Habari za Punde

WAZIRI MKUU AMPA SIKU SABA WAZIRI MWIJAGE KUSIMAMIA KIBALI CHA BM MOTORS


Na scolastica Msewa, kibaha
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amempa siku saba Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linatoa kibali kwa kampuni ya BM Motors cha kutengeneza na kuunganisha bodi za magari. 

Waziri Mkuu alisema hayo wakati akifunga maonesho ya Wiki ya Viwanda yaliyomalizika mkoa wa Pwani, katika Uwanja wa Sabasaba,Picha ya Ndege,  Kibaha.

Alimtaka Waziri Mwijage, ifikapo Ijumaa wiki ijayo ampe taarifa ya maendeleo ya kampuni hiyo kuhusiana na kibali hicho kutoka TBS.

Alisema wakati mwingine huo ni urasimu, kama ana tatizo ambiwe aboreshe hawezi awe amekaa tangu mwaka jana analalamika hajapata kibali cha kutengeneza mabodi.”

Na kwa nini msimpe hiyo fursa atengeneze bodi halafu mmwambie  arekebishe na mkiwa mmejiridhisha kama ana uwezo wa kutengeneza hayo mabodi na Watanzania waendelee kutengeneza hapa nchini,  badala ya kuagiza nje kwa gharama kubwa haina maana” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aliongeza kuwa  “ulisema unaogopa kutumbuliwa (Mwijage), sasa sikutumbui nakupa wiki moja nipate taarifa ya mwenendo wa kampuni yetu ya ndani inayotaka kuunganisha mabasi.”

“Kwanza ni kampuni pekee inayotaka kuunganisha magari nchini, apewe fursa atujengee magari ya luxury (ya starehe) hapa Tanzania, alifafanua.

Mapema Waziri Mwijage akisalimia wananchi, alisema kwamba mashirika yaliyo chini ya wizara yake yakifanya kinyume yanahatarisha ajira yake, na yeye hayuko tayari kwa hilo.

Waziri Mkuu, aliutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kujipanga kwa kuandaa maonyesho ya viwanda kama hayo kila mwaka, ili wajasiriamali wapate fursa ya kuonyesha bidhaa zao.
Pia aliagiza miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kutumia bidhaa zinazotengenezwa nchini zikiwemo saruji, nondo na mabomba.

Akizungumzia eneo linalomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha lililopo Kibaha, Pwani, Majaliwa alisema shirika hilo liendelee kutafuta wawekezaji zaidi kwa eneo hilo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Evarist Ndikilo wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mkoa  huo,  alisema shirika hilo limepata mwekezaji ambapo limetenga eneo la hekta 38.8  kwa ajili ya ujenzi wa shughuli za kibiashara kama hoteli na maduka makubwa,  na hekta 100 ambazo zimetengwa kwa ajili ya makazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.