Habari za Punde

MO Dewji akanusha kuzungumza kuhusu pesa za tetemeko la ardhi Kagera


Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji amekanusha taarifa ambazo zimesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa amefanya mahojiano na kituo cha Redio cha Times FM kuhusu pesa zilizochangishwa katika Tetemeko la Ardhi la Kagera lililotokea mwezi Septemba, 2016.

Dewji amesema hajafanya mahojiano na kituo chochote cha habari kuhusu tetemeko la Kagera na habari hiyo haina ukweli wowote zaidi ni mbinu ambayo imetumiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya kuchafua jina lake na kampuni yake ya MeTL Group ambayo mpaka sasa ina wafanyakazi zaidi ya watu 28,000.

Aidha Dewji amesema ana imani na Serikali ya awamu ya tano na kuwatoa hofu Watanzania kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kutumia nusu ya utajiri wake kusaidia watu wenye uhitaji.

“Nitumie nafasi hii kuwajulisha Watanzania wenzangu kuwa hii habari ambayo inasambazwa na watu katika mitandao ni ya uongo na haina ukweli wowote, sijafanya mazungumzo na media yoyote na mimi nilichangia pesa kwa nia nzuri, nina imani na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa inafanya kazi kwa faida ya watu wote bila kufanya ubaguzi,” amesema Dewji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.