MKE wa Rais wa Zanzibar
Mama Mwanamwema Shein ameeleza kuwa umoja na mshikamano ndio njia pekee ya
kujiletea maendeleo endelevu katika jamii.
Mama Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Ikulu Ndogo Migombani wakati alipofanya
mazungumzo na viongozi wanaounda Umoja wa wake wa Viongozi kwa upande wa
Zanzibar, wakiwemo wake wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge pamoja
na viongozi wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika maelezo yake,
Mama Shein akiwa ndie mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi, aliwakaribisha wake
wa viongozi wa Majimbo yote ya Unguja katika Umoja huo na kueleza kuwa
mafanikio makubwa yamepatikana ndani ya Umoja huo kutokana na mashirikiano
makubwa yaliopo.
Alisema kuwa mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika
kuwaepelekea maendeleo wananchi na kusisitiza kuwa ushiriki wao una nguvu kubwa
katika kuwasaidia wananchi, kuisaidia nchi yao sambamba na kukiimarisha Chama
chao cha CCM.
Nae Mama Asha Balozi,
Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Umoja huo
aliwaeleza wake hao wa viongozi pamoja na viongozi wengine waliohudhuria mkutano
huo umuhimu na malengo ya Umoja huo katika
kuisaidia jamii kwa kushirikiana na Serikali iliyopo madarakani chini ya
uongozi wa CCM.
Mama Asha alieleza
kuwa uongozi wa Chama sio ajira bali ni jukumu katika kuwatumikia wananchi
ikiwa ni pamoja na kuwasaidia katika kuzitatua changamoto wanazozikabili
sambamba na kushirikiana nao katika shughuli zote za maendeleo.
Nao wake hao wa
viongozi wakiwemo viongozi wa Viti Maalum walitoa pongezi zao kwa Mama
Mwanamwema Shein kwa kubuni wazo lake hilo ambalo limeweza kutoa mchango mkubwa
katika kuisaidia jamii katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba pamoja na
kuendelea kukipa ushindi chama cha CCM huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono.
Wakati huo huo, Mama Shein amepokea
fedha taslim kiasi cha Shilingi milioni kumi za Kitanzania, zilizotolewa kwa
lengo la kuuimarisha Umoja huo ili uzidi kuimarika na kuwasaidia wananchi
katika Majimbo yao, fedha hizo ni ahadi iliyotolea na Mwakilishi wa Jimbo la
Uzini Mohammed Raza na wenzake hivi Karibuni huko katika Ukumbi wa Nyumba za
Wazee Sebleni, wakati Mama Shein alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wa Unguja pamoja na viongozi wa Viti Maalum.
Mohamed Raza ametoa
jumla ya Shilingi milioni nne kwa niaba ya familia yake, Amani Makungu ambaye aliwakilishwa
na Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Salim Aljazira, ambaye alikabidhi
Shilingi milioni mbili na Taufiq Salim Turky ambaye ametoa Shilingi milioni
mbili kwa niaba ya familia yake.
Hassan Mohammed Raza nae
alikabidhi Shilingi milioni mbili kwa niaba ya familia ya Mfanyabiashara
maarufu Naushad Mohammed, ambao wote kwa pamoja waliahidi kuendelea kuunga
mkono Umoja huo kwa kuthamini majukumu yake katika kuisaidia jamii pamoja na kuiendeleza
CCM ili iendelee kutekeleza vyema Ilani yake ya Uchaguzi.
Aidha, Mama Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kubwa kwa wapenda maendeleo hao
ambao aliwahakikishia kuwa fedha hizo zitatumika vizuri ili kufikia malengo
yaliokusudiwa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment