Habari za Punde

Zanzibar na China Zatiliana Saini ya Makubaliano ya Madaktari wa China Wanaokuja Kufanyakazi Zanzibar Kukaa Kwa Mwaka Mmoja Badala ya Miaka Miwili.

Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu na Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo wakitia saini makubaliano mapya ya china kuendelea kuleta madaktari na kutumika kwa mwaka mmoja badala ya miwili, wanaoshuhudia Mwanasheria wa Wizara ya Afya Amina Moh’d na Mkuu wa kitengo cha uchumi na fedha wa ubalozi wa China Zanzibar Chen LI hafla hiyo ilimefanyika Wizara ya Afya.
Balozi Xie Xiaowu na Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo wakibadilishana hati za makubaliano ambapo China itaendelea kuleta madaktari Zanzibar na kufanyakazi kwa kipindi cha mwaka mmoja.Picha na Makame Mshenga.

Na. Ramadhani Ali –Maelezo Zanzibar.
Serikali ya Watu wa China imetiliana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar makubaliano mapya ambapo China itaendelea kuleta madaktari kutoa huduma Zanzibar na kuanzia sasa watakuepo nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo zilifanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja ambapo Zanzibar iliwakilishwa na Waziri Mahmoud Thabit Kombo na China iliwakilishwa na Balozi wake mdogo aliepo Zanzibar Xie Xiaowu.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri Mahmoud alisema kundi la kwanza la madaktari 21 watakaofanyakazi kwa utaratibu mpya wa mwaka mmoja limeanza kazi mwezi Julai ambapo madaktari 12 wapo Unguja na tisa Pemba.

Waziri wa Afya aliwatoa wasi wasi wananchi juu ya  utaratibu wa sasa wa madaktari hao kufanyakazi mwaka mmoja  na kuondoka kwavile ni wamajaribio na  ukionekana unaleta usumbufu utaratibu wa zamani wa miaka miwili unaweza kurejeshwa.

Wakati huo huo Waziri wa Afya alisema Madaktari bingwa watano wa maradhi ya Saratani, wakiwa na vifaa vya kisasa, kutoka Hospitali ya Nanjing China wanatarajiwa kuwasili Zanzibar mwisho wa wiki hii kuungana na madaktari wazalendo katika kampeni maalum ya uchunguzi wa maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi.

Alisema kampeni hiyo itaanza rasmi tarehe 10 hadi tarehe 23 mwezi huu katika Hospitali za Unguja na Pemba na amewahimiza akinamama waliofikia miaka 18 kuitumia fursa hiyo kuchungaza afya zao.

Alisema uamuzi huo unafuatia uchunguzi uliofanywa kwa akinamama wanaojifungua baadhi yao kubainika kuwa na chembe chembe za maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi

Waziri Mahmoud alikumbusha kuwa maradhi ya saratani sio rahisi kugundulika  bila ya kufanyiwa uchunguzi na dawa kubwa ya maradhi hayo ni kugundulika mapema na kupatiwa tiba katika hatua ya awali.

Nae balozi Xie Xiaowu aliahidi kuwa Serikali ya Watu wa China itaendeleza uhusiano wa kihistoria wa kuisaidia  Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kuimarisha huduma za Afya.

China  ilianzisha makubaliano na Zanzibar kuleta madaktari kutoa huduma katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee Mkoani tokea mwaka 1964 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.