Habari za Punde

Serikali Haina Mpango Kulibinafsisha Zao la Karafuu -Dk Shein.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba                                                                                                                04.04.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewaeleza wananchi kisiwani Pemba kuwa kamwe Serikali anayoiongoza haina mpango wa kulibinafsisha zao la karafuu na badala yake imeweka mipango kabambe ya kuliimarisha na kupambana na wale wanaouza zao hilo kwa njia ya magendo.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kukizindua kituo cha ununuzi wa karafuu kilichopo Ngomeni na kuangalia mradi wa upelekaji umeme na ujenzi wa kituo cha afya pamoja na skuli ya Msingi miradi ambayo yote ipo katika kijiji hicho cha Ngomeni.

Dk. Shein alisema kuwa zao la karafuu litaendelea kuwa chini ya Serikali na jitihada za kuliendeleza zitaendelea kuchukuliwa ikiwa ni kuendelea kuwapa  wakulima wa karafuu bei nzuri na kulinda ubora wa zao hilo katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wa bei ya karafuu Dk. Shein alisema, bado Serikali itaendelea kununua kilo moja kwa shilingi 14000/=, ambapo alisisitiza kuwa bei hiyo haitoshushwa na wajibu wa serikali ni kutafuta soko zuri popote duniani.

“karafuu ndio uhai wao serikali, bado inaendelea kulienga enga ili historia ya Zanzibar na karafuu iendelee kuhimili katika kuwaendeleza wananchi”.

Aidha, aliwataka wakulima kuacha kuziuza karafuu kwa njia ya magendo na badala yake waziuze katika  Shirika la ZSTC ili wananchi waweze kupata maendeleo bora pamoja na maendeleo ya nchi kwa jumla .

“Magendo sio mazuri ndio maana tunapambana nayo, na mwaka huu Serikali itazidi kasi kuliko miaka iliyopita, ukiuza karafuu serikali utapata faida mara mbili, utapata wewe muuzaji pamoja na Serikali kwa jumla”alisema.

Akizungumza kuhusu azma ya Serikali ya kujenga Vituo  vya Karafuu  Dk. Sheina, alisema kuwa nia ya Serikali kujenga vituo vya kununulia Karafuu ni kuimarisha hadhi za wanyonge katika kuuza karafuu zao huku akiwahakikishia wananchi kwua huduma zote muhimu zitakuwepo katika vituo hivyo.

“Katika vituo hivi ZSTC itaweka maji ya kunywa, chai, tende, halua na hata biskuti huku mkiwa mmekaa kwenye viti mkiuza karafuu zenu na kwamwe hamtokopwa hata ukija na magunia kumi utauza na kupewa pesa zake zote hapo hapo”,alisema Dk. Shein

Dk. Shein aliongeza kuwa upelekaji wa maendeleo hayo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015/2020, katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kama chama hicho kioivyotoa ahadi wakati wa uchaguzi.

Wakati huo huo, Dk. Shein ameitaka Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha    wanafanya kazi kwa uhakika na kuhakikisha miezi mitatu ijayo kituo cha Afya Ngomeni kiwe kimeshamaliza ujenzi wake.


Hatua hiyo imekuja baada ya Dk Shein kutokuridhishwa na mwendo wa Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya, kwa kushindwa kumalizika ujenzi wake kwa wakati muwafaka kama aliyotoa agizo lake Novemba mwaka jana.

“Nilipotembelea kijiji hichi cha Ngomeni Novemba mwaka jana, niliagiza ZSTC kujenga kituo cha kununulia karafuu, ZECO kupeleka umeme, Wizara ya Afya kujenga kituo cha afya na vyote nilitoa miezi mitatu tu kazi iwe imemalizika, Mawasiliano nikawapa mwaka mmoja kwa ajili ya ujenzi wa barabara”alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliitaka Wizara hiyo ya Afya kukaa kwa pamoja na kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika ndani ya muda wa miezi mitatu, ili Julai aende akikifungue rasmin.

Alisema wananchi wa Ngomeni wanahitaji kituo cha afya kwa lengo la kuwapunguzia masafa ya kufuata huduma hiyo katika kijiji cha Mgelema ambacho kiko masafa ya mbali yapatayo Kilomita 4 kutoka kijijini hapo.

Nae Waziri wa biashara Viwanda na masoko Zanzibar Mhe:Balozi Amina Salim Ali, alisema mikakati ya ZSTC ni kupeleka maendeleo vijijini na kuondosha wimbi la Umaskini kw awananchi.

Alisema Serikali imejipanga vizuri, kuhakikisha sheria ya karafuu inafanyiwa mabadiliko na kutiwa makali zaidi, ili kuhakikisha suala zima la magendo ya karafuu kwa Zanzibar linakuwa historia.

Alisema Serikali imetoa silimia 80% ya bei iende kwa wakulima, na asilimia 20% inaenda serikalini na hyo wananchi wananufaika nayo kwa kuwa pelekewa huduma mbali mbali muhimu.


Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanayaitunza maendeleo waliyopatiwa na serikali yao.

Katibu mkuu Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar, Bakari Haji alisema kuwa kituo cha Mgelema na Ngomeni vimegharimu jumla ya shilingi Milioni 160 hadi kukamilika kwake.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa skuli ya Ngomeni, Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba, Salum Kitwana Sururu, alisema ujenzi huo umegharimujumla ya shilingi Milioni 31,258,640/=.

Nae Meneja wa shirika la Umeme Zanzibar ZECO, Hassan Ali Mbarouk, alisema jumla ya Tsh. Milioni 178,142,791/= zimetumika katika kazi za upelekaji wa umeme katika kijiji cha Ngomeni, chenye wakaazi 500.

Dk. Shein pia, alifika Mgelema na kukizindua kituo cha ununuzi wa karafuu na baada ya hapo alifanya ziara ya kukagua mradi wa barabara ya Ole-Kengeja kupitia Pujini mpaka Ole Muhogoni, Kiziwamaji na kupata maelezo mafupi.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822  
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.