Habari za Punde

Umoja wa Falme za Kiarabu UAE Kufungua Ubalozi Mdogo Zanzibar.Na.Abdi Shamna, Zanzibar. 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema  Umoja wa Falme za Kiarabu  (UAE) unalenga kufungua Ubalozi mdogo hapa Zanzibar, kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Hatua hiyo itawezesha kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo, zenye  historia na ushirikiano a muda mrefu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ussi Haji Ussi ‘Gavu’, katika Hoteli ya Park Hayyat mjini hapa, wakati wataalamu kutoka UAE, walipokutana na Ujumbe wa Zanzibar, uliongozwa na Waziri huyo.

Ujumbe huo wa wataalamu 16 uliowasili nchini jana kwa ziara ya siku nne, umekuja nchini kwa lengo la kukazia na kuandaa taratibu za utekelezaji wa yale yaliokubaliwa kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, iliyofanyika UAE, January, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kikao hicho maalum, Waziri Gavu alisema  miradi mbali mbali kupitia sekta za Afya, Mawasiliano, Elimu sambamba na ukuzaji  ushirikiano kati ay nchi mbili hizo, itajadiliwa.

Mapema Waziri wa Nchi Ushirikiano wa kimataifa wa UAE Reem Ibrahim alisema,  Umoja wa Falme za Kiarabu unakusudia kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo, kw maslahi ay wananchi wake.

Alisema kuwasili nchini kwa ujumbe wa UAE utawezesha nchi hiyo kufungua milango ya uwekezaji kupitia sekta mbali mbali, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika katika kipindi kifupi kijacho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.