Habari za Punde

Kikosi cha KMKM Kisiwani Pemba Wakama Mzigo Unaodhania kusafirishwa Kwa Magendo.

Na.Salmin Juma Pemba.
Raia wanne wa Kenya wamekamatwa na kikosi Maalum cha KMKM Kamandi ya Pemba wakiwa na magunia ishirini  (20) ya nazi ambazo walikuwa wakiingiza nchini bila ya kufuata taratibu za kulipa kodi.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Wete , Kaimu Kamanda wa KMKM Kamandi ya Pemba , Luteni Kamanda Hassan Hussein Ali amesema wakenya hao wametiwa mikononi na KMKM katika bandari ya Kichungwani Ungi Shehia ya Msuka Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema Mzigo huo  ulikuwa ndani ya chombo kinachofahamika kwa jina la Mdodoki huku kikiwa hakina namba za usajili na kilikuwa na mahabaria watano wanne ni Raia wa Kenya na Mmoja ni Mtanzania ambaye anaishi Mkoa wa Tanga na kilikuwa kinatoka Mombasa Kuja Pemba.

“Askari wa KMKM katika Kambi ya Msuka wakishirikiana na wenzao wa Kambi ya Tumbe wamefamikiwa kukamata chombo hicho chenye jina la Mdodoki kilichokuwa kinatoka Mombasa kuja Pemba kikiwa na magunia ishirini ya nazi ”alieleza.

Aidha Kaimu Kamanda wa KMKM Pemba ambaye pia ni Mkuu wa Operesheni wa kikosi hicho  amesema kuwa katika tukio hilo pia wamekamata marobota kumi na moja ya nguo za vitambaa ambayo nayo yalikuwa yanaingia nchini bila ya kulipiwa ushuru.

“Wahusika wa Marobota haya walidhamiwa na Sheha wa Shehia ya Tumbe lakini mizigo yao iko kituoni ambapo taratibu za kisheria zinafuatwa ”alifahamisha.

Mmoja wa Mabaharia hao Mohammed Mwasemi Asiran ameeleza kwamba walilazimika kutia nanga katika bandari hiyo baada ya chombo chao kuharibika jambo ambalo pia liliwalazimu kuutosa baharini baadhi ya mzigo yao.

Amesema mzigo huo walikuwa wanaupeleka katika soko la Qatar lililoko Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusuni Pemba  na kukiri kwamba walikuwa bado hawajafuata taratibu kisheria.

Amesema wakiwa ndani ya chombo kuelekea katika bandari ya Wesha , chombo chao kiliharibika na kulazimika kutia nanga katika bandari ya Kichungwani ili kuhami usalama wa maisha yao na kujikuta wakiwa nchini ya ulinzi wa KMKM.

“Vibali tunavyo lakini tulikuwa bado hatujalipia kwani safari ilikuwa inaendelea kuelekea katika bandari ya Wesha na mzigo huu tulikuwa tunaupeleka katika soko la Qatar, tuliharibikiwa na kulazimika kuweka nanga katika eneo la Kichungwani ”alieleza.

Ameongeza kwamba baada ya kuharibikiwa na chombo walilazimika kuipunguza mizigo yao kwa kuitosa baharini ili kunusuru usalama wa maisha yao ambapo jumla ya magunia tisa ya nazi waliyatosha baharini.

Mabaharia wengine ambao wamekamatwa na KMKM ni Hassan Omar Koja 58, Othman Omar koja 33, Omar Bakar 45 wote ni Raia wa Kenya pamoja na Mussa Omar Ambulue 75 Mkaazi Mkoa wa Tanga .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.