Habari za Punde

Taarifa maalum kuhusu hali ya mafuta Zanzibar

TAARIFA MAALUM KUHUSU HALI YA MAFUTA ZANZIBAR

Kufuatia hali ya kupungua Mafuta ya Petroli iliyojitokeza hasa katika Vituo vya Mafuta vya Kampuni ya GAPCO, na kusababisha Foleni katika Vituo vya Mafuta vya Kampuni za ZP na UP, ZURA imechukua hatua zifuatazo kukabiliana na changamoto hiyo:-

Meli ya MT Ukombozi Jana imefanikiwa kupakia Mafuta ya Petroli Tani Elfu Moja na Mia Nne (1400 Metric Tones) sawa na Lita Milioni moja Laki Nane na Arobaini na Nane Elfu (1,848,000). Mafuta hayo yanatarajiwa kufika Leo na kusambazwa Vituoni Kesho.

Pia ZURA inaendelea kusimamia zoezi la usambazaji na uuzwaji wa mafuta vituoni kwa yale yaliyopo hadi Mafuta yaliyoagizwa yatakapofika nchini na kuhakikisha yanauzwa kwa mujibu wa maelekezo ya Mamlaka.

Katika kutekeleza hili, ZURA inahakikisha Mafuta yaliyopo yanasambazwa Vituoni ili kukabiliana na hali iliyotokea.

Hali ya Mafuta iliyopo Nchini kwa sasa ni kama ifuatavyo:-

Kampuni ya GAPCO

·        Petrol: Lita 20,000

·        Diesel: Lita 314,106

·        Kerosene: Lita 78,576

Kampuni ya ZANZIBAR PETROLEUM (ZP)

·        Petrol: Lita 40,000

·        Diesel: Lita 89,884

·        Kerosene: 144,443

Kampuni ya UNITED PETROLEUM (UP)

·        Petrol: Lita 60,000

·        Diesel: Lita 1,006,000

·        Kerosene: Lita 312,663

Aidha, upungufu umejitokeza kwa Mafuta ya Petroli tu, hali ya upatikanaji wa bidhaa nyengine za Mafuta kama vile Dizeli na Mafuta ya Taa ipo kama kawaida.

Kwa Kampuni za ZP na UP zinatarajiwa kuingiza Mafuta kwa kutumia Meli zao kuanzia Kesho Tarehe 4/01/2018, ili kuongeza kiwango cha Mafuta kuwa ya kutosheleza nchini.

Wananchi wanaombwa kuwa wastahamilivu, wakati Mamlaka inafanya juhudi za kutosha kuhakikisha hali ya upatikanaji wa Mafuta inarejea katika hali ya kawaida na kukidhi mahitaji ya Soko.

Matarajio ya ZURA ni kwamba hadi Siku ya Ijumaa Tarehe 5/01/2018 upatikanaji wa bidhaa za Mafuta utakua umeshapatiwa ufumbuzi na kurudi katika hali ya kawaida, na kuanzia Jumamosi Tarehe 6/01/2018 Mafuta yatakua yanapatikana kwa uhakika. Tunaomba ushirikiano kutoka kwa Wadau wote wa Mafuta na Wananchi, aidha tunawaomba Wananchi wawe watulivu na wastahamilivu katika kipindi hiki.

IMETOLEWA NA MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI ZANZIBAR (ZURA)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.