Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Akabidhiwa Taarifa ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Ikulu leo.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akipokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano (ZEC) kutoka kwa Mhe. Jecha Salim Jecha alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Wajumbe wa Tume yake leo


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kutekeleza vyema majukumu yake ndani ya miaka mitano kwa kuendesha chaguzi zote huku Zanzibar ikiendelea kuwa yenye amani na utulivu mkubwa.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha akiwa amefuatana na wajumbe wa Tume hiyo kumkabidhi Ripoti ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kilichoanzia tarehe 30 April, 2013 mpaka tarehe 29 April, 2018.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa Tume hiyo inastahiki pongezi kwa kuifanikisha vyema kazi waliyopea ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo Uchaguzi Mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa.

Dk. Shein alisema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilionesha juhudi kubwa na ilikuwa imara huku ikisimamia Katiba, Sheria na Kanuni za Tume hiyo na kusisitiza kuwa kwa niaba ya Serikali na wananchi wote wa Zanzibar inaipongeza Tume hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata.

Aidha, Rais Dk. Shein aliithibitishia Tume hiyo kuwa ameipokea kwa furaha kubwa Ripoti aliyokabidhiwa na Tume hiyo na kueleza jinsi alivyoridhika na Tume hiyo kutokana na utendaji wake wa kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano.

Aliongeza kuwa katika kipindi chote cha miaka mitano ya Tume hiyo hakuiingilia hata siku moja na aliiwacha Tume hiyo kufanya kazi zake  kwa uhuru na kuahidi kuwa hata Tume ijayo hatoiingilia na itaendelea kuwa huru.

Alieleza kuwa Taasisi hiyo iko huru na hakuna chombo chochote duniani kitakachoweza kuiingilia katika kazi zake huku akiipongeza kwa jinsi Tume hiyo inavyoendelea kupata heshima kubwa katika pembe zote za duniani.

Alisema kuwa Tume hiyo imeendelea kupata heshima kubwa duniani ikiwa ni pamoja na kuhudhuria katika vikao kadhaa vikiwemo vile vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na vyenginevyo ambapo hiyo yote inatokana na jinsi inavyofanya kazi zake kwa viwango kikubwa.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa licha ya kuwepo baadhi ya changamoto lakini kwa upande wake amechukua juhudi kubwa kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuwakabidhi jengo ambalo litafanywa ghala la Tume hiyo pembezoni mwa jengo la Tume hiyo hapo Maisara pamoja na kuwakabidhi kiwanja kwa ajili ya jengo la kisasa la Tume hiyo ambalo aliahidi kuwa litajengwa na Serikali.

Aidha, Dk. Shein aliahidi kuwa Serikali itanunua gari mpya za Tume hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 ambapo tayari imeshazifanyia ukarabati gari zote za Tume hiyo zilizokuwa mbovu.

Pia, Rais Dk. Shein aliwaeleza Wajumbe wa Tume hiyo ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Tume inafanya kazi zake kwa kutumia njia ya kisasa za sayansi na Teknolojia (TEHAMA) ili Zanzibar nayo isiwachwe nyuma.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha akitoa taarifa yake kwa Rais Dk. Shein alisema kuwa Tume inaamini kwamba, mafanikio yaliopatikana wakati wa utekelezaji wa majukumu ya Tume hasa wa kiuchaguzi yalitokana na ushirikiano wa Wadau mbali mbali na wananchi kwa jumla.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ndani ya miaka mitano Tume hiyo imeweza kuendesha jumla ya chaguzi ndogo nne, zikiwemo chaguzi ndogo tatu za Udiwani na chaguzi moja ya uwakilishi pamoja na kusimamia uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 na ule wa marudio yake tarehe 20 Machi 2016.

Aidha, Alieleza kuwa Tume hiyo imefanya mapitio ya Majimbo ya uchaguzi na kubadilisha mipaka ya Majimbo ya uchaguzi, majina ya Majimbo na kuongeza idadi ya majimbo kutoka 50 hadi 54.

Pamoja na hayo, alisema kuwa Tume hiyo imeweza kufanya uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu mbili na kuliendeleza daftari la kudumu la wapiga kura sambamba na kuendesha programu mbali mbali za elimu ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wadau, uchapishaji wa vipeperushi, majarida na makala mbali mbali.

Aidha, Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imechaguliwa kuwa kiongozi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini Kongo utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Mwenyekiti huyo pia, alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto mbali mbali za Tume hiyo huku akimueleza kuwa Ripoti hiyo itasambazwa sehemu mbali mbali zikiwemo Ofisi na Taasisi za Serikali, Mahkama, Baraza la Wawakilishi, Vyama vya Siasa, Maktaba Kuu, Maktaba za Vyuo vya Elimu ya Juu, Taasisi zisizo za Serikali pamoja na Wadau wengine mbali mbali.

Mwenyekiti Jecha alieleza kuwa Wajumbe walioteuliwa na Rais mnamo tarehe 30 Aprili mwaka 2013 ni Mwenyekiti wa Tume hiyo Jecha Salim Jecha na Wajumbe wengine ni Jaji Abdul-hakim Ameir Issa, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Nassor Khamis Mohammed, Ayoub Bakari Hamad, Haji Ramadhan Haji na Salmin Senga Salmin ambao wote hao waliapishwa rasmi tarehe 4 Mei 2013.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Maelezo ya Mwenyekiti huyo katika mkutano wake wa mwanzo wa Tume hiyo uliofanyika tarehe 9 Mei 2013 ulimteua Jaji Abdul-hakim Ameir Issa kuwa Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo uteuzi uliofanywa chini ya Kifungu cha 119(2) (b) cha Katiba ya Zanzibar huku akisisitiza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni chombo huru kilichoanzishwa chini ya kifungu cha 119(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.