Habari za Punde

DK.MABODI AKEMEA USALITI NDANI YA CCM Z'BAR.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma Mabodi amesema chama hicho hakitowavumilia baadhi ya wanachama na viongozi wanaotumiwa na vyama vya upinzani kuvuruga mshikamano uliopo ndani ya taasisi hiyo.  

Alitoa msimamo huo wakati akihitimisha ziara zake za kuimarisha chama na kuwapa mikakati ya kiutendaji viongozi wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa chama hicho kuanzia ngazi za matawi hadi majimbo Unguja, uko katika Tawi la Ijitimai jimbo la Mwanakwerekwe.

Alisema kupitia uchaguzi wa chama unaofanyika kwa ngazi mbali mbali ni lazima wanachama wasaliti wawekwe kando kwa kutopewa nafasi za uongozi na kiutendaji ili kunusuru uhai wa chama hicho kisiasa.

Aliwasihi  viongozi waliochaguliwa kuzitendea haki nafasi zao kwa kushuka ngazi za chini kutafuta wanachama wapya hasa wa vyama vya upinzani wajiunge na CCM ili mwaka 2020 upatikane  ushindi wa kihistoria.

Aidha aliwataka viongozi hao  wapya kutumia rasilimali watu  za  wanasiasa wakongwe na wazee wa chama hicho kujifunza itikadi na historia ya chama ili watekeleze kazi zao kwa ufanisi.

“ Ustawi na umadhubuti wa CCM utaendelezwa na nyinyi ambao mmepewa dhamana ya uongozi kwa njia ya kidemokrasia kupitia chama chetu, pamoja na mambo mengine ni kumbukeni kuwa mtaji wetu kisiasa ni wapiga kura hivyo hakikisheni mtaji huu unaendelea kuimarika ili 2020 tushinde na kubaki madarakani.”, alieleza Dk.Mabodi.

Dk. Mabodi alisema chama hicho kina imani kubwa na viongozi wake wa jumuiya na chama waliochaguliwa  kuwa watakivusha na kuendeleza mambo mema yaliyoachwa na watangulizi wao.

Alisema CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020  ili kero mbali mbali zinazowakabili wananchi ziweze kutafutiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kupitia ziara hiyo aliwaagiza makatibu wa Matawi wa chama hicho pamoja na kamati zingine kuhakikisha wanashuka ngazi za chini za zoni kutafuta wanachama wapya pamoja na kufanya shughuli za kijamii za kuwasaidia wazee katika maeneo mbali mbali nchini.

Sambamba na hayo alitoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi na wanachama wanaouza kadi za uanachama kwa wapinzani na kuwataka waache tabia hiyo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kimaadili kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

 Naye Katibu wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe , Ramadhan Fatawi alisema  Madiwani kwa kushirikiana na Mwakilishi wa jimbo hilo wamesimamia na kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo kusimamia ujenzi wa barabara ya lami inayotoka katika mtaa wa Kwamabata kwenda magogoni iliyogharamiwa na Wizara ya nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalum.

Mradi mingine ni uendelezaji wa  ujenzi wa chuo cha Amali cha jimbo hilo, kulipia ada za masomo  wanafunzi wa vyuo vikuu na sekondari, kujenga vyoo katika skuli ya Urafiki ya Mwanakwerekwe.

Alizitaja changomoto zinazowakabili katika jimbo hilo kuwa pamoja na mafuriko yanayotokea kila mwaka, upungufu wa ajira kwa vijana pamoja idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika darasa moja maskulini.

Pamoja na hayo Katibu huyo aliahidi kuwa Chama cha Mapinduzi ndani ya jimbo hilo kimejipanga kuhakikisha Uchaguzi ujao wanarudisha nafasi ya kiti cha Ubunge kilichoshikiliwa na chama cha upinzani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.