, kuelezea jins-i wanavyosumbuka na suala la miundombinu ya barabara.
Mwananchi huyo kwa niaba ya wenzake, alisema pamoja na eneo hilo kuzalisha karafuu kwa wingi lakini wanakabiliwa na matatizo kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa barabara.
Aliitaja matatzio mengine kuwa ni ukosefu wa kituo cha afya, huduma ya nishati ya umeme, uhaba wa maji safi na salama ambapo miundombinu ya maji yaliopo yameshaanza kuchakaa.
Baada ya maelezo ya wananachi hao, ndipo Rais huyo wa Zanzibar alipowataka wakuu wa taasisi hizo kujibu hoja hizo za wananchi, ambapo aliziagiza wizara zake kufanikisha maombi ya wananchi hao.
Aidha rais huyo wa Zanzibar aliipa miezi tisa kuanzia mwezi huu wizara ya afya kujenga kituo cha afya cha cha daraja la kwanza, ili wananchi hao wafikao 600 waondokane na tatizo la kufuata huduma hiyo masafa marefu.
“Hii serikali iliopo madarakani, lengo la madhumuni yake ni kuwahudumia wananchi wote katika sekta zote, zikiwemo za afya, ndani ya miezi tisa, kituo cha afya kiwe kimekamilika’’,alifafanua.
Hata hivyo dk Shein amesikitishwa na wananchi wa shehia hiyo ya Mgelema kijiji cha Ngomeni kuendelea kuuza karafuu zao kwenye banda la zamani, ambapo alilitaka ZSTC kujenga kituo kipya ndani ya miezi mitatu.
Alisema alishatoa maagizo zamani kwa ZSTC, kujenga vituo vipya na vya kisasa vya kuuzia karafuu, na anashangaa kuona maeneo yenye kuzalisha karafu kwa wingi vimejengwa na kuacha maeneo mengine ikiwemo Ngomeni.
“Sasa baada ya miezi mitatu, nitakuja tena Ngomeni kuja kuona kituo kipya cha kununulia karafuu, ili kila mmoja aone jinsi kijiji hichi kinavyopendeza kwa kituo hicho’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi dk: Ali Mohamed Shein ameiagiza wizara inayoshugulikia maji, kuyafanyia mapitio miundombinu iliopo ili wananchi wapate huduma hiyo.
Alisema hakuna sababu kwa wananchi hao kuendelea kupata huduma hiyo usiku mkubwa, na sasa lazima wizara husika ifanye kila mbinu kwa kushirikiana na Mkuu wa mkoa lipatiwe ufumbuzi.
“Maji ndio kila kitu, lazima mkuu wa Mkoa washirikiane pamoja na ZAWA, ili huduma ipatikane, lakini nayo mabadiliko tabia nchi yametuathiri, lakini hayo haba yaliopo yapatikane’’,alifafanua.
Kuhusu huduma ya nishati ya umeme kwa wananchi hao wa Ngomeni, ameigeukia wizara hiyo ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kupitia shirika la umeme ZECO, nao kutumia miezi mitatu kufikisha huduma hiyo kijijini hapo.
Aidha rais huyo wa Zanzibar amewaahidi wananchi hao kwamba atafika kijijini tena hapo kwa ajili ya kuangalia huduma nyengine kama za kielimu na nyengine alizozitolea maagizo.
Wakati huo huo rais huyo wa Zanzibar akizungumza na wananchi wa Shehia ya Minazini wilaya ya Mkoani, mara baada ya kuikagua barabara ya Mgagadu- Kiwani amewahakikisha kuwa barabara hiyo itafika hadi mwisho kwa kiwango cha lami.
“Mimi nimepokea ombi lenu, kwamba barabara ifike hadi mwisho wa pwani, lakini tukubaliane kwamba itakuwa ni kwa awamu ya pili hii kwanza tuache ifike hadi hapo tulipokwisha jipangia’’,alifafanua.
Akizungumza na wananchi wa Mgelema wilaya ya Chakechake, wamewasisitiza kuendelea kuuza karafuu zao ZSTC, ili serikali ipate fedha kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.
Aliwataka wananchi hao wasikubali kuwaauza wahujumu w auchumi kwa kusafirisha magendo, na badala yake waziuze serikali ili, kufanikisha malengo yake.
“Barabara yenu ya Kipapo –Mgelema tuaijenga kwa kiwango cha lami tena kabla ya mwaka 2020, kwa fedha hizi hizi ambazo mnauza karafuu zenu ZSTC, sasa lazima tuwa makini na wasafirishaji magendo’,alifafanua.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid Abdalla, alisema wamekuwa karibu mno za wizara kadhaa, katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi na Utunzani Barabara UUB- ZanzibarAli Tahiri Fatawi alimueleza rais huyo, uchakavu wa vitendea kazi, huzorotesha ujenzi wa barabara.
“Vifaa kadhaa likiwemo la kumwagia lami, ni vya zamani sana, sasa wakati mwengine huharibika na kutengeneza lakini vimeshachoka, ndio maana tunakwenda kwa kusita sita’’,alifafanua.
Aidha rais huyo wa Zanzibar amendelea kurejea kauli yake, ya kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida, maana uchaguzi umeshakamilika na rais ameshapatikana.
“Endeleni na kazi zenu, mvuvi akavue, mkulima aendelee, anechonga muda ndio huu, hakuna rais mwengine na wala hakuna uchaguzi mwengine mapaka 2020’, msidanganywe’’,alifafanua.

Katika ziara hiyo rais huyo na ujumbe wake, alitembelea barabara za Mgagadu - Kiwani, barabara ya Ole – Kengeja, Kuyuni – Ngomeni na Kipapo- Mgelema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.