Habari za Punde

Kuandaliwe Kwa Program ya Pamoja Kuimarisha Uvuvi wa Bahari Kuu.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na mwenyeji wake Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Uhuru Kenyatta, baada ya Uzinduzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi Endelevu wa Bahari,(Sustainable Blue Economy) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kenyatta Nairobi Kenya leo.  

Na. Suzan Kunambi Nairobi Kenya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe Dk.Ali Mohamed Shein, alisema kuwa Kenya na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla zina uhusiano wa kihistoria na kindugu ambao ni lazima uimarishwe na uendelezwe kwa faida ya pande zote mbili.
 Dk. Shein aliyasema hayo wakati akizungumza  na Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta mjini Nairobi . Katika mazungumzo hayo,Dk. Shein  alisisitiza juu ya   ushirikiano katika kuendeleza uchumi wa bahari kuu baina  Kenya  na  Zanzibar na Jamhuri ya Muungano ya  Tanzania kwa jumla.
 Dk. Shein  alisema kwamba    watu wa Tanzania ni ndugu na  wamoja kwa hivyo ni muhimu pande mbili hizo kuzidisha ushirikiano  huo uliopo katika  masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia suala la  kuendeleza uchumi wa bahari kuu, Dk. Shein alishauri kwamba  ni muhimu    kuandaliwe programu ya pamoja  ya kuimarisha uvuvi wa  bahari kuu,   hatua ambayo ni muhimu katika jitihada zinazoendelea za kukuza ajira kwa vijana  na kuwa na matumizi bora  ya rasilimali za  bahari.
Vile vile, katika  kufanikisha   mikakati na mipango iliyopo ya kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za  bahari, mito na maziwa alisema kwamba ni vyema nchi hizo zikahakikisha kwamba sekta binafsi zinashirikishwa kikamilifu.

Aidha, Dk. Shein alipendekeza kwamba  itakuwa ni vyema kuanzisha utaratibu ambao utaziwezesha timu za viongozi  na wataalamu kutoka pande mbili hizo kukutana mara  kwa mara, ikiwa ni hatua muhimu ya kujadili mafanikio na changamoto mbali  mbali zinazojitokeza katika sekta hiyo. Aliongeza kusema kwamba hatua hiyo  ni muhimu  katika kuimarisha uhusiano uliopo.
Kwa upande wake, Rais  wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Ali Mohamed  Shein na ujumbe aliofuatana nao  kwa  kwa kukubali mwaliko wa kuhudhuria katika mkutano wa Kimataifa wa Uchumi Endelevu  wa bahari unaoendelea nchini humo.
 Rais Kenyatta alipongeza uamuzi wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuanzisha safari za meli baina ya Zanzibar na Mombasa kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri, biashara na kuendeleza uhusiano wa kidugu na kihistoria  uliopo baina ya wananchi wa pande mbili hizo.
Vile vile, alishauri kwamba itakuwa ni vyema hivi sasa kuimarisha huduma za usafiri kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja  baina ya  Zanzibar na Mombasa, ili kufanikisha utekelezaji wa   mipango na mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii, hasa ikizingatiwa kwamba sekta hiyo ni muhimu kwa uchumi wa pande zote mbili. 
 Alisema kwamba hivi sasa wapo watalii wengi  wanaotembelea  Mombasa  ambao wangependa  kusafiri moja kwa moja kwenda Zanzibar lakini hushindwa kufanya hivyo kutokana na kukosekana kwa usafiri wa aina hiyo.
Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, alihimiza haja ya kuimarsiha mikakati iliyopo ya kudhibiti uvuvi haramu katika mwambao wa Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha  hali ya usalama katika ukanda huo.
  Katika kikao hicho viongozi hao walikubaliana ziwepo ziara za mara kwa mara za viongozi wa ngazi mbali mbali la kuongeza maelewano na kuhakikisha utekelezaji wa mambo wanayokubaliana .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.