Habari za Punde

Mambo 10 Unayotakiwa Kuyafahamu Kuhusu Ukimwi.

Na Jumia Travel Tanzania
Wakati dunia ikielekea kuadhimisha siku ya UKIMWI kila ifikapo Desemba mosi ya kila mwaka, bado Virusi Vya UKIMWI (VVU) na ugonjwa huo unabaki kuwa ni changamoto muhimu ya kiafya ndani ya jamii hususani kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati.

Kutokana na maendeleo yaliyofikiwa sasa katika upatikanaji wa tiba ya mchanganyiko wa dawa zinazotumika kuzuia VVU kuongezeka mwilini (antiretroviral therapy - ART), watu waliogundulika kuwa na VVU wanaishi kwa muda mrefu na maisha yenye afya. Kwa kuongezea, imethibitishwa kwamba dawa hizo zinazuia kuendelea kuongezeka kwa VVU.

Katika kukupatia elimu zaidi juu ya ugonjwa huu, Jumia Travel ingependa kukufahamisha juu ya mambo yafuatayo ambayo yamebainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambalo huunga mkono nchi mbalimbali katika kuunda na kutekeleza sera na programu ili kuboresha na kuongeza jitihada za kuzuia VVU, matibabu, huduma na kutoa msaada kwa watu wote wanaohitaji msaada.

Taafirifa hizi zinatoa takwimu zilizopo sasa kuhusu ugonjwa huu pamoja na njia za kuuzia na kuutibu:

VVU huambukiza seli za kwenye mfumo wa kinga za mwili. Maambukizi husababisha kuendelea kuzorota kwa mfumo wa kinga ya mwili, huvunja uwezo wa mwili kuweza kuepuka baadhi ya maambukizi na magonjwa. UKIMWI hujulikana kuwa ni hatua ya juu kabisa ya VVU ambapo hujipambanua kwa kujitokeza kwa maambukizi kati ya zaidi ya 20 au saratani zinahusiana na virusi hivyo.   

VVU vinaweza kuambukizwa kwa njia kadhaa. VVU vinaweza kuambukizwa kupitia: kujihusisha na ngono isiyo salama; kuhamishiwa damu au bidhaa inayohusiana na damu au kufanyiwa upandikizaji ambao sio salama; kushirikiana kutumia vifaa vya kutobolea mwili (sindano) na vimiminika au vya kuchorea michoro mwilini (tattoo); kutumia vifaa vya upasuaji na vinginevyo vyenye ncha kali; na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto mchanga wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.   
Zipo njia kadhaa za kuzuia maambukizi ya VVU. Njia muhimu za kuzuia maambukizi ya VVU ni: kufanya ngono salama kama vile kutumia kondomu; kupima na kupatiwa matibabu kwa magonjwa yaliyoambukizwa kupitia ngono, ikiwemo VVU ili kuzuia maambukizi kuendelea; hakikisha kwamba damu au bidhaa yoyote inayohusiana na damu unayotaka kuitumia imepimwa VVU; chagua njia salama ya kimatibabu wakati wa tohara endapo unatoka katika nchi ambazo huchangia vifaa; kama una VVU anza mara moja kutumia dawa za kusaidia kupunguza virusi kuongezeka mwilini kwa manufaa yako na pia kuzuia kuambukiza VVU kwa mwenza au mtoto wako (kama ni mjamzito au unanyonyesha).  
Watu milioni 36.7 duniani wanaishi na VVU. Duniani kote, inakadiriwa kuwa watu milioni 36.7 (milioni 34.0 - 39.8) walikuwa wanaishi na VVU mwaka 2015, na kati ya hawa milioni 1.8 (milioni 1.5 - 2.0) walikuwa ni watoto. Idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU wanapatikana kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Inakadiriwa watu milioni 2.1 (milioni 1.8 - 2.4) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015. Inakadiriwa watu milioni 35 mpaka sasa wamefariki kutokana na VVU, wakiwemo milioni 1.1 (940,000 mpaka milioni 1.3) mwaka 2015.    
Mchanganyiko wa dawa za ART huzuia virusi hivyo kuongezeka mwilini. Endapo kuzaliana kwa VVU kukikoma, basi seli za kinga za mwili zitaweza kuishi kwa muda mrefu na kuupatia mwili kinga dhidi ya maambukizi. Ufanisi wa dawa za ART hupelekea kupungua kwa virusi, kiasi cha virusi mwilini, kwa kiasi kikubwa hupunguza kuambukiza virusi kwa watu walio kwenye mahusiano ya kimapenzi. Endapo mmojawapo wa wapenzi kwenye mahusiano anatumia dawa za ART ipasavyo, kuna uwezekano wa maambukizi ya njia ya ngono kwa mwenza ambaye hana VVU kupungua kwa kiasi cha takribani 96%. Kupanua wigo wa matibabu ya VVU kunachangia katika jitihada za kuzuia VVU.   
Katikati ya mwaka 2016, watu milioni 18.2 duniani walipokea dawa za kusaidia kuzuia VVU kuongezeka mwilini. Kati ya hawa zaidi ya milioni 16 wanaishi kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Mwaka 2016, WHO ilitoa toleo la pili la “Miongozo juu ya matumizi ya dawa za kusaidia kuzuia kuongezeka VVU mwilini ili kutibu na kuzuia maambukizi ya VVU.” miongozo hii imetoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo pendekezo la kutoa dawa za kusaidia kuzuia VVU kuongezeka mwilini kwa watoto kwa kipindi chote cha maisha yao, vijana na watu wazima, wakiwemo wanawake wajawazito na wanaonyonyesha waishio na VVU, licha ya idadi ya CD4 walizonazo mara baada tu baada ya kugundulika.          

