STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba
24.08.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, ameutaka uongozi wa Mkoa
wa Kaskazii Pemba, Wilaya ya Micheweni na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo
na Uvuvi zishirikiane katika kuhakikisha soko la Tumbe linaanza kutumika ndani
ya miezi miwili.
Dk. Shein aliyasema hayo katika hotuba yake ya
majumuisho aliyoitoa baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa
Kaskazini Pemba, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA), huko Mchangamdogo.
Dk. Shein alisema kuwa iwapo itashindikana basi
wapeleke Serikalini mapendekezo juu ya matumizi mbadala ya soko hilo kwa hapo
baadae.
Soko hilo limejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Mradi wa MACEMP na kuzinduliwa na Rais Dk. Shein mnamo mwaka
2015 na kutoa huduma kwa kipindi cha miezi miwili tu na baadae kusita kutumia
hadi hivi leo.
Kusita kwa soko hilo kunatokana na mivutano
iliyopo kati ya wananchi na taasisi zinazosimamia soko hilo.
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pia,
imetakiwa kufanya uwamuzi wa haraka sana wa kuwaajiri na kuwapeleka Pemba
vijana wanaomaliza masomo yao katika Chuo cha Kilimo Kizimbani, ili kutatua
tatizo uhaba la bibi shamba na bwana shamba.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimtaka Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba na Mkuu wa Wilaya ya Wete na Micheweni wapite katika skuli kwa
kushirikiana na Wakaguzi wa Elimu wa Wizara ya Elimu ili kuwachukulia hatua za
kinidhamu walimu watoro.
Dk. Shein pia, aliipongeza Wizara ya Afya kwa
kujenga benki ya damu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba na kutoa agizo kwa Wizara
kuwa makini katika suala hilo nyeti sana katika kuanishwa na kuiendesha benki
hiyo ya damu iwapo haitajiandaa vizuri na kuwa waangalifu na waadilifu lengo
hilo halitofanikiwa.
Wizara ya Afya pia, ilitakiwa kununua mashine
‘ultrasound’ kwa ajili ya matumizi ya huduma za wajawazito kwenye kituo cha
Junguni na vituo vyengine vitano vitakavyojengwa katika maeneo mengine ya
Unguja na Pemba.
Kwa upande wa jukumu la wanaCCM, Dk. Shein ambaye
pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amewataka wanaCCM kudumisha umoja na
mshikamano, kuandaa utaratibu mzuri wa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya
Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020 pamoja na kuyatumia matawi kwa ajili ya
kuimarisha chama.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein aliupongeza
uongozi wa Mkoa huo kwa juhudi unazoendelea kuchukua katika kuimarisha hali ya
usalama katika Mkoa huo ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za
kiuchumi na kijamii kwa amani na utulivu.
Dk.Shein aliitaka Ofisi ya Mkoa, Wilaya ya Wete
pamoja na Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira kushirikiana katika
kufanya maandalizi madhubuti ya kufanikisha uzinduzi wa umeme kwenye Kisiwa cha
Fundo huku akiipingeza Wizara hiyo kupitia ZECO kwa kuupeleka umeme kisiwani
humo.
Ofisi ya Mkoa na Kamisheni ya Ardhi nayo ilitakiwa
kuendeleza mikakati ya kukabiliana na matatizo ya ardhi ikiwa I pamoja na
kushughulikia suala la uvamizi katika eneo la skuli ya Chimba.
Kwa upande wa Sekta ya Michezo, Dk. Shein aliutaka
uongozi wa Mkoa na Wilaya ya Micheweni kushirikiana na Wizara ya Habari,
Utalii, Utamaduni na Michezo katika utekelezaji wa uwanja wa michezo Micheweni
kwa haraka iwezekanavyo.
Aidha, Dk. Shein alitoa agizo na kutaka Mkuu wa
Mkoa huopamoja na RPC wa Mmkka huo wa Kaskazini kuwa wahusika wote wa tukio la
tarehe 21 Agosti mwaka huu kuhusiana na dawa za kulevya watafutwe na kupelekwa
katika vyombo vya sheria na kutaka ndani ya wiki mbili jambo hilo likamilike.
Pia, aliutaka Mkoa kupitia Baraza la Mji la Wete
na Halmashauri ya Wilaya ya Miheweni wasimamie usafi na sheria za mipango miji
katika kuyaimarisha mazingira ya miji
Kwa upande wa zao la karafuu, Dk. Shein
alisisistiza haja ya kuendeleza jitihaza za kukabiliana na magendo ya karafuu
na Serikali itafanya kila linalowezekana katika kupambana na watu wanaoendesha
hujuma dhidi ya zao la karafuu.
Aidha, alilitaka Shirika la ZSTC kuwa makini
katika kulishughulikia zao la karafuu katika uchumaji, ununuzi, uuzaji nje ya
nchi huku likihakikisha kuwa wakulima wa karafuu hawapati usumbufu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment