Habari za Punde

Zanzibar Kujengwa Uwanja wa Ndege Mpya

MAOFISA kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar wakikagua eneo linalotarajiwa kujengwa kiwanja cha ndege huko Kigunda Jomba Mkoa wa Kaskazini Unguja.

OFISA habari wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Makame Abdallah akizungumza na waandishi wa habari walipofika katika eneo lilipangwa kujengwa kiwanja cha Ndege Mkoa Kaskazini Unguja.
MKUU wa Wilaya Kaskazini ‘A’ Unguja Hassan Ali Kombo akimkabidhi pesa taslim Bakari Adibu Makame kama fidia ya malipo ya mazao yake katika hafla ya uzinduzi wa kulipa fidia uliofanyika Ofisini kwake Gamba.
MKUU wa Wilaya Kaskazini ‘A’ Unguja Hassan Ali Kombo akimkabidhi pesa Bi. Mtumwa Mwaga Jecha kama fidia ya mazao yake.

Picha na Makame Mshenga.

Na Salum Vuai, MAELEZO. 4 Novemba, 2017
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar iko katika maandalizi ya ujenzi wa kiwanja kipya kidogo cha ndege kitakachosaidiana na kile cha Abeid Amani Karume kilichoko Kisauni Wilaya ya Magharibi ‘B’.

Kiwanja hicho kinatarajiwa kujengwa kwenye kijiji cha Kigunda Mkoa wa Kaskazini Unguja kilichoko takriban kilomita 50 kutoka mjini Unguja.

(Leo Novemba 4, 2017), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), ilianza kuwalipa fidia ya mazao wananchi 99 kutoka shehia za Tazari, Kilindi na Kigunda waliokuwa wakiendesha shughuli za kilimo katika eneo linalotarajiwa kujengwa kiwanja hicho.

Kwa mujibu wa ofisa uhusiano wa mamlaka hiyo Makame Abdalla Seti, takriban shilingi 57,000,000 zimelipwa kwa wakulima hao baada ya kuvifanyia tathmini vipando vyao kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa malipo kwa  wakulima hao uliofanyikia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’Gamba,  Seti alisema eneo lenye urefu wa kilomita mbili na upana wa mita 200 limetengwa na mamlaka kwa ajili ya mradi huo utakaogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema kitakapokamilika, kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege mbili ndogo mfano wa ATR 172, C 208, C 172, Bombadier na nyengine zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi 50.

Alifahamisha kuwa lengo la ujenzi huo ni kupunguza msongamano katika uwnaja wa Abeid Amani Karume, na  mzunguko wa safari za watalii ambao kwanza hufika Tanzania Bara au hata nchi jirani za Afrika Mashariki na baadae kuja hapa Zanzibar.

Alisema watalii hao ni wale wanaofikia hoteli zilizoko ukanda wa utalii wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwenye maeneo ya Nungwi, Matemwe na Kiwengwa ambako harakati za kitalii zimeongezeka maradufu.

“Tunajua watalii wengi wanaokuja nchini mwetu huwa wanataka kupumzika na hawapendi kusafiri masafa marefu kuzifikia hoteli zao wanazopanga, hivyo kiwanja hichi kitasaidia kuwafikisha moja kwa moja badala ya kuteremka Kisauni na kupoteza saa kadhaa barabarani,” alifafanua.

Halikadhalika, alisema iwapo kutatokezea dharura yoyote itakayozuia matumizi ya uwanja wa sasa, kiwanja hicho kitatumika kama mbadala kwa kupokea ndege zitakazofika nchini za kiwango husika.

Ofisa huyo alisema, hatua ya kwanza ilikuwa kulizuia eneo hilo na inayofuata ni kulisafisha huku taratibu za kutangaza zabuni kwa wakandarasi zikiendelea kufanyika.

Naye Ofisa Mazingira wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar  Suleiman Hamad Omar, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi waliokuwa wakitumia ardhi hiyo kwa kuridhia kupisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya kijiji chao na taifa kwa jumla.

Aidha, alieleza kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya Wilaya kuwatafuta,kuwaorodhesha wahusika, kuvitathmini vipando vyao na hatimaye kuwezesha kuwalipa stahiki zao kwa mujibu wa thamani sahihi.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Hassan Ali Kombo, alisema ridhaa ya wananchi hao inatokana na kutambua umuhimu wa miradi ya maendeleo inayoanzishwa na serikali, na mbali ya kuwashukuru, aliwataka kutumia fedha walizolipwa kutafuta shughuli za uzalishaji zitakazowainua kisha na familia zao.

Kwa upande wao, wanufaika wa malipo hayo, wameishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa kuwapa muda wa kuvuna mazao yao kabla kuanza kuisafisha ardhi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, na kusisitiza kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ mradi huo utakapoanza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.