Habari za Punde

Waziri wa Fedha na Mipango azindua Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji Mali za Serikal Zanzibar.

 Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Dkt. Khalid Salum Mohamed akizindua Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji Mali za Serikali  katika utekelezaji wa majukumu ya kazi zao huko Mazizini Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uondoshaji Mali  za  Serikali Zanzibar Abdulrahman Mwinyi jumbe  (kushoto) Mkurugenzi  wa  Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji Mali za Serikal Othman Juma Othman wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Bodi hiyo. 

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Khalid Salum Mohamed  katikati akiwa katika Picha ya pamoja na Wajumbe wa  Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji Mali za Serikal Zanzibar.
                Picha Na Miza Othman Maelezo –Zanzibar.


Na   Khadija Khamis –Maelezo    03/07/2018.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Khalid Salum Mohamed ameitaka Bodi ya Mamlaka ya ununuzi na uondoshaji wa mali za Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia maadili  na kujenga uwadilifu katika kuhakikisha wanafanyakazi kwa mujibu wa sheria .

Hayo aliyasema leo huko   katika ukumbi wa Ofisi ya Takwimu Mazizini wakati wa uzinduzi wa  Bodi  mpya  ya Mamlaka  ya ununuzi na uondoshaji wa mali za Serikali.

Alisema  kufanyakazi kwa ufanisi na kuzingatia maadili kutasaidia kuweka misingi madhubuti ya kazi na kuhakikisha fedha za Serikali zinalindwa na kusimamiwa ipasavyo .

Aidha alisema wajumbe wa Bodi hiyo ndio wasimamizi wakuu wa fedha za Serikali, hivyo iko haja ya kuhakikisha matumizi ya fedha yanatumika kisheria na kuwepo  usimamiaji  wa uhakika ili  kuepukana na ubadhilifu wa mali ya umma .

 “Matumizi yakienda kiholela holela kwa watendaji hatupati kitu lengo ni kuwapatia maendeleo wananchi wetu  katika sekta mbali mbali za kiuchumi ,huduma za  afya, miundombinu ikiwemo barabara majengo makubwa ya Serikali,  majengo ya skuli na kadhalika .”Alisema  Dkt Khalid.

Alifahamisha ununuzi wa vifaa unachukua fedha nyingi  za Serikali katika ujenzi ,bidhaa pamoja na huduma za wananchi   hivyo ndio maana  ikaanzisha  chombo hichi maalum cha kusimamia na kudhibiti matumizi ambayo huchangia kuzorotesha maendeleo ya taifa .

Alieleza chombo hichi kisimamiwe na kutoa muongozo katika masuala ya ununuzi wa bidhaa na kuhakikisha fedha iliyotumika inalingana na kifaa ambacho kimenunuliwa ili kwenda sambamba na sheria .

“Tusipokuwa waadilifu katika dhamana ambazo tumepewa tuhakikishe sisi ni wachache kulingana na kundi kubwa linalotutizama  na tunauangamiza umma tuheshimu sheria na taratibu zinazotuongoza pia tumuogope Mwenyezi Mungu ,”Alisema waziri wa fedha .

Nae Mwenyekiti wa Bodi hiyo  Abdulrahman  Mwinyi Jumbe alisema ingawa mwanzo ni mgumu lakini atahakikisha wanafanya kazi kwa uwadilifu na kuzingatia misingi ya sheria .
Alisema anaelewa kwamba nchi yetu iko katika mageuzi makubwa ya kiuchumi hivyo itaendeleza kuleta mabadiliko ili kuhakikisha yanapatikana  maendeleo endelevu  katika huduma za wananchi .

Nae Mkurugenzi  wa bodi hiyo Othmani Juma Othman amesema atawajengea uwezo wafanyakazi kwa kuweza kuwapa mafunzo mbali mbali ya kielimu ili kufanyakazi kwa ufanisi na kuacha kufanya kazi kwa mazowea .

Aidha alisema atahakikisha kila mfanyakazi anajulikana kipato chake , hivyo iwapo akionekana maisha yake yamepanda kwa haraka hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na wananchi watapewa elimu ya kuweza kutoa taarifa za kipato hicho katika sehemu zinakohusika 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.