Habari za Punde

Katibu tawala mpya Mkoani aomba kuungwa mkono

Na.Haji Nassor. Pemba. 
KATIBU Tawala mpya wa wilaya ya Mkoani Pemba, Miza Hassan Faki, amewaomba viongozi wa wilaya hiyo, pamoja na mkoa wa kusini Pemba, kumpa kila aina ya ushirikiano, ili atimize majukumu yake, kwenye nafasi hiyo.
Alisema, kama viongozi wenzake hawakumpa ushirikiano, kumkosoa, kumuelekeza na kumuonyesha njia za kutekeleza majuku yake, kamwe lengo la kuwahudumia wananchi wa wilaya hiyo hatolifikia.
Katibu tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, akila kiapo cha kushika nafasi hiyo.
Katibu Tawala huyo, alieleza hayo ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, muda mfupi mara baada ya Mkuu wa mkoa huo Mwanajuma Majid Abdallah, kumuapisha kushika majukumu yake, kufuatia uteuzi wake uliofanya na rais wa Zanzibar Juni 19 mwaka huu.
Alisema, yeye ni mdogo kiumri, elimu na anaouzefu mdogo kwenye uongozi, hivyo kwa kiasi kikubwa anawategemea viongozi hao, ili afanikishe vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwenye nafasi yake hiyo.
“Mimi bado mdogo kwenye uongozi jamani, sasa lazima mnishauri, mnielekeze, mniambie na muniite mkiona naenda kombo, mkifanya hivyo lengo la Rais kuniteua litafikiwa”,alisema.
Mapema Mkuu wa Mkoa huo, Mwanajuma Majid Abdalla, alisema rais hakukosea kumteua Katibu tawala huyo, kutokana na umahiri wake kwenye kazi.
Alisema, kwa vile anamfahamu vyema Katibu tawala huyo, anaamini hakutakuwa na kazi kubwa ya kumuelekeza kwenye nafasi yake hiyo mpya.
“Mimi naamini, mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, hatokuwa na kazi kubwa sana kwa Katibu tawala wake, maana anaweza na anafundishika”,alieleza.
Kwa upande wake, Katib Tawala Mkoa wa Kusuini Pemba Yussuf Mohamed Ali, alimtaka Katibu tawala huyo wa wilaya ya Mkoani, kubisha hodi kila mara kwenye ofisi yake, ikiwa atahitaji maelekezo.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, alimueleza Katib tawala huyo, kukubali kufundishwa, kuelekezwa na kukosolewa, ikiwa ni njia moja wapo ya kuelekea mafanikio.
Aidha Hemed, alimueleza Katibu huyo, kwa vile anaongoza jamii kubwa ya watu, ajue kuwa, atakumbana na vikwazo, makero, shida, watu kutomkufahamu ingawa yote hayo ni sehemu ya uongozi.

Rais wa Zanzibar na Mwneyekiti wa baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe: dk Ali Mohamed Shein, kwa kutumia kifungu cha 15 (1,2,na 3) sheria no 8 ya mwaka 2014 ya Tawala za Mikoa alifanya utezi wa viongozi mbali mbali, akiwemo Katibu tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.