Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar Yatiliana Saini na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.Tiba ya Moyo,Mifupa,Ngozi na Upandikizaji wa Vifaa Vya Kusikia na Figo.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Jamala Adam Taib na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Laurence M. Museru wakitia sain mkataba wa ushirikiano wa utoaji huduma katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara Mnazimmoja mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Jamala Adam Taib na Profesa Laurence M. Museven wakibadilishana hati baada ya kutiliana saini mkataba wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Laurence M. Museru akizungumza na waandishi wa habari baada ya  kutiliana saini Mkataba wa ushirikiano na Wizara ya Afya Zanzibar (kulia) Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya (wa kwanza kulia) Mshauri wa Waziri wa Afya Dkt. Mohamed Jidawi na (kushoto) Mwanasheria wa Hospitali ya Muhimbili Veronica Hellar.
                              Picha na Miza Othman –Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar                                      22.11.2018
Wizara ya Afya Zanzibar imetiliana saini Mkataba wa Ushrikiano na Hospitali ya Taifa Muhimbili juu ya utoaji huduma kwa wananchi na kubadilishana Tiba na ujuzi baina ya Wataalamu wa afya wa pande hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Laurence Museru walitia saini mkataba huo katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar, Mnazimmoja.
Dkt. Jamala alisema Mkataba huo mpya wa ushirikiano utawasaidia wagonjwa  ambao matibabu yao yanapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili kupelekwa katika Hospitali hiyo badala ya kuwasafirisha nje ya nchi.
Alisema hatua hiyo itapunguzia gharama kwa wananchi na Serikali ya kutumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kuwasafirisha nje na watapatiwa Tiba kwa njia rahisi katika mazingira waliyozoea.
Hata hivyo Dkt. Jamala amewahakikishia wananchi kuwa Serikali haitafunga milango ya kuwapeleka nje ya nchi wagonjwa ambao Bodi na Utawala wa Wizara wataamua kupatiwa matibabu nje kwa magonjwa ambayo yataonekana ni tatizo kutibika Muhimbili .
Aliongeza kuwa katika makubaliano ya Mkataba huo, wataalamu wa afya wa kada mbali mbali wa Wizara ya Afya Zanzibar watafaidika kupatiwa mafunzo kwa mujibu wa taaluma zao kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbuli Prof. Laurence Museru alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Hospitali hiyo imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma za kibingwa katika magonjwa mbali mbali.
Alizitaja huduma za kibingwa za Tiba ya moyo, mifupa, ngozi na upandikizaji wa vifaa vya kusikia na figo zimekuwa zikifanyika katika Hospitali hiyo kwa mafanikio makubwa na hatua za kufanya Tiba nyengine za kibingwa kwa maradhi mengine zinaendelea
 Aliongeza kuwa Tiba hizo zimepunguza gharama ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 70 na imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi na Serikali kwa jumla.
Prof. Museru alitoa mfano wa gharama ya Tiba ya upandikizaji wa vifaa vya kusikia kwa mgonjwa mmoja nje ya Tanzania ni sh. milioni 100 lakini Tiba hiyo ikifanywa Hospitali ya Muhimbili gharama yake ni sh. milioni 33.
Alisema ushirikiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbi na Wizara ya Afya Zanzibar upo kwa muda mrefu lakini Mkataba mpya wa ushiririkiano wa sasa utatoa fursa  kubwa zaidi kuhakikisha Maendeleo ya Tiba yaliyofikiwa na Hospitali hiyo yanawanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
                                                   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.