Habari za Punde

Wakulima wa karafuu wajawa na matumaini tele

NA HAJI NASSOR, PEMBA
WAKULIMA na wananchi waliokodia mashamba ya mikarafuu kisiwani Pemba, wamesema kutokana na msimu wa mwaka huu kuwa wa aina yake kutokana na mzao kunongoka, wanamatumaini makubwa ya kufanikisha malengo yao ya kimaendeleo.
Walisema wanatarajia kukuza na kuendelea biashara zao, mara baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka huu wa uvunaji na uuzaji wa zao hilo la taifa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari kwa nyakati tofauti, walisema kwa vile msimu ni mkubwa kuwahi kutokea kama miaka kumi (10) sasa iwapo bei ya shilingi 14,000 itaendelea wanatarajia kupata mafanakio mazuri.
Mmoja kati ya wakuli hao mkaazi wa Toroni wilaya ya Mkoani Mwantatu Zubeir Mjaka, alisema karibu misimu mitatu alikuwa hajawi kufunga biashara zake mjini Unguja, ingawa mwa msimu huu unavyotarajiwa kuwa mkubwa amelezimika kufunga.
“Mimi namiliki mikarafuu 73 ambayo kwa mzao ulivyo basi kila mkarafuu ntapata pishi 100 mbichi, wastani wa guni moja kavu sasa ntakunja hadi shilingi milioni 1 (1,000,000), sasa hapo piga kwa mikarafuu 73”,alieleza.
Nae Jabir Idrissa Makame wa Mizingani alisema, pamoja na kumilika mashamba mawili inayojumuiasha mikarafuu 400, alisema kwanza anachoomba kwa serikali kuhakikisha hawashushi bei wala wakulima kukopwa wanapokwenda kuuza ZSCT.
“Mimi mara nyingi ukimaliza msimu wa uchumaji hupeda kununua aradhi, kama nilivyofanya mwaka juzi kununua na kupanda miche 100, na mara hii ntafanya hivyo lakini pia na kunu gari aina ya ‘carry’ kwa ajili ya shughuli zangu”,alifafanua.
Hata hivyo mkulima Mmanga Hemed Sultan alienunua shamba la mikarafuu 550 hivi karibuni mabonde ya Ngomeni na Mgelema alisema anachokusudia kufanya kwa msimu huu baada ya kutoa haki za watu ni kununua gari moja kwa ajili ya biashara.
“Matumaini yangu kwanza mpaka nishewalipa vibarua, kutoa gharama za usafishaji wa shamba lakini baada ya hapo ni kutafuta gari moja aina ya ‘haice’ kwa ajili ya biashara”,alieleza.
Kwa upande wake mchumaji maarufu wa karafuu Kassim Haji Kassim (45) wa Ziwani wilaya ya Chakechake anasema, anachosubiri kwa hamu kwanza ni kuanza kwa msimu, ambapo malengi yake hapo kisha yatajipanga.
“Mimi msimu uliopita nilianza ujenzi wa nyumba ya kudumu, na kwa hatua iliobakia kama matajiri wataniita kuchuma kibarua basi ni kuhakikisha nakamilisha ujenzi kwa hatua ya kuezeka”,alisema.
Fatma Muhunzi Ameir (30) wa Piki wilaya ya Wete alieleza kuwa yeye msimu huu itakuwa ni mara yake ya kwanza kuchuma karafuu, kwa vile alikuwa misimu kadhaa hakuwepo kisiwa Pemba.
“Mwaka jana nilimaliza chuo na sasa nipo mtaani, hivyo karafuu zikianza tu name ntafuata walionayo ili kuchuma, lakini nikipata fedha nataka ninunue cherehani ya sinja, na kompyuta kwa ajili mwanangu kufanya mazoezi anaporudi skuli”,alifafanua.

   Mdhamini wa Shirika la taifa la ZSTC Kisiwani Pemba Abdalla Ali Ussi, alisema shirika halina nia wala mpango wa kushusha bei ya karafuu na waka hakutakuwa na mkulima atakaekopwa fedha wakati anapokwenda kuuza karafuu zake.
Alisema Serikali kupitia shirika lake pekee lililoruhusiwa kununua karafuu limejipanga kuhakikisha linawafikia wananchi na wakulima wote kwenye vituo rasmi vya kuuzia karafuu, na wala wasikubali kuwauzia watu wengine wanaopita mitaani.
Ussi hakuwa tayari kutaja kima halisi wanachotarajia kununua kwa msimu huu mpya, ingawa alisema baadae wataweka bayana, huku akiwasisitiza wananchi kuwa walinzi wa magendo ya karafauu hizo, ili ziendelea kubakia nchini kwa maslahi ya wananchi wenyewe.
Msimu mpya wa uvunaji wa zao la karafuu ambao unatabiriwa kuwa mkubwa kuliko misimu mengine ya miaka 10 iliopita, umeshazinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe: Baloz Seif Ali Idd hivi karibuni kisiwani Pemba.

                                  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.