Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Akizundua Ripoti ya Hali ya Utafiti wa Umasikini Zanzibar.

Balozi Seif akizindua Rasmi Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar  hapo katika Jengo Jipya la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mazizini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano Maalum wa  uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar  hapo katika Jengo Jipya linaloendelea kujengwa la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  liliopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Fedha Duniani { World Bank } Bibi Bella Bird akitoa salamu kwenye Mkutano Maalum wa Uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bibi Mayasa Mahfoudh akitoa Taarifa ya masuala ya Takwimu kwenye Mkutano Maalum wa Uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar uliofanyika kwenye Jengo lao jipya Mazizini.
Baadhi ya Washirika wa Maendeleo waliohudhuria Mkutano Maalum wa Uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar  ya Mwaka  2009/2010 hadi 2014/2015.
Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Mabalozi wa Nchi za Nje waliopo Tanzania wakishuhudia uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar  ya Mwaka  2009/2010 hadi 2014/2015.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga.
Balozi Seif akitoa ufafanuzi mbele ya Wana Habari kuhusu Ripoti ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar mara baada ya kuizindua rasmi hapo katika jengo la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa SMZ Mazizini.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na. Othman Khamis. OMPR.  
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kupungua kwa kiwango cha umaskini miongoni mwa Wananchi hapa nchini kinatokana na matokeo ya Maarifa ya Elimu  ya  Maisha iliyopatiwa Jamii sambamba na mbinu za uwezeshwaji Wananchi Kiuchumi katika maeneo tofauti Visiwani Zanzibar.

Alisema kiwango cha umaskini kilichokuwa kikiwakabili wananchi walio wengi kimepungua kutoka asilimia 34.9 hadi asilimia 30.4 kati ya Mwaka 2009/2010 na 2014/2015 jambo ambalo limeleta faraja na kupungua kwa ukali wa maisha  kwenye Kaya nyingi Unguja na Pemba.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika Mkutano Maalum wa  uzinduzi wa Ripoti ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar  hapo katika Jengo Jipya linaloendelea kujengwa la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  liliopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ndani na Nje ya Nchi itaongeza nguvu katika kuimarisha miundombinu sambamba na kuendelea kutoa Taaluma ili kuona Wananchi wa maeneo yanayokabiliwa na umasikini mkubwa yanakwamuka na kadhia hiyo.

Balozi Seif alisema kuongezeka kwa umaskini kwenye maeneo ya Vijiji hasa katika Kisiwa cha Pemba ni suala nyeti ambalo Serikali inalazimika kuwa na mbinu mbadala za kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuleta ahuweni kwa Jamii inayozunguuka  maeneo hayo.

Alisema vyuo vya Amali vinaendelea kuimarishwa katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ili vitoe mafunzo ya ujasiri Amali utakaowasaidia Vijana kuzalisha  uwezo wa kubuni na hatimae kuendesha Maisha yao bila ya kusubiri ajira kutoka Serikalini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali Kuu iko tayari kuifanyia kazi Ripoti hiyo ya hali ya Utafiti wa Umaskini Zanzibar ili iende sambamba na  mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa 2020 uliolenga kupunguza idadi ya Watu wanaoishi ndani ya kundi  la Umaskini Zanzibar.

Ameishukuru na kuipongeza Benki ya Dunia pamoja na Taasisi na Mashirika mengine ya Kimataifa na yale ya Kitaifa kwa hatua wanazochukuwa za kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika mapambano yake dhidi ya kukabiliana na umaskini kupitia Miradi na mipango tofauti.

Mapema akitoa Taarifa ya masuala ya Takwimu, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bibi Mayasa Mahfoudh alisema Ofisi ya Takwimu itaendelea kufanya utafiti wa masuala mbali mbali ya kila Nyanja kuhusu Uchumi, Jamii na maendeleo katika wajibu wake wa Kuishauri Serikali na Taasisi za Umma na zile za kiraia kutambua hali na mazingira ya Nyanja hizo.

Bibi Mayasa alisema hatua hiyo itasaidia kutoa mwanga wa kuelewa maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii sambamba na kufahamu changamoto zinazojitokeza katika tafiti mbali mbali ili hatua zichukuliwe kwa wakati muwafaka.

Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameziomba na kuzihimiza Taasisi za Umma, binafsi na Makampuni yote kuzitumia Takwimu zinazotolewa na Ofisi hiyo kwa lengo la kupiga hatua za haraka za Maendeleo na kwenda sambamba na mabadiliko ya Dunia ya Sayansi na Teknolojia.

Akitoa salamu za Shirika la Fedha Duniani { World Bank } Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi hiyo ya Kimataifa Bibi Bella Bird alisema Takwimu za Utafiti uliofanywa Zanzibar miaka Michache  iliyopita zimeonyesha kuwepo kwa baadhi ya Maeneo yenye hali tete za ukali wa maisha zaidi Vijijini hasa katika maeneo ya Kisiwa cha Pemba.

Bibi Bella aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa hatua iliyochukuwa ya kubuni Mpango wa Taifa wa Kupunguza Umaskini Zanzibar { MKUZA } uliolenga kupunguza ukali wa maisha kwa Wananchi wake pamoja na kuimarisha Uchumi na Maendeleo kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkaazi huyo wa Benki ya Dunia Bibi Bella aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Benki hiyo itaendelea kuziunga MkonoSerikali zote mbili katika Sekta za Elimu, Afya na Uchumi kupitia Mradi wa Tasaf.

Wakitoa maelezo na ufafanuzi wa Utafiti wa hali ya Umaskini Zanzibar katika Mkutano huo wa siku Moja Wataalamu wa Uchumi Bibi Nadia Belhaj Belgith Kutoka Benki ya Dunia na Bibi Nour Abdulwahid kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walisema hali ya umasikini imepungua kidogo miongozi mwa Wananchi Visiwani Zanzibar ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Wataalamu hao walisema Utafiti umeonyesha wazi kwamba Idadi kubwa ya Wananchi wanaoishi Vijijini ndio wanaoendelea kukabiliwa na ukali wa maisha ikilinganishwa na wale wanaoishi katika maeneo ya Miji.

Walisema utofauti huo uliojionyesha wazi katika maeneo hayo mawili unatokana na suala kubwa la ongezeko kubwa la upatikanaji wa elimu linaloonekana kuimarika zaidi katika maeneo mbali mbali ya Miji.

Hata hivyo walisema ipo hatua kubwa iliyopatikana ya kuimarika kwa kiwango cha elimu hasa Mjini lakini hakiendani sambamba na upatikanaji wa ajira kutokana na upungufu wa mbinu za kuwaezesha wasomi hao kuweza kujiajiri na kujitegemea wenyewe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.