Habari za Punde

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII AWAASA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA NIDHAMU YA HALI YA JUU


Na.Lusungu Helela. 

Meja Jenerali Millanzi ameelezea kufurahishwa kwake na ushirikiano alioupata kutoka kwa watumishi wa Wizara hiyo na kuelezea kuwa, ndio umemwezesha kuiongoza vema wizara hiyo kwa kipindi alichokuwepo madarakani na kupelekea mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Wanyamapori, Utalii, Misitu na Nyuki na Malikale.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii imepata mafanikio makubwa katika  vita dhidi ya ujangili  ambayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopatikana kutoka kwa watumishi wa Wizara, wananchi, Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa Wanyamapori.

“Katika Kipindi tulichokuwa  pamoja, kuna mambo mengi tumeyakamilisha. Nimefanya kazi nanyi na kila mmoja wenu alikuwa akinisaidia ili Wizara yetu iweze kusonga mbele. Hakuna hata mmoja aliyeonyesha kutaka kunikwamisha. Ninawashukuru sana”Alisema Meja Jenerali Millanzi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kumuaga Meja Jenerali Gaudence Millanzi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa UDOM jijini Dodoma  na kuhudhuriwa na watumishi wapatao 113 wa Wizara hiyo, Kaimu katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Aloyce Nzuki, amempongeza Meja Jenerali Gaudence Millanzi kwa kumaliza salama Utumishi wa Umma na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kipindi kirefu.

Amesifu Meja Generali Millanzi kwa umahiri wake katika utendaji hasa namna alivyoweza kufanya kazi na raia kwa ushirikiano wa hali ya juu wakati yeye ni mwanajeshi.

“ Umefanya mambo makubwa kwa kuweka mifumo mizuri pamoja na kubuni mikakati na mbinu za kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Wizara kiutendaji na 
kuhakikisha watumishi wanapata utulivu wa akili kwa kujali maslahi ya watumishi na haki zao na hivyo kuwawezesha kufanya kazi wakiwa na utulivu wa akili jambo liliongeza ufanisi katika kazi.”ameelezea Dkt. Nzuki.

Akitoa Shukrani kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa Dkt. Nzuki wakati akiiongoza Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Millanzi amesema, amepata ushirikiano mkubwa kiutendaji kutoka kwa Dkt. Nzuki na kuwaasa watumishi wote waendelee kutoa ushirikiano mkubwa kwa Kaimu Katibu Mkuu huyo  na kwa viongozi wengine wa Wizara ili kuhakikisha Malengo ya Kitaifa yanafikiwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Ni muhimu sana kuhakikisha tunamuunga mkono Rais wetu Mhe. John Pombe Magufuli katika juhudi kubwa anazozifanya kuhakikisha tunapata nyenzo za kutuwezesha kuongeza idadi ya watalii nchini ikiwemo ununuzi wa ndege ujenzi wa miundo mbinu ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege na madaraja ya juu kwa juu (Fly overs) jambo ambalo litarahisisha huduma za usafiri na kuondoa kero ya foleni kwa raia na wageni na hivyo kuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii nchini.
Meja Jenerali Millanzi amesema, pamoja na kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa watumishi, lakini anaamini kuwa yapo maamuzi aliyoyafanya ambayo anaamini hayakuweza kumfurahisha kila mmoja lakini yalikuwa mazuri kwa maslahi ya nchi. Na huu ndio uongozi.
Ameongeza kuwa “ Ninamshukuru MUNGU nimestaafu salama kwani Wizara ya Maliasili na Utalii ni Wizara Muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na inagusa maslahi ya wengi. Wakati huo huo jukumu nililopewa na Mhe. Rais ni kusimamia maslahi ya nchi na si ya mtu mmoja mmoja hivyo naamini kuna maslahi ya watu yalivurugwa na hivyo mimi kuwa mwiba kwao.”
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bwana Lusius Mwenda amesema, kwa kipindi kifupi alichofanya kazi na Meja Jenerali Gaudence Millanzi amepata kujifunza mambo mazuri kutoka kwake akiwa kiongozi  Mtendaji wa Wizara hiyo.
Ameyataja mazuri hayo kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka, uwezo wa kusikiliza walio chini yake kiumakini na kutoa maamuzi yenye busara pamoja na kujali maslahi ya Watumishi.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mtumishi Eliud Kilo amemwelezea katibu Mkuu huyo kuwa, alikuwa kiongozi wa watu aliyekuwa akisikiliza shida za watumishi wake ikiwa ni pamoja na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.”
“Katibu Mkuu tulikupenda sana kwa jinsi ulivyokuwa ukifanya kazi na sisi.” Amesisitiza Mtumishi Eliudi.
Wakielezea namna walivyofanya kazi na Meja Jenerali Gaudence Millanzi, baadhi ya Watumishi waliopata fursa ya kutoa maoni yao kuhusiana na Katibu Mkuu huyo, wamesema, Kwa staili yake ya uongozi, ukiwa hujakamilisha kazi aliyokuagiza, utajikuta moyo wako unakusuta na kujikuta bila ya kusukumwa na mtu unabakia ofisini kuhakikisha unakamilisha kazi yako ili usijikute ukimkwaza kiongozi huyo mahiri aliyewapenda na kuwaheshimu watu walio chini yake. Tunatamani angeendelea kutuongoza na kukamilisha malengo tuliyokuwa tumejiwekea kiwizara. Watumishi hao walimuombea kila la heri katika maisha yake ya Kustaafu.
Meja Jenerali Gaudence Millanzi aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii mwezi Disemba 2015 na kustaafu Jeshi na Utumishi wa Umma tarehe 16 Mwezi Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.