Habari za Punde

Korea yaiahidi makubwa Zanzibar



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                     10.1.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Jamhuri ya Korea kupitia Mashirika yake kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Dk. Shein aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokutana na uongozi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (KOICA) ukiongozwa na Makamu wa Rais wa KOICA pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa Seoul Broadcasting System (SBS TV), Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi hizo za Mashirika hayo ya Korea katika kuunga mkono harakati za maendeleo hapa Zanzibar na kueleza kuwa mradi wa skuli ya Kwarara ni wa mwazo katika miradi ya elimu ambayo haijawahi kutokea.

Dk. Shein alisema kuwa Tanzania na Jamhuri ya Korea zilianza mahusiano ya Kidiplomasia mnamo mwaka 1999 ambapo nchi hiyo imeweza kuisaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar mambo mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu, kuimarisha kilimo cha mpunga, kilimo cha umwagiliaji maji na hivi karibuni mradi wa kufuga samaki nao unatarajiwa kuanza.

Katika mradi huo mpya wa kufuga samaki Dk. Sgein alisema kuwa umradi huo utazalisha vifaranga vya samaki na majongoo ya bahari huko Beit-el-Rais mradi ambao utagharamiwa na KOICA.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Korea kupitia mashirika yake hayo kwa ujenzi wa skuli mpya ya kisasa na ya aina yake huko Kwarara inayotarajiwa kufunguliwa kesho (11.1.2016) ambapo alisema hiyo ni ishara ya urafiki kati ya nchin hiyo na Zanzibar.

Nao uongozi wa KOICA umetoa pongezi kwa Dk. Shein kwa mafanikio makubwa yaliofikiwa hapa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Shirika la SBS lilieleza kuwa mikakati yao ni kujenga skuli mia moja katika bara la Afrika na skuli hiyo ya Kwarara ni ya Miamoja kati ya 99 ambazo wamejenga katika nchi nyengine ila kwa upande wa skuli hiyo ni ya kipekee kutokana na kuwa na studio na mambo mengine ya habari, mradi ambao KOICA nao wamesaidia kwa asilimia 50.

Sambamba na hayo, Shirika la KOICA linatarajia kutoa msaada wa dola za Kimarekani milioni 10 ambazo zitapitia kwa Shirika lisilo la Kiserikali la Korea kwa ajili ya kuimarisha elimu ya Sekondari kwa wanafunzi wa kike.

Aidha, Shirika la Good Neighbors Tanzania wamekubali kujenga skuli ya msingi huko Kwarara itakayokuwa na madarasa 24 ambapo tayari eneo la skuli hiyo limeshapatikana.

Pamoja na hayo, KOICA imeahidi kuunga mkono katika miradi mengine mipya itakayoianzisha hapa Zanzibar huku wakitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa mashirikiano mazuri waliyayapata kutoka kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Shirika la SBS TV limeadihi kuitangaza Zanzibar nchini mwao sambamba na kuutangaza utamaduni wa Zanzibar kutokana na vipindi maalum vya Televisheni watakavyovitengeneza ambapo pia uongozi huo ulimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake za kuchapa kazi .

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.