Habari za Punde

Wizara ya Afya yapokea msaada wa dawa kutoka China wenye thamani ya Bilioni Moja

Mfamasia Mkuu wa Serikali Zanzibar, Habib Ali Sharif akitoa shukrani kwa Serikali ya China kwa msaada mkubwa wa dawa katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Mjini Zanzibar
 Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu akimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed msaada wa dawa uliotolewa na Serikali ya China, makabidhiano haya yamefanyika Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed na Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar  Xie Xiaowu wakisaini hati ya makabidhiano ya dawa zilizotolewa na Serikali ya watu wa China.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed akizungumza na wafanyakazi wa bohari kuu ya dawa mara baada ya makabidhiano ya dawa yaliyofanyika katika Ofisi hiyo Maruhubi Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed katikati na Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu katika picha ya pamoja na timu ya madaktari wa china wanaofanyakazi Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar                                               
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amewataka wafanyakazi wa Bohari Kuu kutumia mifumo ya kisasa ya kuagiza dawa kujuwa takwimu sahihi ya dawa zilizopo kuepuka kununa dawa ambazo zipo kwa wingi katika Bohari na hazitumiki kwa wingi ili kuzinusuru kuharibika .
Waziri Hamad ameeleza hayo Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi alipokuwa akipokea msaada wa dawa tafauti na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja kutoka kundi la Madaktari wa China wanaofanyakazi Hospitali ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee Mkoani.
Alisema kuwa na takwimu sahihi ya dawa, matumizi ya kila siku na sehemu ambazo aina ya maradhi yanawasumbua zaidi wananchi ni hatua muhimu ya kufanikisha kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.
Waziri wa Afya aliishukuru Serikali ya Watu wa China kwa misaada mikubwa wanayotowa katika kusaidia sekta ya Afya ikiwemo dawa na vifaa tiba na kufanya tafiti za magonjwa mbali mbali yanayosumbua Zanzibar na hatimae kuyatafutia suluhisho bila ya kuweka masharti.
Alisema hivi sasa madaktari wa China wa kishirikiana na Madaktari wazalendo wanaendelea kufanya uchunguzi wa maradhi ya Saratani kujua ukubwa wa tatizo hilo Zanzibar na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Hata hivyo amewahimiza wafanyakazi wa Wizara ya Afya kufanya kazi kwa uzalendo na kuweka mbele maslahi ya Taifa na kuhakikisha kwamba dawa zilizopo zinawafika wananchi bila malipo ikiwa ndio sera ya Serikali.
Aliwashauri wafanyakazi wa Afya kutafuta nafasi za masomo nje ya nchi ili kuongeza utaalamu wao na viongozi kwa upande wao kuwaruhusu bila masharti wafanayakazi wanaopata nafasi kwani elimu ndio msingi mkubwa wa maendeleo mengine katika nchi.
Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu alimuhakikisha Waziri wa Afya kwamba nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya Afya ili kuboresha utoaji  huduma kwa wananchi.
Alisema ushirikiano kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar ni wa muda mrefu na kila upande umekuwa ukinufaika kupitia ushirikiano huo na kueleza kuwa utaendelea kuimarika siku hadi siku.
Mfamasia Mkuu wa Serikali Habib Ali Sharif alisema msaada wa dawa uliokabidhiwa  leo umekuwa ukiletwa kila mwaka na makundi ya madaktari wanaokuja kufanyakazi Zanzibar lakini katika kipindi cha nyuma walikuwa wakizihifadhi wao wenyewe na kuwahudumia wananchi bila ya kuzikabidhi Wizara.
Alisema hivi sasa wamebadilisha utaratibu huo na wameamua kuzikabidhi Wizara ya Afya lakini  wataendelea kuzitumia katika Hospitali wanazofanyia kazi Mnazimmoja na Abdalla Mzee ya Mkoani na inapotokea dharura katika Hospitali nyengine watazipeleka kusaidia sehemu hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.