Habari za Punde

Kamishna Mkuu Kichere Awataka Wafanyakazi Sirari Kuendelea na Utoaji wa Kodi Stahiki.

Na: Veronica Kazimoto.                                                                                    
Sirari 01 Februari, 2018.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere amewataka Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali wakiwemo wa mamlaka hiyo wanaofanya kazi katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari  kilichopo wilaya ya Tarime mkoani Mara kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha wanaendelea kutoza kodi stahiki.

Akizungumza wakati wa ziara yake kituoni hapo, Kamishna Mkuu Kichere alisema nchi inaendeshwa kwa kodi za ndani hivyo ni muhimu kila taasisi iliyopo eneo hilo kutimiza wajibu wake katika suala zima la ukusanyaji wa kodi.

"Wote mnajua umuhimu wa kodi na pia mnafahamu kuwa, kwa kupitia kodi hizi, Serikali inajenga miundombinu ya barabara, umeme, inasomesha wanafunzi, inajenga shule, inalipa mishahara ya wafanyakazi wake na mambo megine mengi. Hivyo, mfanye kazi kwa bidii na kwa weledi ili mkusanye kodi inayotakiwa kukusanywa kwa mujibu wa sheria bila kumuonea mtu yeyote." alisema Kichere.

Kichere aliongeza kuwa, wafanyakazi wote kituoni hapo wana wajibu wa kukusanya kodi ili kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo kwa kutumia mapato yanayokusanywa nchini kupitia kodi mbalimbali.

Aidha, Kamishna Mkuu huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama  pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano wanaoutoa kwa TRA.

"Nachukua fursa hii kukushukuru wewe Mhe. Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama na pia napenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Glorious Luoga kwa ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania," amesema Kichere.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alisema kwamba, mkoa wake umepanga utaratibu wa kufanya kikao kila mwezi ili kupitia taarifa ya ukusanyaji mapato mkoani humo.

"Kwa mkoa wa Mara kituo hiki cha Sirari ni muhimu sana na kina maslahi makubwa hususani katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, hivyo sisi kama mkoa tumejipanga kila mwezi kukaa pamoja kupitia taarifa ya TRA ili kupata viashiria vya maeneo muhimu ya ukusanyaji mapato ndani ya mkoa wetu," alisema Malima.

Naye Kaimu Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mkoa wa Mara Laurent Kagwebe ameushukuru uongozi wa mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika suala zima la ukusanyaji mapato mkoani humo na kusema kuwa ushirikiano huo ukiendelea, kuna dalili njema za kuongezeka kwa makusanyo hapo baadae.

"Nikili wazi kuwa, nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya mkoani hapa na kama ushirikiano huu ukiendelea, nina imani  kuwa, makusanyo yataongezeka kwa kiasi kikubwa," amefafanua Kagwebe.

Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kina jumla ya wafanyakazi 86 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyakazi hao wana jukumu la kulinda afya za wananchi kwa kukagua bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia kituo hicho, kulinda usalama wa raia pamoja na kukusanya mapato ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.