Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Ujenzi wa Makao ya Nyumba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akitembelea na kuangalia ujenzi wa Majengo ya Nyumba za Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zinazojengwa katika eneo la Pagali Wilaya ya Chake chake, akiwa katika ziara yake kisiwani Pemba.
 Balozi Seif akikagua baadhi ya Majengo ya Nyumba za Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zinazojengwa katika eneo la Pagali Wilaya ya Chake chake Pemba.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Maalim Abdulla Mzee Abdulla akiteta na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwenye majengo ya Skuli Mpya ya Sekondari inayojengwa katika Kijiji cha Wara Chake Chake Pemba.
Mhandisi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Wara Ali Khamis Shaibu akimpatia maelezo Balozi Seif kuhusu ujenzi wa majengo ya Skuli hiyo unaokwenda kwa wakati uliopangwa.
Umma wa Wananchi wa Kijiji cha Mwambe waliokuwa wakisikiliza nasaha za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani alipofika kukagua Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari kwenye eneo hilo.
(Picha na OMPR)

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziubar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazidi  kuimarisha miundombinu ndani ya Sekta ya Elimu, Wanafunzi Nchini wanalazimika kujikita zaidi katika kutafuta Elimu itakayowajengea njia ya Maisha ya furaha wao na Familia zao.
Alisema wanafunzi hao wakiamua kusoma kwa juhudi na maarifa na kufikia kiwango cha Elimu ya juu ya Vyuo Vikuu watakuwa na nafasi pana ya kujihakikishia fursa za ajira zilizozoweya kufanywa na Wataalamu wa Kigeni.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akisalimiana na Wananchi wa Mwambe akiendelea na ziara yake ya kukaguwa Majengo mapya ya Skuli za Sekondari zinazojengwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mshirika wa Maendeleo Mfuko wa Kimataifa wa Opec.
Alisema Taifa linahitaji kuwa na Wataalamu wake wenyewe  watakaotokana na Wanafunzi wake ambao watapaswa kuweka malengo ya kusoma kwa bidii kwa lengo la kuwahudumia Wananchi kwa kiwango cha uzalendo zaidi.
Balozi Seif alimuhimiza zaidi Mtoto wa Kike Nchini kusoma kwa ziada ili zile kazi za Kitaalamu zinazofanywa na Wanaume akatolea mfano za huduma za Afya wazifanye wenyewe katika azma ya kulinda na kuheshima mila, sila, Tamaduni na hata imani za Kidini.
Katika kutilia mkazo nafasi ya mtoto wa kike kusoma kwa malengo Balozi Seif  ameagiza Wazazi wowote watakaohusika na kitendo cha kuwaozesha  Watoto wao wa Kike wakati wanasoma Uongozi wa Serikali ya Mkoa usimamie katika kuona Vyombo vya Dola vinawachukulia hatua za Kisheria mara moja Wazazi hao ikiwa ni pamoja na kuwaweka ndani.
“ Jamii inahitaji kuwa na Ewataalamu wa Kike ambao watahusika kushughulikia huduma zinazofanywa na Wanaume Kitaalamu ambazo hazistahiki kutokana na Tamaduni na Imani wa Kidini”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba tabia hii inayoonekana kuendelea kwa baadhi ya Mitaa Nchini inarejesha nyuma maendeleo ya Mtoto wa kike aliyekandamizwa kwa muda mrefu kutokana na mfume Dume uliozoeleka kwa kipindi kirefu kilichopita.
Alieleza kwamba matukio hayo  ni miongoni mwa matendo yanayoonyesha muendelezo wa unyanyasaji wa Kijinsia uliomgubika Mtoto wa Kike unaopswa kuondolewa hivi sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia yaliyoanza kumfunulia njia Mtoto wa Kike.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wazazi na Wananchi wa Mwambe kutokana na mwamko wao mkubwa wa kuwapelekea Skuli Watoto wao jambo ambalo linafaa kuigwa na Wazazi wengine Nchini.
