Habari za Punde

Mahafali ya 18 ya Chuo cha Abdulrahman Al-Sumait

  Gwaride la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait yakiingia uwanjani wakati wa Mahafali ya 18 yaliyofanyika kempasi yao, Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Bendi ya Jeshi la Polisi ikitumbuiza katika Mahafali ya 18 ya Chuo Kiuu cha Abdulrahman Al- Sumait kiliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait Professa Amran Rasli akimkabidhi zawadi mwanafunzi Bora wa mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Al-Sumait, Thuwein Thabit Mzee.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al- Sumait Dk. Abdulrahman Almuhilan akiwatunuku vyeti wahitimu mbali mbali katika Mahafali ya 18 Chuo hicho.
Baadhi ya waalikwa waliohudhuria Mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al- Sumait Chukwani Mjini Zanzibar wakifuatilia mahafali hayo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma akiwahutubia wahitimu na wahadhiri pamoja na waalikwa waliohudhuria mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait kiliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.        

Na Ramadhan Ali Maelezo 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali imeanzisha na kuimarisha Mfuko wa Wajasiriamali ili kuwawezesha vijana kiuchumi katika kukabiliana na tatizo la ajira linalozikabili nchi nyingi duniani ikiwemo Zanzibar.
Amewashauri vijana wanaomaliza Vyuo Vikuu na Elimu ya juu nchini kuunda vikundi vya Ujasiriamali na kufuatilia taarifa za mfuko huo katika Wizara ya Kazi, Uwezesdhaji, Wazee, Vijana na Watoto ili kuitumia fursa iliyopo ya kupatiwa mikopo kwa lengo la kuweza kujiajiri wenyewe.
Dk. Shein alieleza hayo katika Mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Bi. Riziki Pembe Juma katika Kempasi ya Chuo hicho Chukwani.
Alisema lengo la kuanzishwa Mfuko huo mwishoni mwa mwaka 2013 ni kuwasaidia wajasiriamali wakiwemo vijana wanaomaliza vyuo na elimu ya juu na wananchi wengine wanaopendelea kujiendeleza kimaisha kwa njia ya kujiajiri wenyewe.
”Kuanzia mwezi Januari hadi Septemba 2018  jumla ya mikopo 441 yenye thamani ya shilingi 685 milioni ilishatolewa kwa vikundi mbali mbali vya ujasiriamali Unguja na Pemba na mikopo zaidi itaendelea kutolewa mwaka huu,” alisema Rais wa Zanzibar.
Alieleza kufurahishwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Al-Sumait kuanzisha mafunzo maalumu kwa wanafunzi katika mwaka wao wa mwisho wa masomo yenye lengo la kuwapata taaluma na ujuzi unaohitajika katika kukabiliana na soko la ajira na alivishauri Vyuo Vikuu vyengine viliopo Zanzibar kuiga mpango huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikipongeza Chuo hicho kwa kazi nzuri ya kuzalisha walimu wenye sifa za juu za kufundisha skuli mbali mbali na wataalamu wengine walioajiriwa katika Taasisi za Serikali na binafsi.
Hata hivyo aliushauri uongozi wa Chuo Kikuu cha  Al Sumait wakati wanajiandaa kuanzisha shahada ya Uzamili ya ‘Islamic Sheria’ kuwa waangalifu na kukaa pamoja na Kamisheni ya Mipango ya Zanzibar ili kupata ushauri na kujua vipaumbele vinavyohitajika katika mahitaji ya taaluma nchini.
Aidha Dk. Shein alipendekeza Vyuo Vikuu vitatu viliopo Zanzibar hivi sasa, Abdulrahman Al-Sumait, SUZA na Zanzibar University cha Tunguu kuunda Kamati ya pamoja kukaa na kubadilishana mawazo kuhusu aina ya programu wanazoanzisha ili kuepuka kuanzisha programu zisizokuwa na uhalisia.
Akizungumza katika mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Sumait Professa Amran Rasli aliwanasihi wanafunzi waliomaliza na wanaoendelea na masomo chuoni hapo kuweka umuhimu wa kulipa madeni ya mikopo waliochukua kwa ajili ya masomo.
Aliwakumbusha wanafunzi kuwa deni ni amana na kulipa deni ni ibada hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa makini na madeni anayodaiwa bila kuangalia kuwa ni deni la Serikali ama la mtu binafsi.
Alisema katika kukiimarisha chuo hicho, wameanzisha programu ya kusomesha wanafunzi wa chekechea ili kuhudumia jamii inayoishi karibu kwa lengo la kujenga umoja na  ushirikiano kati ya chuo na jamii.
Alizitaja hatua nyengine wanazoendelea kuzifanya ni kuimarisha miundombinu, nyenzo, taratibu na sera kwa ajili ya huduma, maslahi na mazinguira mazuri ya wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho.   
Jumla ya Wahitimu 571 wakiwemo 226 wa shahada ya kwanza, 277 wa stashahada na 68 wa cheti walitunukiwa shahada na vyeti vyao baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya ualimu ambapo asilimia 33 ni wahitimu wanawake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.