STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
25.10.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameupongeza uongozi wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kutekeleza vyema majukumu yake na kusisitiza
kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na elimu bora.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana
na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa
mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa
kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba kwa mwaka 2017.
Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi
wa Wizara hiyo ya Elimu, pamoja na watendaji wake wote kwa kwenda sambamba na
azma ya Serikali ya kuwa na elimu bora huku akisisitiza haja ya Kujituma katika
majukumu yao yote.
Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi huo haja ya
kufanya kazi kwa pamoja, kusaidiana na kushirikiana katika kutekeleza majukumu
yao ili Wizara hiyo ienndelee kupata mafanikio makubwa zaidi na kuwasisitiza
kuwa wasichelee kuchukua hatua pale inapobidi kufanya hivyo.
“Hapa mlipofika leo pazuri sana, hivyo jitahidini
msirudi nyuma kwani mmefanya kazi kubwa na nzuri, hivyo ni lazima
tukupongezeni, hongereni sana na sote tumeridhika”, aliongeza Dk. Shein.
Mapema akizungumzia suala la utafiti, Rais Dk.
Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa tafiti katika Wizara kwani hatua hiyo itasaidia
kwa kiasi kikubwa kuibua mambo mbali mbali na hatimae kupata majibu na kueleza
kuwa Wizara yoyote ya Serikali haiwezi kwenda bila ya utafiti.
Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa
vuguvugu la mashindano ya riadha kwa wanafunzi katika kipindi cha sherehe za
elimu bila malipo kwa lengo la kuibua vipaji.
Alieleza kuwa ni vyema kwa kila mwanafunzi akapata
muda wa kucheza na kuweza kushindana na wanafunzi wenziwe katika skuli nyengine
ili wawe wakakamavu na kusisitiza haja ya kila skuli kuwa na mwalimu maalum wa
michezo kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya
michezo ni vyema Wizara hiyo ikatilia mkazo sanaa, katika skuli na hata katika
Vyuo Vikuu kwani sanaa ni sehemu ya kuimarisha utamaduni, hatua ambayo pia, huchangia
kupata wasanii mahiri.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alitoa pongezi kwa Wizara hiyo na
kusisitiza haja ya kuimarishwa kwa Maktaba za Skuli pamoja na kulielezea suala
zima la ukaguzi wa skuli na kutaka walimu wakuu wawe wakaguzi wa kwanza katika
kuwasimamia walimu wanaowaongoza katika skuli zao.
Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa shukurani kwa Rais
Dk. Shein kwa jinsi alivyokuwa karibu sana na Wizara hiyo kwa kuwapa miongozo
na maelekezo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza sekta ya
elimu.
Alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 2,655 wakiwemo
372 wapya na 2,283 wanaoendelea na elimu ya juu wamepatiwa mkopo kupitia Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya juu ya Zanzibar ambapo jumla ya TZS Bilioni 2,630
zimelipwa. Aidha, Bodi imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS milioni 480, kutoka
kwa wadaiwa waliohitimu.
Hata hivyo, Waziri huyo wa Elimu alieleza kuwa
katika mwaka wa afedha 2017/ 2018, Wizara
inaendelea na malengo ya kupanua upatikanahji wa huduma za elimu na kuimarisha
ubora wa elimu inayotolewa kwa
kuimarisha elimu ya Maandalizi ikiwa ni pamoja na kujenga skuli ya Maandalizi huko
Mbuyu maji, Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Pia, kuimarisha Elimu ya Msingi kwa kujenga skuli
mbili katika maeneo ya Kwarara an Fuoni-Pangawe, kuwajengea uwezo walimu katika
kutathmini maendeleo ya watoto katika kusoma, kuandika na kuhesabu, kununua
vitabu vya kujifunza kusoma na kutoa huduma ya chakula kwa skuli 10 za Unguja
na Pemba.
Lengo jengine ni kuimarisha elimu ya Sekondari kwa
kujenga skuli mbili Mwanakwerekwe na Wingwi, madarasa 48 na maktaba katika
skuli 23 za Unguja na Pemba, kukamilisha ujenzi wa vituo viwili vya Mafunzo ya
Amali vya Daya kwa Pemba na Makunduchi kwa Unguja na kukamilisha ujenzi wa
majengo ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume na Taasisi ya Maendeleo
ya Utalii ya Maruhubi na kujenga viwanja 11 vya michezo katika skuli 11.
Aidha, Waziri huyo alieleza changamoto katika sekta
hiyo ya elimu ikiwa ni pamoja na kasi ya ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa
katika skuli za msingi na sekondari hasa katika skuli za Mkoa wa Mjini
Magharibi haiowani na ongezeko la miundombinu ya skuli na matokeo yake idadi ya
wanafunzi kwa darasa inaongezeka, hali inayoathiri ubora wa elimu.
Uongozi wa Wizara hiyo pia, ulieleza hatua
walizozichukua katika kupita maskulini na kuangalia usomeshaji na mahudhurio ya
walimu madarasani sambamba na kuchukua juhudi za kuwashajihisha walimu kufanya
kazi kwa ufanisi huku ukielezea jinsi ulivyofanya ukaguzi wa kushtukiza ambao
umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa.
Pia, katika maelezo yao uongozi wa Wizara hiyo
walieleza changamoto iliyopo hivi sasa ya uhaba wa walimu uliopo ambayo pia,
huchangiwa na tabia ya baadhi ya walimu kuhama hama kwa visingizo mbali mbali
na baadhi ya wengine kukataa kushomesha katika skuli za vijiji na hata katika
skuli za Pemba.
Ungozi huo pia, ulieleza haja ya kuwepo kwa
Maktaba za Wilaya kwa ajili ya kuwafikishia watoto huduma hiyo kwani matumizi
ya Maktaba Kuu iliyopo mjini kwa hivi sasa idadi ya watumiaji wake ni ndogo hali
ambayo inatokana na masafa na umbali ya watoto wanakoishi pamoja na wazazi
wengi kutowashajiisha watoto wao kutumia Maktaba.
Sambamba na hayo, uongozi huo ulieleza azma yake
ya kuimarisha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na kukamilisha madarasa 200
yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi Unguja na Pemba pamoja na juhudi
wanazoendelea nazo katika ukusanyaji wa fedha za madawati.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment