Habari za Punde

Wanafunzi jimbo la Magomeni watakiwa kushughulikia masomo yao na kakujiepusha na tamaa

Na Mwashungi Tahir       Maelezo    
NAIBU Waziri wa  Wizara  ya Kazi, Uwezeshaji,  Wazee ,Wanawake na Watoto Shadya Mohamed Suleiman amewataka wanafunzi wa jimbo la Magomeni kushughulikia masomo yao na kujiepusha na mambo ya tamaa kwani  yanaweza kuwapelekea kutofikia malengo yao.
Hayo ameyasema  leo  huko katika ukumbi wa skuli ya Maandalizi ilioko Jimbo la Magomeni wakati wa sherehe ya utoaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu kuingia michepuo , kidato cha pili na kidato cha tano kwa mwaka 2017/2018.
Amesema ili wafanikiwe zaidi katika elimu ni lazima wawe wasikivu na wavumilivu kwa kufuata ushauri wa walimu ndipo watafanikiwa kwani elimu ndio mustakabali mzima wa maisha  na kuwataka waongeze bidii katika masomo  kwani wao ndio wataalamu  watarajiwa wa hapo baadae.
“Wacheni tamaa za kutamani vitu ambavyo wazazi hawana uwezo navyo mambo haya ndio yanayoweza kukuharibieni malengo yenu mliojiwekea ya baadae shuhulikieni masomo yenu”, alisema Naibu huyo.
Vile vile Mh Shadya amewapongeza watoto wa kike kwa kufaulu wengi na kuwataka waache ukimya pale wanapokabiliwa na vitendo vya udhalilishaji kwa kuwaripotia wazee wao ili sheria zichukuliwe kwa haraka.
Aidha aliwataka walimu kuongeza bidii  kwa kuwa karibu na wanafunzi ili kuwashajihisha na Serikali inawaandalia walimu mazingira mazuri na kuwaondolea changamoto zinazowakabili.
Pia aliwaasa wazee kufata nyendo za watoto wao na kuwataka kuwa karibu nao kila wakati kwani vitendo vya ushalilishaji vinazidi kushamiri  hasa kwa wanawake na watoto pamoja na   wanafunzi .
“Vitendo vya udhalilishaji vipo hivyo wazazi wenzangu tujitahidi kuwa na watoto wetu kila wakati ili kuzijua nyedo zao za kila siku, na ukimuona ana kitu cha thamani tusiogope kuwauliza na kufatilia wapi kapata”, alisema Shadya.
Nae Mbunge  wa Jimbo hilo Jamal Kassim na Mwakilishi Rashid Shamsi Makame wamesema wameanza kutoa zawadi hizo tangu walipoanza kuingia madarakani ,  huu ni muendelezo na wameahidi kuendelea kutoa zawadi hizo kwa kila wanaofaulu ili kuwajengea hamasa na kuzidisha bidii katika masomo yao ikiwa ni ahadi zao walizoziahidi.
Wakitoa wito kwa wazee na walimu kuwa na mashirikiano kwa lengo la kuona vijana hao wanafikia nafasi nzuri kielimu kwani duniani kote sasa elimu  ndio inoleta maendeleo na mafanikio hayawezi kupatikana iwapo watakosekana wasomi.
Pia wamekemea vikali wale wote waliohusika na uvujaji wa mitihani kwani kufanya hivyo kutaweza kukosa wataalamu wenye sifa na badala yake Serikali haitokuwa na viongozi wazuri hapo baadae.
“Tunalaani wale wote waliohusika na uvujishaji wa mitihani ya kidato cha pili hawaitakii mema Serikali na tunaomba hatua za haraka zichukuliwe kwa wale wote waliohusika”, walisema viongozi hao.
Nao wanafunzi wamewashukuru viongozi wao kwa kuwapatia zawadi hizo pamoja na Serikali kwa kuweka kipaumbele masuala ya elimu  na kuwaahidi watafanya vizuri zaidi ili waweze kufikia elimu ya juu zaidi kwani na wao wanathamini juhudi hizo.
Jumla ya Milioni 5 laki 7 na 20 elfu zimeweza jkutumika kwa zawadi hizo ambapo ni pamoja na uniform , mabuku na kampas, na wanafunzi 440 wamefaulu katika jimbo hilo kutoka shehia mbali mbali ikiwemo Nyerere A na B, Sogea, Magomeni , Wandaras na Meya juu na Bondeni wanaume 156 na wanawake 284.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.