Habari za Punde

ZRB yaja na njia mpya ya ulipaji kodi



NA HAJI NASSOR, PEMBA

BODI ya Mapato Zanzibar ZRB, imesema iko katika hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu wa kielektroniki kupitia simu ya mkononi, ili kuwawezesha wanaopaswa kulipa kodi, kufanya hivyo kwa kupitia mfumo huo, ambapo utawapunguzia muda wa kuweka foleni kwenye mabenki.

ZRB imesema, mifumo ya kisasa ya ulipaji wa kodi ukiwemo ule wa kulipitia benki haitoondolewa, ingawa mlipa kodi atakuwa na njia nyingi zaidi za kulipa madeni yake, kwa mujibu wa urahisi wake.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Afisa Mdhamini Elimu kwa walipa kodi kutoka Bodi hiyo Shaaban Yahya Ramadhan, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa wilaya ya Chakechake, kwenye semini juu ya kueleweshwa mabadiliko ya sheria za kodi.

Alisema ZRB imejiandaa vyema kuhakikisha inawarahisishia ulipaji wa kodi wadau wake, ndio maana imeshaandaa njia ya kupitia simu ya mkononi, ambapo zoezi rasmi litazinduliwa wakati wowote.

Aidha alieleza kuwa, kwa sasa wanaendelea na majaribio hayo kwa watendaji wake, na baadhi ya wafanyabiashara kuanza kuutumia, lakini rasmi muamala huo utazinduliwa hapo baadae.

“Sasa mnaotaka kulipa kodia pamoja na zile njia za zamazni lakini, kwa sasa pia tuna njia nyengine kupitia mtandao wa simu, tembeleeni ofisi zetu mtape maelekezo ya kina”,alifafanua.

Hata hivyo Afisa huyo, amewataka wafanyabiashara hao, kujitayarisha kisaikoloji ujio wa mashine za kielektroniki za utoaji wa risiti, EFD ikiwa ni pamoja na kujifunza matumizi yake mapema.

Alifahamisha kuwa faidi ya kubwa ya mashine hizo, hazipotezi mapato, maana zipo kampuni kabla ya kutumia mashine hizo walikuwa wakilipa kodi shilingi 13 milioni kwa mwaka, ingawa baada ya kuingia kwenye muamala wao sasa, wanalipwa shilingi milioni 167.

Kwa upande wake Meneja Sera, Utafiti, na Mipango kutoka ZRB Zanzibar Ahmed Saadat, alisema Bodi hiyo, itaendelea kuwaelimsha walipa kodi ili walipe kodi zao kwa hiari na wala sio kutumia nguvu.

Alisema ulipaji wa kodi duniani umekuwa na faida kubwa, ikiwa ni pamoja na kuihakikishia serikali kupanga mikakati yake, ya kimaendeleo kwa jamii.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Chakechake, wameiomba ZRB kukaa pamoja na TRA ili kuwe na mkusanyaji mmoja wa kodi ili kuondoa mkanganyiko wakati wa ukusanyaji.

Khamis Mohamed Haji, alisema uwepo wa mamlaka mbili zinazokusanya kodi kwa mfanyabiashara mmoja, ni changamoto ambayo lazima itafutiwe ufumbuzi.

“Sisi wafanyabishara tunapenda sana kulipa kodi, lakini sio kwa utaratibu huu ualipo, kuwa kuna TRA, ZRB, mbali mabaraza ya miji na hapo hujangaalia fedha za kodi, laima ufumbuzi wa kuwa na mkusanyaji mmoja uangaliwe”,alishauri.

Nae Rashidi Nassor Mohamed “manyimbo” alisema lazima maofisa wanaohusika na ukusanyaji wa kodi, wawe na lughua nzuri kwao, ili kujenga urafiki wa kikazi.


Katika semina hiyo ya siku moja, ufafnuzi wa sheria kadhaa 
zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na sheria ya ushuru wa stemp na sheria za nyaraka, ambapo tayari wafanyabishara kadhaa wameshafikiwa na taaluma hiyo. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.