Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda ya Sharjah ambae pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Rawabi Bw. Abdallah Sultan Owais akiwa na Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Majid Faisal Khalid Al Qasemi, walipofika Ikulu Zanzibar leo kwa mazungumzo.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameikaribisha Jumuiya
ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah kuzichangamkia fursa za
uwekezaji zilizopo Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah ambae pia, ni Mwenyekiti
wa Kampuni ya Al Rawabi Abdallah Sultan Owais akiwa pamoja na baadhi ya
viongozi wa Jumuiya hiyo.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji, Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) tayari
imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza hapa nchini na kusisitiza kuwa milango ya
uwekezaji ya Zanzibar iko wazi.
Rais Dk. Shein aliueleza
uongozi huo wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa Sharjah kuwa Zanzibar
ina fursa nyingi za kuwekeza katika sekta mbali mbali hapa nchini ikiwemo sekta
ya utalii, viwanda, ufugaji na nyenginezo ambazo Jumuiya hiyo ina uzoefu.
Mbali ya kuitaka
Jumuiya hiyo kuja kuekeza Zanzibar, Rais Dk. Shein pia alisisitiza haja ya kuwepo
mashirikiano na uhusiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya
Zanzibar huku akisisitiza kuwa Zanzibar iko tayari kufanya kazi na Jumuiya hiyo.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Jumuiya hizo mbili
kutaisaidia kwa kiasi kikubwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya
Zanzibar kupanua wigo na kupata uzoefu kutoka kwa wenzao wa Sharjah.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
ufugaji na kusisitiza azma na malengo iliyoweka ikiwa ni pamoja na kujifunza
kutoka kwa Kampuni ya Al Rawabi ya Sharjah ambayo tayari imeshapata mafanikio
makubwa.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio yaliofikiwa
na Kampuni hiyo ya nchini Sharjah ambayo aliitembelea mnamo mwezi Januari mwaka
huu wakati alipokuwa katika ziara yake katika nchini za Jumuiya ya Falme za Kiarabu
(UAE).
Alisisitiza kuwa Kampuni
ya Alrawabi yenye shamba kubwa la ng’ombe wa maziwa ambayo pia, ina viwanda vya
vinywaji vya matunda pamoja na bidhaa nyengine zinazotokana na maziwa ya ng’ombe
imeweza kupata mafanikio makubwa na ipo haja kwa Zanzibar kupanua wigo kutoka
kwa Kampuni hiyo.
Rais Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza haja ya Kampuni ya ndege ya Al Arabia ya
Sharjah kufanya safari zake Zanzibar kwa azma ya kuongeza huduma za usafiri hasa
kwa watalii pamoja na wananchi na wafanyabishara wa pande mbili hizo.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitoa shukurani na pongezi kwa Sheikh Mohammed bin Rashid Al
Makhtoum Makamo wa Rais na Waziri Mkuu
wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa juhudi alizozichukua za
kuhakikisha Kampuni ya ndege ya Fly Dubai inaleta ndege kubwa tena ya kisasa
hapa Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa
amepokea kwa furaha taarifa hiyo kutoka kwa Mwenyekiti huyo kwani jambo hilo
lina umuhimu wa pekee katika kuimarisha huduma za usafiri wa ndege kati ya
Dubai na Zanzibar sambamba na kuimarisha usafiri kwa watalii kati ya pende
mbili hizo.
Nae, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah ambae pia, ni Mwenyekiti
wa Kampuni ya Al Rawabi Abdallah Sultan Owais ameeleza kuvutiwa kwake na
mazingira ya Zanzibar na kumuahidi Rais Dk. Shein kuwa Jumuiya hiyo
itahakikisha inaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Katika maelezo yake,
kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Jumuiya yake imevutiwa kuja
kuwekeza Zanzibar hasa kutokana na mazingira mazuri sambamba na vivutio kadhaa
ambavyo vimekwua vikiwavutia hasa watalii.
Aliongeza kuwa ujio wa
watalii wengi ambao ameushuhudia yeye mwenyewe ni ushahidi wa pekee kuwa
Zanzibar inajiuza kiutalii hatua ambayo inapokelewa vyema na watalii wa kila
pembe ya duniani na kupelekea kumimininika kwa wingi kuja kuitembelea Zanzibar.
Pamoja na hayo,
kiongozi huyo ameeleza azma ya kukuza uhusiano na ushirikiano kati yake na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara husika ya ufugaji kwa lengo la
kuangalia fursa ya kuja kuekeza katika sekta hiyo ya ufugaji.
Pia, kiongozi huyo
alimueleza Rais Dk. Shein hatua ya Kampuni ya Fly Dubai ya kuleta ndege kubwa
ya kisasa ambayo itafanya safari zake kati ya Zanzibar na Dubai ambayo tayari
imeshaanza kazi.
Mwenyekiti huyo wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah alimpa Salamu Rais Dk.
Shein zinazotoka kwa kiongozi wa Sharjkah Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi
ambaye katika salamu hizo alieleza azma yake ya kuendelea kushirikiana na
Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment