Habari za Punde

Mzee wa Miaka 65 Akijiunga Katika Darasa Kujifunza Kusoma Kisiwani Pemba.

Na.Haji Nassor. Pemba.
Mwalimu Mkuu na waalimu wengine wa skuli ya Tumbe sekondari wilaya ya Micheweni Kisiwani, umeshindwa kuamini macho yao hapo juzi, baada ya mzazi Salama Khamis Hamad (65) kutinga skulini hapo kufuatilia iwapo wajukuu wake wamehdhuria masomo.
Waalimu hao wakiwa katika maonyesho ya maktaba yalioandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, ghafla mzazi huyo alifika mlangoni mwa darasa lililokuwa na maonyesho hayo, na kuwauliza wajukuu wake.
Mama huyo ambaea aliwaacha midomo wazi ya waalimu na wageni wengine kwa ukakamavua na ujasiri wake, yeye kubwa alitaka kuonyeshwa wajukuu wake wawili iwapo wamefika skulini hapo.
Mwandishi wetu aliekuwepo skulini hapo, alielezwa na mama huyo kuwa, amekuwa akipokea taarifa kwa baadhi ya wanafunzi, kuwa wajukuu wake wamekuwa wakiishia vichakani na hawaingii darasani.
Alisema alichokifuata skuli hapo sio jengine bali ni kutaka kujua iwapo wajukuu wake wako darasani na wanaendelea na masomo.
“Mimi nilichokifuata skuli ni kutaka kujiridhisha iwapo wajukuu wangu wapo, maana mimi nahangaika kwa wao mchana mzima, sasa kama hawapo nijuwe vya kufanya”,alisema.
Mlezi huyo mwenye wajukuu wanaosoma dara la kumi na la tisa skulini hapo, alisema yeye hakubali kuona wajukuu wake, wanapuuza masomo kwa vile anajua kuwa aliesoma na mwengine ni tofauti yao.
Katika hatua nyengine mzazi huyo, alisema wakati umefika kwa wazazi wenzake, kutowatwika mzigo wa  waalimu peke yao, lazima na wao wawe bega kwa bega katika kumtafutia maendeleo ya mtoto.
“Huyu mtoto akishasoma na kupata kazi, hata mwalimu wake hamjui tena, sasa lazima sisi wazazi tuwahimize na kuwafuatilia watoto, maana ni wajanja na wakorofi”,alifafanua.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Nassor Bakar Said, alisema ujasiri wa mlezi huyo pamoja na umri wake, umewatia moyo sana katika kazi zao.
Mwalimu mkuu huyo, alisema inawezekana mikutano walioifanya hivi karibuni ya kuwataka wazazi wafuatilie masomo ya watoto wao yameanza kuzaa matunda.
“Hivi karibuni tulifanya mikutano katika kijiji cha Raha kesho shehia ya Tumbe, sasa wazazi pengine wameanza kufuatilia mahudhurio ya watoto wao, sisi twamshukuru”,alifafanua.
Hata hivyo Mwalimu mkuu huyo, aliwataka wazazi wengine kuiga mfano wa mzazi huyo, maana waalimu hawana muda wa kuwafuatilia watoto vichakani.
Baadhi ya wadau wa elimu wa kijiji cha Tumbe, walisema mafanikio ya wanafunzi yanahitaji nguzo tatu, akiwemo mazizi, mwalimu namwafunzi mwenyewe.
“Mimi kwa kweli hadi sasa siamini, kuwa umri alionao yule bibi, lakini kuacha kazi zake na kufika skuli na kufautilia maendeleo ya wajukuu zake, ni mfano hai na mzuri”,alisema Hamad Faki Hamad.
Nae Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria ZanzibarZLSC tawi la Pemba, Siti Habib Mohamed, alisema amevutiwa sana na umahiri na umakini wa mzazi huyo.

“Mimi sijawahi kuona wala kusikia mzazi anaefuatilia maendeleo ya watoto wake skuli, maana hata ukimuona mzazi basi ujue skuli kuna kikao au kaitwa kwa matatizo ya mtoto wake, lakini kwa huyu kafanya jambo jema na la kuigwa”,alisema.Hata hivyo badhi ya wanafunzi wa skuli hiyo, walisema ni kweli wapo baadhi yao huaga nyumbani kwamba wanakwenda skuli, ingawa matokeo yake huishia kwenye vichaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.