Habari za Punde

Balozi Atembelea Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba. Ikiwa ni Maandalizi ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia mazingira halisi ya Uwanja wa Michezo wa Gombani Kisiwani Pemba unaotarajiwa kuhudumia Sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.Nyumba ya Balozi Seif ni Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mihayo Juma Nh’unga na Kulia ya Balozi Seif ni Meneja wa Uwanja wa Michezo wa Gombani Issa Juma Issa.
Katibu wa Sekriterieti ya Kamati ya Kitaifa ya Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Abdullah Hassan Mitawi akitoa ufafanuzi wa maadnalizi yaliyoanza kuchukuliwa na matengenezo ya Uwanja huo wa Gombani.
Balozi Seif akimhakikishia Meneja wa Uwanja wa Michezo wa Gombani kwamba Serikali itachukuwa hatua za kuufanyia matengenezo Uwanja huo ili ukidhi vigezo na mahitaji halisi ya hadhi ya Uwanja huo Kimataifa.Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Matayarisho ya awali ya kuufanyia matengenezo Uwanja wa Michezo wa Gombani Chake chake Kisiwani Pemba yameanza ili kukidhi mahitaji ya Sherehe pamoja na Kilele  cha Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  ya Mwaka 1964.
Kilele cha Maadhimisho hayo Kitaifa kimepangwa kufanyika katika Uwanja huo wa Gombani Kisiwani Pemba ambapo wageni mbali mbali wanatarajiwa kualikwa kuhudhuria Sherehe hizo za aina yake.
Katibu wa Sekriterieti ya Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdulla Hassan Mitawi alieleza hayo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kuukagua Uwanja huo utakaoleta haiba nzuri ya kufanikisha Maadhimisho hayo.
Mitawi alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia Michezo, Taasisi inayosimamia huduma za Maji pamoja na ile ya huduma za Umeme zinasubiriwa kupeleka Bajeti zao ili Matengenezo hayo yaanze kutekelezwa.
Alisema Uwanja huo umebahatika kuwa na Vyumba Vitatu vya Viongozi na Watu Mashuhuri {VIP} pamoja na vyoo 147 kikiwa Kiwanja pekee chenye vyoo vingi Barani Afrika.
Mitawi alisema Wataalamu pamoja na Wahandisi wa Masuala ya Ujenzi wanatarajiwa kushirikishwa katika matengenezo hayo ili kuona Uwanja huo unakidhi vigezo vyote vya kuhudumia bila ya kuleta athari yoyote ya kiufundi.
Mapema Meneja wa Kiwanja cha Gombani Issa Juma Issa alisema lipo tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma za Maji na umeme kwa kipindi kirefu sasa licha uwepo wa huduma hiyo ya  maji kutoa mita chake karibu na uwanja huo.
Issa alisema ipo haja kwa sasa ya kuchimwa kwa kisima kitakachokuwa kinajitegemea chenyewe kuhudumia uwanja huo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya vyoo vinavyopaswa kuwa na huduma ya maji wakati wote.
Alisema hivi sasa ni mifereji miwili tu inayotoa maji katika uwanja huo wakati mfumo wa huduma ya umeme haujafanyia marekebisho tokea kujengwa kwa Kiwanja hicho.
Akizungumza na Uongozi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alizihimiza na kuzikumbusha Taasisi zote zinazohusika na maandalizi ya Sherehe hizo kutekeleza wajibu wao ili wakati utakapokaribia kusiwe na changamoto yoyote itakayosababisha kuvuruga kwa mipango hiyo.
Alisema wakati ndio huu kuanza kufanya maandalizi ya mambo mbali kwani Mwezi Disemba hauko mbali unaotoa uthibitisho wa mafanikio ya maandalizi ya sherehe hizo.
Balozi Seif  alielezea matumaini yake kutokana na Wajumbe wa Kamati mbali mbali zilizopewa jukumu la kusimamia maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kwa kuanza kukutana na kupanga jinsi watakavyotekeleza majukumu hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.