Habari za Punde

Rais Dk Shein aitaka ZBC kujiendesha kibiasharaSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                 09.08.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja kwa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kujiendesha kibiashara ili lizidi kuimarika sambamba na kutekeleza azma ya kutoa elimu kwa umma.

Dk. Shein alieleza hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Uongozi wa Shirika hilo katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa lazima Shirika liendeshwe kibiashara kwa lengo la kuweza kupata faida ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zinazopaswa kutolewa malipo zisitolewe bure ili Shirika hilo liweze kujiimarisha vyema.

Dk. Shein, aliongeza kuwa lengo na madhumuni ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kulibadilisha Shirika hilo na ndio maana juhudi kubwa zimechukuliwa katika kufikia lengo lililokusudiwa na hivi sasa limeanza kupata mafanikio na hasa pale baada ya kufanya ziara zake katika kituo cha Redio na Televisheni na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kuona mafanikio yaliopatikana.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa kwenye vyombo vya habari vya redio na televisheni katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ambapo iliweza kujijengea sifa kubwa na kupelekea wahusika wa kada hiyo kutoka nje na ndani ya nchi waje kujifunza hapa Zanzibar.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa mabadiliko katika Shirika hilo na kueleza kuwa Shirika haliwezi kufanya vizuri iwapo hakutakuwa na mabadiliko. Hivyo, aliungana na viongozi wengine katika kikao hicho kwa kulipongeza Shirika la ZBC pamoja na uongozi wake ukiwemo uongozi wa Wizara kwa kuonesha mabadiliko ya kweli huku akisisitiza suala zima la uzalendo,mashirikiano na mapenzi miongoni mwao.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa vitegemezi vya uchumi wa Zanzibar ni karafuu na ndio maana Serikali anayoiongoza baada tu ya kuingia madarakani ikalipa kipaumbele zao la karafuu kwa kupandisha bei ya zao hilo, hivyo alilitaka Shirika la ZBC kuwa mstari wa mbele kulitangaza zao la karafuu.

Aliongeza kuwa lengo kubwa la Shirika hilo ni kutoa elimu kwa umaa kupitia televisheni na redio, hivyo ni vyema likawaelimisha wananchi juu ya zao la karafuu na kusisitiza haja ya mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji wa Shirika hilo.

Alieleza kuvutiwa kwake na jitihada za ZBC katika kuandaa vipindi vipya vya redio na televisheni sambamba na ubunifu ulioanzishwa na Shirika hilo katika kubuni vipindi mbali mbali vya kuelimisha, kufunza na kuburudisha.

Mapema Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi kwa kazi nzuri inazozifanya Shirika hilo sambamba na juhudi inazozichukua kutoka katika mfumo wa analogi kwenda digitali.

Nae Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alieleza aliahidi kuwa ZBC itaendelea kusimamia juhudi za Dk. Shein ya kuhakikisha Shirika hilo linaimarika huku akieleza kuwa ZBC ina dhima ya kuonesha na kutangaza vipindi vya maendeleo mbali mbali likiwemo zao la karafuu.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Chumu Kombo Khamis alieleza haja kwa Wawakilishi kisiwani Pemba kulitumia vyema Shirika la ZBC kwa kueleza mambo wanayoyafanya.
 
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza haja ya kuandaliwa mapema mpango wa kuwapata wataalamu katika Shirika hilo hasa ikizingauiwa kuwa baadhi ya wataalamu wamekuwa wakistaafu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZBC, Bi Nasra Mohammed alieleza mafanikio na changamoto za ZBC huku akieleza juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Bodi yake ya kufanya ziara katika vituo mbali mbali vya televisheni pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika hilo wanaofanya kazi zao  mjini Dar-es-Salaam.

Nao uongozi wa ZBC ulitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia mitambo ya kisasa, kubadilisha haiba ya studio za ZBC Radio, mafanikio ambayo yameoneshwa na Dk. Shein katika umahiri wake wa kutimiza lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Aliongeza kuwa ZBC imeweza kununua (sever) ili kuhifadhi hotuba za viongozi wa kitaifa, nyimbo za zamani katika mfumo wa kisasa na uhifadhi uliobora zaidi huku akieleza kuwa ZBC Radio kwa sasa imeweka website (www.zbc.co.tz) kwa majaribio na hadi sasa jumla ya wasikilizaji 8000 wanasikiliza ZBC Redio kupitia njia hiyo.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) na uongozi wake na kupongeza mafanikio yaliofikiwa katika kipindi kifupi tokea kuundwa kwa cha Taasisi hiyo.

Nae Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Ali Abeid Karume alieleza umuhimu wa kuundwa kwa taasisi hiyo ambayo itasaidia katika kusimamia viwango vya bidhaa zinazozalishwa ama kuingia Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuwalinda watumiaji.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Ali Seif Mshimba alieleza kuwa madhumuni makubwa ya shughuli za ZBS ni kulinda afya na usalama kwa watumiaji wa bidhaa na huduma, kuhifadhi mazingira ya nchi na kushajiisha ukuaji uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora viwandani na kilimo na biashara ya kimataifa.

Alieleza Dira ya ZBS kuwa ni kufikia kuwa miongoni mwa Taasisi za Viwango Duniani katika kuweka viwango na kutoa huduma za udhibiti, ubora na vipimo vinavyokubalika na kuheshimika.

Nao uongozi wa ZBS ulieleza kuwa jumla ya kampuni 24 zimewasilisha maombi ya kutumia alama ya ubora ya ZBS ambapo bidhaa 31 zimeombewa matumizi ya alama ya ubora na 10 zimepewa cheti cha matumizi ya alama ya ZBS ambapo kati ya hizo 6 za ndani na 4 za nje ya nchi na bidhaa 21 zinaendelea na hatua za kuthibitishwa ubora.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.