Habari za Punde

Maonesho ya Nanenane 2017 Kitaifa Kufanyika Lindi Kuanzia Kesho.

Na Mathias Canal, Lindi
Maonesho ya Kilimo (NaneNane) yanataraji kuanza kesho Agosti 1, 2017 kote nchini kwa ngazi mbalimbali za kanda huku Maonesho hayo Kitaifa yakifanyika Mkoani Lindi huku Maandalizi na maonesho ya  Ki-Kanda yanaratibiwa na uongozi wa  mikoa husika.


Maandalizi ya Maonesho ya 24 ya kilimo na sherehe za Nanenane yatafanyika kwa siku 8 ambapo Kitaifa yatafika ukomo jioni ya Agosti 8, 2017 katika Viwanja vya Ngongo na Maeneo mengine yatakapoadhimishwa kikanda  katika  viwanja vya maonesho ni John Mwakangale –Mbeya; Mwalimu J.K. Nyerere –Morogoro; Themi – Arusha; Nzuguni -  Dodoma; Nyahongolo – Mwanza; na Fatuma Mwassa - Tabora. 


Maonesho ya mifugo sanjari na Maonesho ya Kilimo hutoa changamoto ya kuleta mapinduzi katika Ufugaji, Uvuvi, na Kilimo na kutoa ajira hususani kwa vijana kuwaongezea zaidi kipato na kuondoa umasikini. 


Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg Mathew Mtigumwe wakati akizungumza na Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com  kueleza muktadha wa Maonesho hayo ambayo Kitaifa yanafanyika Mkoani Lindi na kubebwa na kauli mbiu mahususi kwa mwaka huu 2017 isemayo "Zalisha kwa Tija Mazao ya Bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati" 


Mtigumwe ameuambia Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com kuwa Wizara, taasisi/Makampuni ya umma na binafsi, Mabenki na wadau wote wa kilimo na mifugo wataendelea kuwasaidia wakulima na wafugaji hapa nchini ili kuongeza uzalishaji kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyokusudiwa kuanzishwa.

Malengo ya maonesho hayo ni utoaji elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, mashirika ya umma na binafsi.

Teknolojia/Bidhaa zitakazooneshwa ni pamoja na zana za Kilimo, Mbegu bora za mazao mbalimbali, Uzalishaji wa mazao katika mazingira yaliyodhibitiwa ambapo piaTaasisi za kitafiti ambazo zitaonyesha teknolojia mbalimbali za kuongeza tija zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali, Utengenezaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, Uboreshaji wa viasilu ili kupata mifugo na mazao ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa kutokana na maeneo walipo wananchi wanaohitaji kujihusisha na ufugaji na kilimo na udhibiti wa magonjwa.

Pia uzalishaji bora wa mazao ya nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa mayai, Kuongeza thamani mazao ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, ambapo Taasisi za elimu zitaonyesha ubunifu wa kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji wakubwa na wadogo wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.

Maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane yohusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki, Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali yalifunguliwa tarehe 03 Agosti 2016 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe.


Sikukuu ya wakulima inayofahamika kuwa Nanenane ina sherekewa nchini kote tarehe 8 Agosti kila mwaka. Sherehe hiyo inatayarishwa na kuratibiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuhusisha Taasisi, Wizara na mtu mmoja mmoja wanaoshughulika na kilimo.

Miaka ya 1990 sherehe hizi zilikuwa zikifanywa tarehe saba Julai kila mwaka na kuzingatia mafanikio makubwa na changamoto zinazokabili sekta ya kilimo inayowashirikisha wadau wote kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.Ambapo Lengo la serikali likawa kuitumia Saba Saba kama siku ya maonyesho ya biashara ya kimataifa, ambapo wafanyabiashara wengi walijitokeza ama hujitokeza kuonyesha bidhaa zao wanazozalisha na siyo kuwafundisha Watanzania mbinu za kuzalisha biadhaa hizo.
Picha zaidi zinaonyesha maandalizi ya Maonesho ya Nanenane katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.