Habari za Punde

Balozi Seif afunga mkutano wa pamoja wa kimataifa wa vyama vya siasa vya Afrika na Chama cha Kikomunisti cha China

 Naibu Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Chama cha Kikoministi cha Jamuhuri ya Watu wa China  Bibi Shuu Luping akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kuufunga Mkutanowa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na chama cha Kikoministi cha China hapo Serena Hoteli Jijini Dar es salaam.

Kati kati yao ni Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dr. Bashiru  Ali Kapura, na wa kwanza kutoka Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Nd. Philip Mangula.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunga Mkutanowa wa Pili wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na chama cha Kikoministi cha China hapo Serena Hoteli Jijini Dar es salaam.
 Naibu Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Chama cha Kikoministi cha Jamuhuri ya Watu wa China  Bibi Shuu Luping akitoa salamu za Chama cha Kikoministi mwishoni mwa Mkutano wa wa Pili wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na chama cha Kikoministi cha China hapo Serena Hoteli Jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Kinachotawala Nchini Cape Vade Bwana Miguel Petro akitoa salamu za Chama hicho mwishoni mwa Mkutano wa Pili wa Kisiasa Barani Afrika na chama cha Kikoministi cha China Jijini Dar es salaam.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Mataifa ya Bara la Afrika kwa sasa yamekuwa huru  kisiasa, kijamii na kiutamaduni baada ya kutawaliwa na wakoloni kwa karne kadhaa lakini ni ukweli usiopingika kuwa bado Mataifa hayo yanahitaji kuwa huru zaidi kiuchumi.

Alisema maamuzi ya awamu ya pili ya Uhuru ndani ya bara hili ni safari ya kujikomboa kiuchumi ambayo haitakamilika iwapo Waafrika wenyewe hawatosimama imara kupiga vita rushwa, ufisadi, kusimamia uwajibikaji, utawala bora, juhudi za ubunifu na utendaji wenye kuleta matokeo mema na yenye tija kwa Mataifa na watu wake.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufunga Mkutano wa pamoja wa Kimataifa wa Siku mbili wa Vyama vya Siasa kutoka Mataifa mbali mbali Barani Afrika na Chama cha Kikoministi cha Jamuhuri ya Watu wa China {CPC}uliofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Serena Jijini Dar es salaam.

Alisema katika masuala la ukombozi wa kiuchumi Mataifa ya Bara la Afrika yana kila sababu ya kujifunza kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambacho kimeendesha Mapinduzi ya uchumi ya aina yake ambayo hayajapata kushuhudiwa duniani kote.

Alieleza kwamba Taifa la China chini ya Chama cha CPC imeweza kuwakomboa wananchi wake wapatao 800 Milioni pale ilipoanza mapinduzi ya kiuchumi kutoka katika dimbwi la umasikini katika kipindi kifupi kwenye Miaka ya 80ambapo hivi sasa Taifa hili lenye Watu  Bilioni 1.2 wanaendelea kunufaika na mapinduzi hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Juhudi hizo zilizochukuliwa na Jamuhuri ya Watu wa China zimeiwezesha dunia kupunguza dimbwi la umasikini uliokithiri kutoka asilimia 40% hadi asilimia 10% na zaidi. 

“ Kama siyo China hali ya umasikini wa kupindukia duniani bado ingekuwa juu ya asilimia 10. Hivyo basi, kama kungekuwa na kombe la dunia la ushindi wa kuboresha uchumi imara, kombe hilo lingekwenda kwa Jamhuri ya Watu wa China”. Alisisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia Vyama vya Ukombozi Barani Afrika Malozi Seif alisema Uzoefu wa kuja kwa Vyama vyengine visivyokuwa vya ukombozi katika jukwaa la kisiasa Barani Afrika unaonyesha kuwa Vyama vya kisiasa vilivyoleta uhuru hasa Barani Afrika vinapigwa vita na mabepari na mabeberu duniani. 

Alisema Vita hivyo vina lengo la kuviondoa madarakani Vyama vya Ukombozi kitendo ambacho  Watanzania wanaamini vita hivyo vitashindwa kama Vyama Vilivyoleta Ukombozi vitaendelea kuwa Vyama vyenye kutetea maslahi ya wanyonge na kuhimiza utendaji kazi kwa maslahi ya wengi.

