Habari za Punde

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na MBLM Amesema Mafunzo Hayo Yamewajengea Uwezo Wafanyakazi Hao.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                               29.09.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongezwa kwa juhudi zake za kuwawekea mazingira bora wafanyakazi wa sekta ya umma yakiwemo maslahi yao, mafunzo pamoja na vitendea kazi.

Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid Salum aliyasema hayo leo katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi katika hotuba yake ya ufungaji wa mafunzo ya mapishi na ukaribu yalioendeshwa na wakufunzi kutoka Taasisi ya “China National Research Institute of Food and Fermentation Industries”, ya nchini China.

Katika maelezoa yake Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Mafunzo hayo ni kielelezo cha dhamira njema ya Rais Dk. Shein ya kuwajengea uwezo watumishi ili kutoa huduma zilizo bora zaidi na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea “Business as Usual”.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamejenga daraja jengine la ushirikiano na uhusiano mwema kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na wananchi wa nchi mbili hizo.

Aliongeza kuwa Jamhuri ya Watu wa China imeendelea kuwa na mahusiano ya kidugu na ya kihistoria na watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ambapo nchi hiyo imeonesha jitihada kubwa katika kutoa fursa za kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali na viongozi kwa kuwapa mafunzo mbali mbali nchi mwao.

Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kukubali ombi la Rais Dk. Shein la kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo watumishi wanaotoa huduma za mapishi na ukarimu katikaOfisi za Viongozi Wakuu wa nchi pamoja na Walimu wa Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyakazi waliopata mafunzo hayo, kuthamini fursa hiyo adhimu na adimu waliyoipata kwa niaba ya watumishi wengine na kufanyakazi kwa bidii na nidhamu ili waoneshe mabadiliko ya ufanisi katika shughuli zao za kazi.

Pia, alitoa shukurani maalum kwa uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa ushirikiano wao na kukubali kuendesha mafunzo hayo katika taasisi ya Chuo cha Utalii Maruhubi, Zanzibar.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu huyo, alitoa shukurani kwa Wakufunzi wa mafunzo hayo na Taasisi ya “China National Research Institute of Food and Fermentation Industries” kwa kufanikisha utoaji wa mafunzo ya mapishi na ukarimu kwa watumishi wa Ofisi za viongozi wakuu wa Zanzibar pamoja na walimu wa Chuo cha Utalii, Maruhubi Zanzibar.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Biashara wa Taasisi ya “Chaina National Institute of Food and Fermentation Industries” Bibi Luo Yanqin alieleza kuwa mafunzo hayo yameenda vizuri na kuwapongeza watendaji wote walioshiriki mafunzo hayo.

Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuisifu Zanzibar pamoja na mazingira yake yakiwemo mazingira ya kitalii, fukwe, misitu, mazao ya viungo, ukarimu wa watu wake, maeneo ya kihistoria pamoja na mambo mengineyo ya kuvutia.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa mafunzo hayo yamezidi kuw chachu ya mahusiano na mashirikiano mema kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar.

Nao watendaji hao waliopata mafunzo hayo walitoa shukurani maalum kwa Rais Dk. Shein kwa kuwaandalia mafunzo hayo muhimu ili kuwajengea uwezo katika kuzitekeleza vyema kazi zao.

“Tunamwambia ahsante na Mwenyezi Mungu amjaalie kila la kheri, aidha, tunatoa shukurani kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kwa kuyaratibu mafunzo yetu”, walieleza watendaji hao katika hotuba yao iliyosomwa na Mustafa Ahmada Ali ambaye ni miongoni mwa watendaji waliopata mafunzo.

Sambamba na hayo, watendaji hao walitoa ombi maalum la kuongezwa muda wa mafunzo hayo mara nyengine  kwani mafunzo hayo yaliokuwa na nadharia na vitendo yamewapa maarifa mapya na ujuzi wa kuongeza ufanisi wa kazi zao huku wakiwapongeza wakufunzi walioendesha mafunzo hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.