Habari za Punde

Uongozi wa Hospitali za Serikali Wapewa Mafunzo ya Huduma Kwa Wateja.

Naibu Waziri wa  Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akifungua mafunzo ya siku moja kwa walinzi wanaolinda Hospitali za Serekali na kuwataka wawe wakarim katika kutoa huduma.
Mkurugenzi Utawala na Uendeshaji wa Hospitali ya Mnazimmoja Abubakar Khamis Hamadi akitoa maelezo ya mafunzo yakuwajengea uwezo zaidi walinzi wanaolinda Hospitali, mafunzo hayo yamefanyika Hospitali ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Baadhi ya walinzi katika mafunzo wakifuatilia hutuba ya NAIBU Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said hayupo pichani.
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman katika picha ya pamoja na walinzi wanaolinda Hospitali za Serekali.(Picha na Makame Mshenga)

Na Maryam Kidiko - Maelezo Zanzibar.                              
NAIBU  Waziri wa  Afya Harusi Said Suleiman amewataka Walinzi  wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kubadilika  katika utendaji wa kazi zao ili kuongeza mashirikiano kati yao na  wananchi wanaokwenda kwa ajili ya  kupata huduma mbali mbali katika hospitali hiyo  

Hayo aliyasema katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwenye Mafunzo ya Siku moja ya Walinzi wa Hospitali hiyo ambayo  yanalengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi zao na kuongeza   Mashirikiano na wateja wao.

Aliwaeleza walinzi hao kuwa kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya walinzi wamekuwa wakitumia lugha mbaya kwa wagonjwa na wananchi wanaofika kuangalia wagonjwa wao jambo ambalo sio zuri.

Aliwasisitiza walinzi wa Hospitali ya Mnazimmoja kutumia lugha nzuri kwa Wagojwa kwani kufanya hivyo itapelekea kujenga mashirikiano  katika utendaji mzima wa kazi yao.

Alisema kunatofauti  kubwa kati ya ulinzi wa Hospitali na ulinzi katika sehemu nyengine kwani mara nyingi wananchi wanaofika Hospitali wanahitaji kuhurumiwa kutokana na mazingira wanayokuwa nayo.

“Walinzi wetu tunawaamini sana na tunajuwa mnakumbana na changamoto nyingi lakini ni lazima mtumie akili za ziada ili Wagojwa wanapofika  wajiskie furaha hatakama wapo katika huzuni,”Alisema Naibu Waziri.

Hata hivyo alishauri zinapotokea Changamoto ndogo ndogo kuzishughulikia  kwa njia nzuri za ushirikiano  kwa pande zote zinazohusika .

Aidha aliwaeleza walinzi hao kuwa  baada ya kupata mafunzo hayo Serikali haitawavumilia kuona wanaenda kinyume na utaratibu uliowekwa katika kuwahudumia wananchi.

Mkurugenzi Utawala na Uendeshaji wa Hospitali ya Mnazimmoja Abubakar Khamis Hamadi  alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza mashirikiano mazuri kati ya Wagojwa, wananchi wanaofika kwa ajili ya kuangalia wagonjwa na Walinzi.

Alieleza matumaini yake kuwa mafunzo hayo yatawawezesha Walinzi kujuwa njia sahihi za  kuwashuhulikia wateja wao  wanapofika katika Hospitali na kujuwa wajibu wao.

“ Tunapata malalamiko mengi kutoka kwa Wagojwa hivyo tumeamuwa kutowa mafunzo hayo kwa Walinzi ili kuondoa  matatizo na  kuongeza mashirikiano mazuri baina yao,” alisema Mkurugenzi huyo.

Aliwataka walinzi waliopata mafunzo hayo kuyafanyia kazi ili  kutimiza lengo la mafunzo yenyewe na kuleta ufanisi katika kazi yao bila kutokea malalamiko mengine.

Mkurugenzi Abuubakar amewaomba Wananchi wanaofika hospitalini hapo kutowa mashirikano mazuri kwa Walinzi na iwapo litatokezea tatizo wafike katika kitengo cha huduma kwa Mteja kwa lengo la kushughulikiwa.

Msaidizi Mkuu wa Walinzi Aboubakar Hassan Bakari aliahidi baada ya mafunzo hayo watabadilika na kuwashauri walinzi wenzake kuwa waadilifu huku wakijua wao ni kampuni ya ulinzi ya Kibiashara hivyo wanatakiwa kuvutia waajiri wao.

Mmoja wa Walinzi waliopata mafunzo hayo Mwanaidi Mriha Nasibu alishukuru kupata mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kutatuwa Changamoto zilizopo baina yao na Wagojwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.