Na Rajan Mkasaba.
MKE wa Rais wa Zanzibar
Mama Mwanamwema Shein amewataka akinamama pamoja na viongozi na wanachama wa
Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kushirikiana na Serikali yao ya Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na taasisi husika katika vita dhidi ya ukatili na udhalilishaji
wa watoto na wanawake.
Mama Shein aliyasema hayo
leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na akinamama, viongozi na wanachama
wa (UWT) wa Wilaya ya Dimani na Wilaya ya Mfenesini Kichama kwa lengo la
kuwasalimia na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono CCM, ikiwa ni muendelezo
wa ziara zake kwa mikoa yote ya Zanzibar.
Katika maelezo yake
Mama Shein alisema kuwa inasikitisha sana kuona kuwa miongoni mwa jamii wapo
watu ambao wanajitoa mishipa ya ufahamu na kuwadhalilisha watoto kwa kuwafanyia
vitendo viovu.
Aliwataka viongozi hao
pamoja na akinamama kusimama imara na kupiga vita kwa nguvu zao zote vitendo
vya aina hiyo na kuwataka kuungana katika kuvikomesha kwa vile ni kinyume cha
ubinaadamu, kinyumme cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu na pia, ni vitendo
vinavyoiabisha jamii ya Kizanzibari.
Hivyo, Mama Shein
aliwasisitiza viongozi hao,akinamama na wanajumuiya ya UWT kwa kila mmoja awe
askari kwa kuwaripoti, wanaohusika katika vyombo vya sheria, ili wachukuliwe
hatua zinazostahiki.
Mama Shein alieleza
kuwa jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo, haziwezi kufanikiwa iwapo
hali ya amani, umoja na mshikamano vitaondoka.
Alisema kuwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika
hotuba zake amekuwa akikumbusha umuhimu wa kuitunza amani iliyopo na kuitaka
jamii kuijiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kuharibu amani na utulivu wa
nchi.
Hivyo, Mama Shein kwa
upande wake alisisitiza umuhimu wa kuiendeleza amani, na kuwaaasa vijana
kutojiingiza katika vitendo vinavyoweza kuharibu amani.
Akitoa nasaha zake juu
ya matumizi ya mitandao ya kijamii, Mama Shein alisema kuwa ni lazima akinamama
na viongozi wa (UWT) kuwa makini katika matumizi ya mitandao ya kijamii hasa kwa
watoto na vijana kwani ni dhahiri kwamba, baadhi ya vijana hawaitumii vyema
mitandao hiyo na kupelekea kuporomoka kwa maadili na kuathiri utamaduni wa
Kizanzibari.
Katika ziara yake
hiyo, Mama Shein aliwakabidhi kadi 80 kwa wanachama wapya waliojiunga na
Jumuiya hiyo ya (UWT) kwa Wilaya ya Dimani na Mfenesini.
Nae Mama Asha Balozi,
Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kusikitishwa kwake na vitendo vya
ubakaji vilivyokithiri na kusisitiza kuwa nguvu za pamoja zinahitajika ikiwa ni
pamoja na kushirikishwa jamii katika Kamati zilizoundwa kwa makususdi hayo.
Mama Asha alieleza
haja ya kutiliwa nguvu na kauli mbiu iliopo hivi sasa isemayo “Mama mlinde
mwanao na mwana wa mwenzio” na kusisitiza kuwa mtoto kamwe hawezi kulelewa na
mzazi peke yake bali jamii nzima inayomzunguka inalo jukumu hilo.
Nae Mama Fatma Katume
alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa Jumuiya hiyo kujitokeza kwa wingi
kwenda kuchukua fomu za kugombania nafasi mbali mbali za uongozi katika jumuiya
hiyo wakati ukifika tena bila ya woga.
Nae Waziri wa Wizara
ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wawake na Watoto Maudline Castico
aliwaeleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kupambana na vitendo hivyo na kusisitiza
haja ya mashirikiano ya pamoja katika kupiga vita janga hilo.
Nao wanajuiya ya (UWT)
walieleza kufarajika kwao na ziara hizo za Mama Shein na kumsifu kwa uungwana
wake wa kwenda kuwasalimia na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono CCM na kukipa
ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita na kuahidi kuwa ushindi wa chama
hicho utakuwa endelevu katika chaguzi zote zijazo.
Aidha, kwa upande wao
pia walieleza masikitiko yao kutokana na vitendo vya ubakaji.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment