RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba,
Maji na Nishati kwa kutekeleza vyema majukumu yao na kuutaka kuandaa ziara
maalum za kazi kwa ajili ya kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto
zinazowakabili.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2017/2018, na Mpango Kazi wa Utekelezaji
kwa mwaka 2018/2019.
Dk. Shein alisema kuwa kwa vile Wizara hiyo
imeyagusa maisha ya wananchi ni vyema kwa uongozi huo kwenda kuwasikiliza ili
kutambua changamoto zinazowakabili na kuweza kuzipatia ufumbuzi kwani bila ya
kufanya hivyo inawapelekea wananchi kuanza kulalamika kupitia vyombo vya habari
jambo ambalo si busara.
Aliongeza kuwa kumsikiliza mwananchi ni sifa moja
wapo ya kiongozi hivyo ni vyema kwenda
kwa wananchi kuwasikiliza hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo imewagusa wananchi
kwa kiasi kikubwa kutokana na huduma zake inazozitoa ikiwemo maji, ardhi,
nishati, nyumba na mambo mengineyo.
Aidha, Rais Dk. Shein aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa Kamati ya Uongozi wa Wizara
hiyo ambayo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na kuwasisitiza
wajumbe wa Kamati hiyo kuhudhuria vikao husika ambavyo vina umuhimu mkubwa
katika kuiongoza Wizara hiyo.
Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuzingatia na
kufuata sheria na taratibu zinazoongoza Wizara hiyo huku akisisitiza haja ya
kuwaelemisha wananchi juu ya mambo mbali mbali ya Wizara hiyo ambayo wanapaswa
wananchi kuyajua zikiwemo sheria za Wizara hiyo.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji Mpango
Kazi huo iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa kila taasisi ya
Wizara hiyo kutoa huduma zake ipasavyo hasa kutokana na Wizara hiyo kugusa
maisha ya wananchi.
Nae Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati
Salama Aboud Talib alieleza kuwa tayari Wizara
hiyo imekamilisha Sera ya Ardhi ambayo kukamilika kwakwe kutaiwezesha Zanzibar
kuimarisha utawala na maendeleo endelevu ya ardhi na usimamizi wa maliasili
zilizomo katika ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo hapa nchini.
Waziri Salama alieleza kuwa lengo kuu la Sera hiyo
ni kukuza uchumi na kuimarisha thamani ya ardhi pamoja na kuendeleza usimamizi
wa matumizi bora ya ardhi.
Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa Wizara kupitia
Mamlaka ya Maji (ZAWA) imeendelea kusimamia shughuli za program za uhuishaji na
upanuzi wa shughuli za maji Mijini na
usambazaji wa maji vijijini.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa programu hiyo
Mradi wa uchimbaji wa visima na usambazaji wa maji unaofadhiliwa na Jamhuri ya
Watu wa China umefanikiwa kukamilisha ujenzi wa matangi matano ya maji katika
maeneo ya Kisongoni, Chaani na Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kiboje, na
Miwani kwa Mkoa wa Kusini Unguja.
Pia, Waziri huyo alieleza kuwa mradi huo
umekamilisha kazi ya uchimbaji wa visima 11 katika maeneo hayo na ulazaji wa
mabomba kwa masafa ya kilomita 20.17 kwa
maeneo ya mradi, pamoja na kupelekwa kwa umeme, fidia na tayari umeshakabidhiwa
Wizara.
Alieleza kuwa katika juhudi za kuimarisha
mazingira bora ya utekelezaji wa kazi tayari Wizara kupitia ZURA imeanza
kutekeleza shughuli za ujenzi wa jingo la Ofisi hapo Maisara ambalo linatarajiwa
kukamilika mnamo mwaka wka fedha 2019/2020.
Sambamba na hayo, Waziri huyo alieleza kuwa Wizara
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia
(ZPRA) imeendelea na zoezi la kukuza uelewa kwa jaimii juu ya masuala ya Mafuta
na Gesi Asilia Unguja na Pemba kwa kuendesha Semina, Mikutano, Makongamano
pamoja na kurusha hewani vipindi vya redio na televisheni.
Nao viongozi wa Wizara hiyo walimpongeza Rais Dk.
Shein kwa maelekezo yake anayoyatoa kwao hatua ambayo inawarahisishia kutenda
kazi zao huku wakimuhakikishia kuwa wanaendelea kutekeleza vyema kazi zao ili
kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment