Habari za Punde

Benki ya kilimo kusaidia mageuzi ya Kilimo Njombe

Mmoja wa wanachama wa cha Wafugaji wa Ngo’mbe wa Maziwa Mkoani Njombe, Bibi Aloycia Mdenye (wapili kushoto) akitoa maelezo kuhusu hali ya ufugaji wa ngo’mbe wa maziwa mkoani Njombe .
Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wakiangalia ng’ombe wanaofugwa na Bibi Aloycia Mdenye mmoja wa wanachama wa cha Wafugaji wa Ngo’mbe wa Maziwa Mkoani Njombe.
Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wakiangalia ng’ombe wanaofugwa na Bibi Aloycia Mdenye mmoja wa wanachama wa cha Wafugaji wa Ngo’mbe wa Maziwa Mkoani Njombe.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole Sendeka (katikati) akizungumza na ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) walipomtembelea Ofisini kwake Mkoani Njombe. Ugeni uliongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib (wanne kushoto waliokaa).
Kiongozi wa Msafara wa Ukaguzi wa Miradi ya Kilimo Mkoani Njombe ambaye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib (Kulia) akiwa na Meneja Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe (kushoto) wakifuatilia kwa makini mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole Sendeka (hayupo pichani).

Na mwandishi wetu, Njombe
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imesema imejipanga katika kusaidia kuchagiza kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima mkoani Njombe na Tanzania kwa ujumla.

Ahadi imetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib wakati alipouongoza ujumbe wa Benki walipomtembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole Sendeka mkoani Njombe.

Bibi Twalib alisema kuwa TADB ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania ili kuisaidia Serikali kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya  asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi.

Aliongeza kuwa Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika  kilimo nchini.

“Katika kuhakikisha tunafikia malengo ya Serikali Benki imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini” alisema.

Akizungumza na ugeni huo, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Christopher Ole Sendeka alisema kuwa ujio wa Benki hiyo mkoani Njombe kutahamasisha shughuli za kilimo mkoani humo hali itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa Mhe. Ole Sendeka, mkoa wa Njombe umejaaliwa rasilimali nyingi kwenye sekta ya kilimo ila changamoto za ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo zinarudisha nyuma juhudi za wakulima mkoani humo.

“Naishukuru Serikali kwa kuianzisha TADB kwani hali ya ukosefu wa mitaji ya uhakika inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa na kuwasahau wakulima na wasindikaji wa mazao, hivyo tunaamini TADB itasaidia kutatua changamoto hii,” alisema.

Bw.Ole Sendeka alitoa wito wa wakulima mkoani humo kuchangamkia fursa hizo za mikopo ya gharama nafuu inayotolewa na Benki ya Kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji na hivyo kujihakikisha kipato cha uhakika.

Kwa upande wake, Meneja Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe alisema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
Kwa mujibu wa Bw. Pangamawe mikopo hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

“Dhima ya Benki yetu ni kuhakikisha tunawezesha maendeleo na kufanikisha mapinduzi ya sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwenye miradi ya kilimo Tanzania inayolenga kukuza uchumi, kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umasikini wa kipato,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.