Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.


Na Khadija Khamis - Maelezo Zanzibar. 25/06/2018
Kamati ya Bajeti ya Serikali imesema kuwa kushuka kasi ya mfumko wa bei hakujamsaidia mwananchi kumuwekea akiba kwa matumizi mengine .
Hayo yamesemwa huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar  wakati wa uwasilishaji wa hotuba ya kamati ya bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali  mwelekeo wa Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Akisoma kwa niaba ya Mwenyekiti Mjumbe wa Kamati hiyo Asha Abdalla Mussa  alisema kasi ya mfumo wa bei za bidhaa na huduma nchini imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 5.6 ukilinganisha na wastani wa asilimia 6.7 ya mwaka 2016 lakini bado hakujamrahisishia mwananchi kwani hali halisi ya bidhaa za chakula zinaongezeka kupanda bei kila siku.
Aidha alisema kuwa jambo hilo humfanya mwananchi kutumia sehemu kubwa ya kipato anachokipata kujipatia huduma ya chakula tu na kushindwa kujiwekea akiba ya matumizi mengine ya lazima.
Alifahamisha kuwa kamati hiyo imefarajika na mkakati wa serikali ya kupunguza kasi ya mfumko wa bei kwa kutoa punguzo maalum katika ushuru kwa bidhaa muhimu hasa za chakula.
Mjumbe huyo alisema kuwa bidhaa za chakula ni bidhaa muhimu kwani kila mtu anahitaji wa matumizi ya kila siku hivyo ameiomba serikali iweke mikakati ya muda mrefu itakayohakikisha uzalishaji wa chakula unaongezeka kwani athari ya kutopata chakula kwa kiwango kinachostahiki huduma nguvu kazi ya nchi.
Hata hivyo alisema kuwa kamati iliipongeza mamlaka ya uwekezaji wa ukuzaji vitega uchumi (ZIPA)kwa jitihada wanazozichukuwa ili kuhakisha uwekezaji nchini unaimarika kwa lengo la kukuza pato la taifa pamoja na soko la ajira.
Aidha kamati imeitaka serikali kuongeza jitihada ya kujitangaza katika matamasha na maonyesho ya kitaifa ili kuvutia wawekezaji na kuweza kupata masoko mpya kutoka nchi za Asia na mashirika ya mbali hususani katika sekta ya utalii.
Aidha kamati hiyo imetoa wito kwa serikali kupitia wataalamu wake wa uchumi kuhakikisha inafanyia kazi maeneo mbalimbali ambayo ni kivutio kwa wawekezaji ikiwemo mazingira mazuri ya kiuchumi na kumudu ushindani wa kibiashara na uchumi uliopo nchi zinazoendelea.
Alieleza kuwa ZIPA itaweza kutanua wigo wa uwekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar kwa kuanzisha aina nyengine za utalii ambazo ni utalii wa kimatibabu, utalii wa kielimu ambapo mpango huu utaimarisha upatikanaji w a huduma za afya na elimu zenye kiwango bora ambazo wananchi hutumia fedha nyingi kuzifuata nje ya nchi.
“Maeneo  yatakayopewa kipaumbele ni sekta ya utalii, miundombinu pamoja na kilimo ambazo zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi”, alifahamisha Mjumbe huyo.
Hata hivyo kamati imeshauri serikali kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa kwa utekelezaji wa maendeleo zinatolewa kwa ukamilifu na kwa wakati ili kukuza ajira na rasilimali fedha kwa wananchi ambayo ni muhimu kwa kuondoa wimbi la umasikini nchini.
Mwisho
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.