Habari za Punde

Jumuiya ya Maimamu Zanzibar yapinga madai ya wanaharakati wa kutetea haki za wanawake

 Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Sheikh Muhiddin Zubeir Muhiddin akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Majestiki kupinga madai yaliyotolewa na wanaharakati wa haki za wanawake kuhusu uwezekano wa mwanamke kuwa kadhi katika mahakama ya kadhi Zanzibar.
 Mwenyekiti wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji  wa JUMAZA Sheikh Nassor Hamad Omar akitoa ufafanuzi  wa masuali yaliyoulizwa na Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na uwezekano wa mwanamke kuwa kadhi katika mahakama ya kadhi Zanzibar
Mjumbe wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikh Omar Mohd Khamis akitoa ufafanuzi wa masuali yaliyoulizwa na waandishi wa habari  juu ya uwezekano wa mwanamke kuwa kadhi katika mahakama ya kadhi Zanzibar.
Picha na Kijakazi Abdalla – Maelezo

Na Fatma Makame na Miza Kona      Maelezo 

 Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ( JUMAZA ) imepinga  madai ya wanaharakati wa kutetea haki za wanawake  wanaotaka  mwanamke kupewa nafasi ya kadhi katika Mahakama ya Kadhi Zanzibar  jambo ambalo halikubalikia katika dini ya kiislamu .

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisi ya JUMAZA Majestiki,  Katibu  Mtendaji  wa Jumuiya hiyo Sheikh Muhidin  Zuberi Muhidin amesema hakuna sheria katika dini ya kiislamu inayoruhusu mwanamke wa kiislamu kupewa nafasi ya ukadhi.

Alisema uislamu ulikuja kumkomboa mwanamke na kumpa heshima na sio kumnyima haki zake za msingi na kumwekea mipaka ili kuweza kutekeleza majukumu yake yanayokubalika bila kwenda kinyume na maamrisho ya dini.

“Katika kipindi cha Mtume hakukuwa na kadhi mwanamke katika Mahkama ya Kadhi, mwanamke ameekewa mipaka maalum katika dini ya kutoa maamuzi, hawezi kutoa idhini katika ndoa hivyo akishika  nafasi hiyo atalazimika kuozesha jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria ya dini ya kiislam”, alifahamisha Shekh Muhidin.

Katibu Muhidin aliwataka  wanaharati wanaotetea haki za wanawake Zanzibar kuachana na mambo yanayokwenda kinyume na dini na kushughulikia harakati zao ili waweza kuinusuru jamii kuingia katika mfarakano na kupelekea uvunjifu wa amani.

 “Serikali inatakiwa kuwa makini sana na masuala yanayohusu sheria za dini ili kuiepusha jamii kuingia katika hatari uvunjifu wa amani”, alisisitiza Katibu Mtendaji.  

 Nae Mwenyekiti wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji  wa JUMAZA  Nassor Hamad Omar amewataka Wanaharakati hao kutumia nguvu zao kuiokoa jamii katika kupinga vitendo vya udhalilishaji na sio kuibua mijadala isiyokubalika.

Hata hivyo amevitaka vyombo vya habari kufanya utafiti wa kina kuhusu masuala ya dini kabla ya kuzitoa habari ili kuwa na uhakika wa taarifa yenyewe kwa lengo la kuepuka upotoshaji kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.