Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Wanafunzi wa Kidatu cha Sita na Kidatu cha Nne Zanzibar waliofanya vizuri mitihani yao ya Taifa kwa mwaka wa masomo 2017/2018, wakati wa hafla ya chakula maalum alichowaandaliwa kwa ajili ya kuwapongeza na kuwakabidhi zawadi, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka
wanafunzi kuongeza kasi katika kusoma masomo ya Sayansi na Sanaa kwani bado Zanzibar
inahitaji wataalamu wengi zaidi katika fani mbali mbali ili kwenda na
mabadiliko ya karne ya 21.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika hafla ya kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi wa Kidato cha Nne na
cha Sita waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa na kula nao chakula cha
mchana, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa
na viongozi mbali mbali akiwemo makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd na viongozi wengine.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa kila nchi ina mahitaji ya wataalamu wa fani za Sayansi na Sanaa, wakiwemo
madaktari, wahandisi, marubani, viongozi, wanasheria, wanazuoni, mashekhe na
fani nyenginezo.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutangaza rasmi kuwa Serikali imetoa udhamini wa nafasi 30 kwa wanafunzi
waliopata daraja la Kwanza kwenda kusoma vyuo vya ndani na nje ya Zanzibar huku
akisisitiza kuwa Serikali anayoingoza haitosita kufanya hivyo katika uongozi
wake.
Alisema kuwa Serikali
inathamini sana juhudi za wanafunzi hao katika kutafuta elimu na ndio kila
mwaka amekuwa akiongeza nafasi za udhamini kwa wanafunzi wanaopata daraja la
kwanza.
“Nilianza na wanafunzi wa
daraja la kwanza Kidato cha sita 10 baadae wanafunzi 15 na sasa Serikali imeongeza
hadi wanafunzi 30 waliopata daraja la kwanza”, aliongeza Dk. Shein.
Alieleza kufurahishwa
kwake na taarifa ya wanafunzi 126 wanawake 48 na wanaume 78 wa Kidato cha sita
katika mwaka huu wa 2018 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza na wanafunzi
wanawake 61 na wanaume 74 ambao ni jumla ya wanafunzi 135 walifanya mitihani ya
Kidato cha Nne mwezi Novemba mwaka 2017 wamepata daraja la kwanza.
Aliwapongeza wanafunzi
wanaume kwa kuweza kupata daraja la kwanza kwa wingi zaidi kuliko wanafunzi
wanawake kutokana na mwaka jana kuwatia moyo na hamasa katika sherehe kama hizo
huku akieleza kuwa anaamini kwamba mwakani wanawake wataendelea kushika nafasi
yao ya kuongoza.
Aliwapongeza wanafunzi hao
wote kwa kufanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Biashara na Sanaa na kutoa pongezi
maalum kwa mwanafunzi Biubwa Khamis Ussi na Fahad Rashid kwa kupata Daraja la
Kwanza la kiwango cha point 3 kila mmoja na kuwemo katika orodha ya wanafunzi
10 bora katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, aliwapongeza wote
waliopata daraja la kwanza kwa kuwa wameijengea sifa Zanzibar na
kuwadhihirishia wananchi, wazazi na walimu wao kwamba katika mazingira
yaliyoandaliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa kupata daraja la
kwanza kwenye mitihani ya Taifa inawezekana katika masomo ya Sanaa.
Rais Dk. Shein alitoa
pongezi maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud kwa
kutoa zawadi ya Kompyuta 96 aina ya Laptop tarehe 04 Septemba mwaka 2018 katika
viwanja vya Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Mwembe Kisonge kwa wanafunzi wa
Kidato cha Sita wote waliopata daraja la kwanza katika Mkoa wake.
Alimpongeza kwa dhati
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdalla Juma Mabodi kwa kushirikiana na viongozi
wengine wa CCM kwa kuwapongeza na kuwazawadia vijana waliofanya vizuri pamoja
na kuipongeza Mikoa yote ya Pemba pamoja na Mkoa wa Kaskanini Unguja kwa
kufanya hivyo.