Kupima VVU kunasaidia kuhakikisha matibabu kwa watu wenye uhitaji. Upatikanaji wa huduma ya kupima VVU na madawa unatakiwa kuongezeka kwa kasi ili kufikia lengo la kutokuwa na ugonjwa wa UKIMWI kufikia mwaka 2030. Upimaji wa VVU bado ni mdogo, ambapo inakadiriwa kwamba 40% ya watu wenye VVU au zaidi ya watu milioni 14 bado hawajatambulika na hawafahamu hali ya maambukizi yao. WHO inapendekeza ubunifu kwenye mbinu za kujipima wenyewe VVU na wenza wao ili kuongeza huduma za kupima VVU kwa watu ambao hawajagundulika.    
Inakadiriwa watoto milioni 1.8 duniani wanaishi na VVU. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, wengi wa watoto hawa wanaishi katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara na waliambukizwa kutoka kwa mama zao wenye VVU wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaliwa au kunyonyeshwa. Karibu watoto 150,000 (110,000 - 190,000) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015.
Kuondoa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inawezekana. Ufikiwaji wa hatua za kuzuia maambukizi ya VVU umekuwa ni mdogo kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Lakini jitihada zimeendelea kufanyika kwenye baadhi ya maeneo tofauti kama vile kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na kuokoa maisha ya akina mama. Mwaka 2015, karibu wajawazito 8 kati ya 10 wanaoishi na VVU au sawa na wanawake milioni 1.1 walipokea dawa za kuzuia VVU kuongezeka mwilini. Mwaka 2015, Cuba ilikuwa ni nchi ya kwanza kutangazwa na WHO kufanikiwa kuzuia maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mwaka 2016, nchi zingine tatu: Armenia, Belarus na Thailand nazo zilithibitishwa kulifanikisha hilo.        
VVU ni sababu kubwa inayopelekea kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB). Katika mwaka 2015, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.2 (11%) kati ya watu milioni 10.4 duniani waliopata TB walikuwa ni waathirika wa VVU pia. Mwaka huohuo takribani vifo 390,000 vilivyotokana na TB vilitokea miongoni mwa watu waliokuwa wanaishi na VVU. Nchi za Kiafrika ambazo zilizo chini ya WHO zilizidi karibu 75% ya idadi ya vifo vilivyokuwa vinahusiana kati ya TB na VVU.
UKIMWI ni janga ambalo linaikumba dunia nzima Tanzania ikiwemo, licha ya ugonjwa huu kutzungumziwa kwenye kampeni tunazozisikia lakini ukweli ni kwamba bado upo, ni tatizo, unaathiri na kuua nguvu kubwa ya taifa. Katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, Jumia Travel ingependa kuikumbusha jamii inapaswa kutambua kwamba jukumu la kuupiga vita ugonjwa huo bila ya kutegemea taasisi binafsi au mashirika ya nje.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.