Habari za Punde

NBS Tunachangamkia Tekinolojia Mpya ili Kuongeza Ubora wa Takwimu na Kupunguza Gharama za Ukusanyaji Takwimu


Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema inachangamkia matumizi ya tekinolojia za kisasa katika ukusanyaji wa takwimu kuhakikisha inazalishaji takwimu zenye ubora wa hali ya juu pamoja na kuipunguzia serikali mzigo wa gharama kubwa za kuzalisha takwimu rasmi.

Mkuu wa Kitengo cha Mfumo wa Taarifa za Kijiografia wa NBS Benedict Mugambi akizungumza wakati wa mafunzo ya wiki moja ya matumizi ya tekinolojia mpya katika ukusanyaji wa Takwimu amewaambia waandishi wa habari kuwa matumizi ya tekinolojia hizo yataisaidia NBS kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizokumbana wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Tumeelekeza macho na nguvu zetu katika kupata tekinolojia mpya ili tuzitumie kukusanya takwimu zenye ubora wa hali ya juu huku tukitumia gharama kidogo tofauti na huko nyuma  alisema Mugambi.

Alibaianisha kuwa mafunzo hayo, ambayo yanafanyika katika Ofisi za NBS jijini Dodoma, yanayoendeshwa kwa msaada wa  wataalamu kutoka Benki ya Dunia na Mradi wa Data Zetu unawapatia watumishi wa NBS na wizara za Serikali ujuzi wa kutumia tekinolojia inayotumia mfumo wa OpenDataKit (ODK) na OpenMapKit (OMK).

NBS ina bahati ya ushirikiano mzuri na wadau hivo kuvutia ushirikiano katika mafunzo kama haya na kama kawaida imewashirikisha wataalamu wengine kutoka serikalini na taasisi zake ili kujenga timu moja nzuri ya wataalamu katika mbinu za matumizi ya tekinolojia mpya kukusanya Takwimu zenye ubora”

Aliongeza kuwa tekinilojia hizo zitarahisisha kazi ya usimamzi wa ukusanyaji taarifa kwa kuwa wasimamizi na wakusanya taarifa watakuwa wameunganishwa kwa mtandao hivyo zinakupa fursa ya kufahamu kama mhusika amefanya kazi au la na kama amefanya kazi amefanya wa kiwango na gani na kwa ubora gani.

Wakati huo huo, Mtaalamu Mshauri wa masuala ya Geo-spacial wa Benki ya Dunia Deogratius Minja amesema benki hiyo inashirikiana na NBS kutoa mafunzo hayo ili kuijengea uwezo kuendelea majukumu yake ya kutoa takwimu rasmi zenye ubora.

“Sote tunafahamu umuhimu wa takwimu na sisi kama mshirika ni dhamira yetu kuona NBS inaendelea na jukumu lake la kutoa takwimu rasmi zenye ubora kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ulimwengu kwa jumla alisema Minja.

Aliongeza kuwa Benki ya Dunia imefurahishwa na mwitikio mzuri wa wadau ikiwemo Serikali wa kutumia Mfumo wa Ramani Huria ambazo zina ubora wa hali ya juu hivyo kuwezesha kutumika kwa masuala mengi ya kitakwimu.

“Picha za ramani huria zilizo katika mfumo wa digitali inasaidia katika mfumo wa umiliki wa ardhi, inazisaidia manispaa kukadiria kodi za majengo kwa kuwa majengo yote yaliyomo katika maeneo yaliyopigwa picha yanaonekana vilivyo aaeleza Minja.

Aidha, amesema picha za kutumia vifaa vya drone zinasaidia katika kukabiliana na majanga ambapo vifaa hivyo kurushwa na kuchukua picha katika maeneo ambayo hayafikiki kutokana na uharibifu wa mafuriko.

Mtaalamu huyo ameeleza kuwa Benki ya Dunia imefurahishwa kuona kuwa kuwa idadi ya watu wanaofaidika na mfumo huu imeongezeka kutoka 25 mwaka 2001 hadi sasa zaidi ya wafunzi 400 wamepata mafunzi kupitia ratiba zao za mafunzo kwa vitendo.

Kwa upande wake Iddi Chazua kutoka Mradi wa Data Zetu alieleza kuwa matumizi ya mfumo wa OpenDataKit (ODK) ambao unatumia simu za mkononi kukusanya taarifa ni mfumo rahisi usio na gharama lakini wenye uwezo mkubwa wa kuchukua data aina zote.

Mafunzo kama hayo yatafanyika tena mwishoni mwa mwezi huu ambapo yatashirikisha wataalamu kutoka wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.