Habari za Punde

Elimu ya Zaidi Inahitajika Katika Huduma ya Mama na Mtoto Kupunguza Vifo Mama Wajawazito.

Na Mwashungi Tahir - Maelezo Zanzibar.   6-8-2018.
Elimu zaidi inahitajika kwenye Kitengo cha huduma ya 
mama na mtoto ili kupunguza vifo mama wajawazito wakati 
wa kujifungua na watoto wachanga ambapo takwimu 
zinaonyesha  vifo 1,091 vya watoto wachanga na  49 vya uzazi 
vilitokea katika kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Juni 2018 .

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa 
kipindi cha 2017/2018 kwa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya 
Baraza la Wawakilishi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Asha 
Ali Abdulla alisema sababu kuu ya vifo vya uzazi vinatokana 
na uelewa mdogo wa kinmama juu ya umuhimu wa 
kujifungulia hospitali na kuchelewa kufanya maamuzi ya 
kujifungulia hospitali.

Katibu Mkuu alizitaja sababu nyengine za kitaalamu 
zilizopelekea kutokea vifo hivyo ni kifafa cha mimba 
kinachosababishwa na sindikzo la damu, kupasuka kwa fuko 
la uzazi kunakopelekea kupoteza damu nyingi na 
maambukizi kabla na baada ya kujifungua.

Alisema Wizara ya Afya  inaendelea kusimamia  na kuratibu  
shughuli za huduma za mama wajawazito na watoto ili 
kuona wanapata huduma bora ambapo katika kipindi cha 
mwaka 2017/2018 jumla ya wajawazito 
94.181 waliohudhuria klinik angalau mara moja kabla ya 
kujifungua.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya alisema katika juhudi za Wizara 
hiyo kuimarisha huduma za afya ya uzazi na watoto 
wachanga, vifo vyote vinavyotokea hufanyiwa uhakiki ili 
kujua sababu yake na kutafuta mbinu za kupunguza vifo 
vinavyoweza kuepukika.

Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la 
Wawakilishi baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea vituo 
mbali mbali vya afya walieleza kuridhishwa na huduma bora 
zinazotolewa na watendaji pamoja na kuimarishwa vituo 
vingi vya afya.

“Tumeshuhudia huduma zinatolewa kwa kiwango kizuri na 
zinaridhisha, watendaji wanafanya majukumu yao kama 
inavyotakiwa, dawa na vifaa vinaridhisha kwenye vituo vingi 
tulivyotembelea”, alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi 
wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Mwanasha Khamis Juma.

Hata hivyo walisema Changamoto kubwa walioiona ni 
upungufu wa Madaktari Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, 
uhaba wa wafanyakazi kwa baadhi ya vituo vya afya na 
sehemu za uhifadhi wa dawa haziridhishi na kunaweza 
kusababishia uharibifu wa dawa zinapatikana kwa gharama 
kubwa.

Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Wizara ya Afya 
kufanya juhudi za makusudi kuongeza Madaktari, Wauguzi 
na Wakunga katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na vituo 
vya afya vya vijijini ili kazi za kuwahudumia wananchi ziwe 
na ufanisi mkubwa zaidi.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.