Alisema Mikondo Mitatu ya Wanafunzi wanaoingia na kusoma kwenye Skuli ya Mwambe ni ushahidi tosha wa Wazazi hao kutambua uhumihu wa Elimu licha ya Idadi kubwa ya Wakaazi wake ambao Watoto wake walikuwa wakipenda sana kufanya kazi za U vuvi.
Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah alisema ziara zake za Majimbo Tisa akijumisha na maskuli yaliyombo kwenye Majimbo hayo  zimemthibitishia kukithiri kwa utoro kwenye Skuli nyingi za Mkoa huo.
Mh. Suleiman alisema bila ya Elimu hakuna Daktari, Mwalimu na hata Mhandisi, na katika kutambua umuhimu huo Serikali ya Mkoa imeamua kwa makusudi Mzazi ambae mtoto wake atatoroka Skuli atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumkosesha haki ya Elimu Mtoto wake.
Mkuu huyo wa Mkoa Kusini Pemba amewapongeza Swananchi wa Mwambe  kwa uwamuzi wao wa kuimarisha Ulinzi Shirikishi katika Shehia yao kitendo kilicholeta faraja na Amani katika eneo hilo.
Mh. Hemed alisema Kijiji cha Mwambe kilikuwa kikitajika kwa vitendo vya wizi wa mazao na ulevi vilivyosababishwa na baadhi ya Vijana waliokosa muelekeo kutokana na kukosa Taaluma ya Kimaisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua Maendeleo ya ujenzi wa Skuli za Sekondari za Mwambe na Wara Ndugukitu na kuridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Skuli hizo.
Balozi Seif aliwahimiza Wahandisi wa ujenzi wa Majengo hayo kuongeza jitihada ili kuhakikisha kwamba Miradi hiyo inakamilika katika wakati uliowekwa pamoja na kiwango cha hadhi inayokubalika ya kimajengo.
Mapema asubuhi Balozi Seif  alikagua Bara bara mpya inayojengwa kwa kiwango cha Lami katika Kijiji cha Ole hadi Kianga inayokadiriwa kuwa na urefu wa Kilomita 10.
Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Hemed Baucha alimueleza Balozi Seif kwamba kipande kilichobaki cha Bara bara hiyo kimechelewa kumalizika kutokana na Nyumba Nne zilizolazimika kuvunjwa kupisha ujenzi huo ambazo mwanzoni hazikuwamo.
Hata hivyo Nd. Baucha alisema Wataalamu wa Wizara hiyo wameshafanya tathmini na taratibu za malipo ya Fidia kwa Wananchi wanaohusika na Nyumba hizo zikamilike.
Balozi Seif alipongeza Wataalamu wa Idara ya Utunzaji na Ujenzi wa Bara bara {UUB} kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ambapo Serikali Kuu imeridhika na Taaluma waliyonayo Wahandisi hao wazalendo.
Alisema wakati Serikali inajitahidi kuangalia uwezekano wa kuwapatia vifaa zaidi vya ujenzi Wahandisi wa Idara hiyo lakini bado wana dhima ya kuhakikisha kazi wanazopewa wanazikamilisha kwa wakati muwafaka.
Wakati huo huo Balozi Seif  alifika Pagali kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ujenzi unaofanywa  chini ya Wahandisi wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo anzibar  Z{KMKM}.
Mshauri Muelekezi Mkuu  wa Ujenzi huo Mhandisi Ramadhan Mussa Bakari alimueleza Balozi Seif kwamba Ujenzi huo ulioanza Rasmi Tarehe 23 Juni 2018 unaendelea vyema licha ya changamoto ya uopatikanaji wa huduma za Maji.
Mhandisi Ramadhan alisema ili kazi hiyo iendelee kama ilivyopangwa na kukusudiwa upo umuhimu wa kuchimbwa Kisima ndani ya eneo hilo ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Akikagua baadhi ya Majengo ya Nyumba hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliridhika na kiwango pamoja na uharaka wa Wahandisi hao wanaouendeleza na kujenga matumaini yake ya kumalizika Mradi huo kwa wakati uliopangwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.