Alieleza kasi hiyo inayowalenga zaidi Wananchi waliowengi hupata baraka ya kuungwa mkono kwa vile inahimiza masuala ya kuimarisha elimu pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani. 

Balozi Seif ambae pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema kwa bahati nzuri Chama cha Mapinduzi CCM Tokea  kuanzishwa kwake kimekuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa kwa nguvu zake zote.

Alisema Chini ya Mwenyekiti wake Dkt John Pombe Magufuli vita dhidi ya rushwa vimeimarishwa nchini pamoja na kuongeza kasi ya usimamizi wa utendaji kazi wenye kuleta tija chini ya bango la Hapa Kazi tu.  

“ Juhudi hizi za Mwenyekiti wetu zimezaa matunda na kama alivyoeleza katika hotuba yake ya ufunguzi uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa”. Alisisitza Balozi Seif.

Akitoa salamu Naibu Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Chama cha Kikoministi cha Jamuhuri ya Watu wa China kilichoandaa Mkutano huo Bibi Shuu Luping alisema Chapa cha Kikoministi cha China {CPC} hakikufanya makosa kuichagua Tanzania kwa kufanyika kwa Mkutano huo.

Bibi Shuu alisema Tanzania ndio Nchi pekee ya mfano Barani Afrika iliyosimama kidete katika usimamizi wa Kuona Mataifa yote ya Bara hilo yanakomboka Kimaendeleo na kujitegemea Kiuchumi.

Alisema Mkutano huo wa uhusiano kati ya China na Mataifa ya Bara la Afrika kwa sasa maazimio yake ni vyema yakawa na muelekeo wa kujenga mkakati wa kuimarisha Uchumi kwa Mataifa yote ambayo hivi sasa yameshakomboka Kisiasa.

Alieleza kwamba pande zote mbili ambazo ni China na Mataifa ya Bara la Afrika zina wajibu wa  kutengeneza Sera za Kitaifa zinazoleta uchumi bora katika dhana nzima ya kuondoa au kupunguza dimbwi la umaskini ndani ya Bara kla Afrika.
Bibi Shuu alisema hivi sasa zipo njia nyingi za Uhusiano na ushirikiano kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Mataifa ya Bara la Afrika katika kuweka  msingi imara kwenye zama hizi mpya za kufungua fursa zaidi za Maendeleo yatakayostawisha maisha ya Wananchi walio wengi hasa Vijijini.

Naibu Mkuu huyo wa Idara ya Uhusiano wa Chama cha Kikoministi cha Jamuhuri ya Watu wa China aliwahakikishia Viongozi Washiriki wa Mkutano huo wa Uhusiano kati ya China na Afrika kwamba China na Afrika zitaendelea kushirikiana ili Mataifa yake yaweze kujikwamua Kiuchumi.

Mapema Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Kisiasa vya Afrika Bwana Nafia Ali Nafia alisema Afrika inapita katika mabadiliko makubwa ya Kisiasa kasi ambayo vyama vya Kisiasa vina wajibu wa kuwa makini katika kukabiliana na wimbi hilo.

Bwana Nafia alisema vyama vingi vya Kisiasa Barani Afrika vilishindwa kukidhi mahitaji ya Wanachama na Wananchi wao hasa baada ya kujitokeza kwa kero nyingi zikiwemo Ukame ulioambatana na Uwajibikaji mbovu.

Alifahamisha kwamba vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa vilichangia uwepo wa migogoro ya Kisiasa na hatimae kuibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyogharimu maisha mengi ya Wananchi wake wasio na hatia.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuufunga Mkutano huo wa Dunia Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dr. Bashiru Ali Kapura alisema Viongozi washiriki wa Mkutano huo wamekubaliana kwamba Vyama vya siasa ni muhimu na muhimili katika Ujenzi wa Uchumi katika Taifa lolote.

Dr. Bashiru alisema yapo makosa yaliyowahi kutokea kwa baadhi ya Viongozi wa Kisiasa ndani ya Bara la Afrika kuvitumia vyama vya Kisiasa kwa Mtaji wao wakishindwa kuelewa kwamba ndio silaha pekee ya kusimamia Uchumi na kujetegemea.

Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi aliwasisitiza Viongozi hao wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika ni vyema wakajiepusha na Umaskini wa fikra ambao ni mkubwa na hatari kulikochochote katika maisha ya kila siku ya Mwanaadamu.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.