Na Takdir Ali,
Wanafunzi wametakiwa kuacha kutumia mitandao vibaya na badala yake waitumie kwa kujifunza ili iwasaidie katika mitihani yao ya Taifa.
Akizindua zoezi la usafi wa Mazingira Skuli za Mbarali ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 54 ya elimu bila malipo Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli hiyo Bw. Ramadhani Abdallah Rajabu amesema baadhi ya Wanafunzi wanaitumia mitandao kuangalia Picha za ngono jambo ambalo linasababisha kukosa ufanisi wa kuendelea na masomo.
Amewataka kuacha kujiingiza katika utumiaji wa Dawa za kulevya, Bangi, Wizi na Uhasharati ili kupata muda mzuri wa kudurusu masomo yao.
Mbali na hayo Mwenyekiti huyo amewasihi Waalimu kuchukuwa bidii ya kuhamasisha Wanafunzi kuitumia vizuri mitandao ya kijamii na kuwataka Wazazi kuwaunga Mkono Waalimu katika ufundishaji wao.
Hata hivyo amewataka wazazi kushirikiana na Waalimu katika kuhakikisha watoto wao wanapaitiwa elimu kama ilivyoagizwa na Sera ya elimu Zanzibar.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Meli 4 Swaleh Juma Kinana amewataka Wanafunzi kuwa na Hekima,Busara na ustahamilivu ili waweze kufikia malengo waliojipangia ya kupata elimu itakayowaongoza katika maisha.
Nao Waalimu wa Skuli hiyo wamesema wapo mstari wa mbele katika kuwahamasisha Wanafunzi wao kupenda kudurusu masomo yao na kukabiliana na wakati uliopo wa Sayansi na Teknolojia.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.
No comments:
Post a Comment