Habari za Punde

Wazazi waaswa kuwarudisha watoto waliotoroka Vyuoni (Madrasa)

Na Salmin Juma, Pemba

Wazazi na walezi wa watoto kisiwani Pemba wametakiwa kushirikiana na walimu wa madrasa  kuwashajihisha watoto waliotoroka vyuoni kurejea kwa lengo la kuisoma dini yao na kuifahamu  ili waweze  kukabiliana na changamoto mbali mbali  katika maisha ikiwemo changamoto kubwa ambayo inaonekana kua ni adui wa kila eneo la maendeleo kwa mtoto ambalo ni utandawazi.

Wito huo umetolewa jana na  msaidizi mwalimu Mkuu wa madrasatul Rahman iliyopo Chanjamjawiri Gereji chakechake Pemba Ustadhi  Suleiman Khamis Mohd alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika chuoni hapo kwa lengo la kutazama maendeleo ya madrasa za kiisilamu pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo.

Ustadhi Mohd amesema, hali sasa imekuwa tofauti na zamani  kwani watoto wengi kike na kiume wanapofikia umri wa miaka 15 kujia juu   hutoroka vyoni na badala yake kujikita zaidi na masomo ya kidunia pekee  na wengine  kuzurura  bure mitaani na hatimaye hutumbukia katika matendo maovu  yakiwemo ulevi na mapenzi  katika umri mdogo.

Amesema , changamoto kubwa katika hilo bado wazazi hawajawa na muamko kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu ya dini ya kiislamu  lakini pia inaonekana elimu hii zama hizi imeshushwa hadhi na badala yake watoto huelekezwa katika elimu ya dunia pekee na wanasahau kua elimu ya dini ya kiisilamu ndio elimu itakayowawezesha  kumjua Mola wao kikamilifu na kuishi kwa kujitambua.

Aidha amesema ,licha ya madrasa hiyo kutoa mafunzo ya fani tofauti kwa wanafunzi ikiwemo  sira, hadithi za mtukufu mtume Muhammad SAW, lugha ya kiarabu na kiengereza , lakini pia wanatoa mafunzo ya compyuta kwa wanafunzi waliomaliza mashafu ili kuwajenga kitaaluma  zaidi ya kupambana na mazingira ya ulimwengu wa leo  popote wanapokua.

Ustadh Mohd amefahamisha, licha ya kuwepo kwa juhudi kubwa wanazozichukua kuwasaidia wanafunzi katika madrasa yao  lakini bado  wanakumbana na changamoto kubwa zinazokwamisha juhudi hizo ikiwemo  uhaba wa compyuta na walimu wa lugha ya kiarabu na kiengereza.

Amesema kuwa inafikia hadi compyuta moja kutumiwa na wanafunzi wawili hadi watatu kwa wakati mmoja na  kulazimika kuwagawa wanafunzi hao katika vipindi vitatu tofauti hali inayopelekea ugumu kiasi fulani.

Ametoa wito kwa serikali, taasisi na watu binafsi kujitokeza kusaidia madrasa hiyo kwani wapo kwaajili ya Allah SW hivyo kutoa kwaajili ya Allah kuna kheri kubwa huko tuwendako.

Amemalizia kwa kuwataka wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika vikao vya madrasa sambamba na kuchangia ada kwa ajili ya walimu waliojitolea kufanya kazi hiyo ngumu inayohitaji uvumilivu wa hali ya juu ili kuwatia moyo wandelee kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.