Rais Dk. Shein
aliipongeza Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kuwazawadia vijana hao na kuahidi
kuwa huo ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kuwaandaa vijana ili wawe mabingwa wa
fani mbali mbali na bila shaka juhudi hizo zitaendelezwa kwa nguvu na
mashirikiano makubwa.
Alieleza kuwa mwakani
sherehe kama hizo atazifanya kubwa zaidi na ziwe za aina yake wakati wa usiku
ili vijana washereheke kwani ni kumbukumbu ya maisha yao huku akieleza kuwa
juhudi hizo ni azma ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
”Sherehe hizi ni sehemu
ya kazi…..na kama mnavyojua kuwa ukiona vyaelea ujue vimeundwa”, aliongeza Dk.
Shein.
Kutokana na juhudi kubwa
za kusoma za wanafunzi hao Rais Dk. Shein alimnukuu mwanasoka maarufu Duniani,
Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele pale aliposema
“Mafanikio sio ajali ni
kazi ngumu inayotaka jitihada za wakati wote kujifunza, kusoma, kujitolea na
miongoni mwa yote hayo ni mapenzi kwa yale unayotaka kufanya ama kujifunza”.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
walimu, wazazi, walezi na wale wote walioshiriki katika kuwalea, kuwasomesha na
kuwatayarisha wanafunzi hao hadi wakapata matokeo mazuri yanayofurahisha.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuandaa utaratibu wa
kuwazawadia walimu waliofanya vizuri katika kuwasomesha na kuwaandaa wanafunzi
katika mitihani yao ya Taifa hapo mwakani ili nao wazawadiwe katika siku kama
hiyo.
Kwani alisema kuwa
kufanya hivyo kutawapa ari, nguvu na hamasa walimu wengi zaidi kufanya vizuri
katika ufundishaji na utayarishaji wa wanafunzi kwa ajili ya mitihani yao.
Pia, aliuagiza uongozi
wa Wizara hiyo uandae utaratibu wa kuzizawadia skuli mpya zilizojengwa katika
kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya uongozi wake kwani aliwashaagiza kufanywa
hivyo wakati akitoa hotuba yake ya majumuisho ya ziara ya Mkoa wa Kusini Pemba
Agosti 19 mwaka jana 2017.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alisema kuwa tamko alilolitoa Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Mzee
Abeid Amani Karume la kutangaza elimu bure kwa wananchi wa Zanzibar bila ya
ubaguzi ndio msingi wa mafanikio ya maendeleo yanayopatikana hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa kila
Mzanzibari mwenye elimu hivi sasa kwa njia tafauti amefaidika na juhudi za
Serikali za kutoa elimu bila ya Malipo. “haitofilisika Serikali kwa kutoa elimu
bure na afya bure kwani ndio Sera ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo jambo la tatu
ni ardhi ambayo yote ni mali ya Serikali”, alisema Dk. Shein.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
kuendeleza utamaduni wake huo na kumuahidi kuwa Wizara yake itaendelea kumuunga
mkono na kuimarisha juhudi katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika.
Waziri Pemba alimpongeza
Rais kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu na sekta ya afya ambazo zote kwa
pamoja zinaenda sambamba katika kuleta matokeo mazuri ya mitihani ya wanafunzi
ikiwa ni pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alitumia fursa hiyo
kuwasisitiza vijana hao kuwa wazalendo kwa nchi yao na kusisitiza kuwa Wizara
yake inaendelea kupata nafasi kadhaa za masomo ndani na nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Dk. Idrisa Muslim Hija alisema kuwa wanafunzi wa
Kidato cha Nne jumla ya wanafunzi 11,402 walifaulu kwa madaraja mbali mbali na
jumla ya wanafunzi 142 wamefaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza na kati ya
wanafunzi 1,777 wa Kidato cha Sita wanafunzi 126 wamefaulu kwa kiwango cha
daraja la Kwanza.
Katibu Mkuu huyo alitoa
pongezi kwa jitihada za Rais Dk. Shein pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar za kuiendeleza sekta ya elimu juhudi ambazo zimeiwezesha Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali kupeleka vitabu na vifaa vya maabara katika skuli
zote zenye Kidato cha Tano na Sita kwa masomo yote.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment