Na ZUHURA JUMA, PEMBA
JESHI la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, limesema mpango
wa kuzisimamia kesi za jinai na kuzipa namba maalum, (Investigation Register),
uliokuwepo kisheria na mwaka 2016 kuutekeleza rasmi, umesaidia kugundua makosa
100 ya jinai.
Kabla
ya Jeshi hilo kuanza kuutumia mpango huo ambao upo kisheria, kwa mwaka jana
waligundua makosa 39 ya jinai, ambayo ndio pekee walioyapa namba za usajili wa
kosa husika ‘IR number’.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi mkoani humo Haji Khamis Haji,
alisema awali Jeshi hilo lilishindwa kutekeleza mpango huo, kutokana na kuhofia
uwingi wa majalada kwa kesi ambazo tayari jamii wameshazifanyia sulhu.
Alisema
kuanzia mwaka 2016, rasmi Jeshi hilo limeamua kila kesi itayofikisha kwao,
kwanza ni kuipa namba maalumu na kuwa nayo kwenye kumbu kumbu za kipolisi, kwa
ajili ya shughuli nyengine.
“Kesi yoyote inayokuja kuanzaia sasa tunaipa namba
‘IR number’ hata kama mwishowe haina na kesi ya kujibu ndani yake, mwaka jana
ilikuwa mpaka tujiridhishe kuwa kuna ushahidi katika kesi husika, ndio tuipe namba,
kwani wananchi huwa na tabia ya kusuluhishana na kupelekea kuwepo mrundikanao
wa majalada”, alisema Kamanda huyo.
Kamanda
huyo alieleza kuwa, sababu nyengine iliopelekea kuongezeka kwa matukio hayo, ni
kutokana na mwaka huu kuwepo na harakati za kupita uchaguzi, ambapo matukio
mengi ya uhalifu hujitokeza.
Alisema
kuwa, makosa ya jinai ya mwaka 2015 ni kesi za kubaka tisa (9), kunajisi tano
(5), uvunjaji kwa dhamira ya kutenda
kosa 10, wizi wa mifugo tatu (3), bangi sita (6) na madawa ya kulevya nne (4).
“Kati
ya kesi zilizopelekwa mahakamani ni 17, zilizopata hatia 17, zinazoendelea
mahakamani tatu (3), zilizo chini ya upelelezi tano (5) na zilizofungwa 14”,
alisema Kamanda
Kamanda
Haji alieleza kuwa, mwaka huu kumeripotiwa kesi za kubaka 23, uvunjaji kwa
dhamiara ya kutenda kosa 47, wizi wa mifugo mbili (2), kupatikana na bangi 15,
kupatikana na madawa ya kulevya 12 na kesi ya mauwaji moja (1).
Kati
ya kesi hizo, zilizopelekwa mahakamani ni 55, upelelezi 26, zilopata hatia 38,
zinazoendelea mahakamani 17 na zilizofungwa 19.
“Kesi
ambazo zimefungwa ni kutokana na ushahidi haukuweza kulinganisha na kosa, hivyo
ni vyema kwa wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi, kwani bila ya
ushahidi hakuna hatia”, alieleza Kamanda huyo.
Alisema
kuwa, ili kesi kupata nguvu na kuweza kupunguza wimbi la matukio ya kihalifu
katika jamii, wanajamii hawanabudi kutoa ushahidi wa kutosha na kuwataka wasichoke kwani hiyo ni haki yao
ya msingi.
Haji
aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi hilo kwa kuyaripoti matukio
yanayotokea katika maeneo yao, ili kuweza kufanikisha kupunguza ama kuondosha
matukio ya kihalifu.
Kwa
upande wa wananchi wa Mkoa huo walieleza kuwa, wamekuwa wakichukua juhudi za
kuwakamata wahalifu na kuwafikisha kituo cha Polisi, ingawa huvunjika moyo wa
kuendelea kutokana na wahalifu hao kuwaona wanaranda mitaani na kuzidisha
uhalifu mara dufu.
“Wahalifu
hata tukiwapeleka wanatolewa na wakija mitaani huzidisha uhalifu, hivyo tumechoka
na kupelekea baadhi ya wananchi kujichukulia hatua mikononi mwao, kwani wanaona
haki haitendeki”, walisema wananchi hao.
Wananchi hao waliliomba Jeshi la Polisi
kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu, ili nao kuweza kupata nguvu ya
kuyaripoti matukio hayo pale yanapotokea, jambo ambalo litaweza kuondosha
matatizo katika jamii
0 Comments