Habari za Punde

Uzinduzi wa Jengo la Mama na Mtoto Hospitali ya KMKM Kibweni Zanzibar, Ikiwa Shamrashamra za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mkuu wa Kitengo cha Mama na Mtoto LCDR. Mwashamba Mbarouk Salum akimpa maelezo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipotembelea Jengo la Mama na Mtoto na kulifungua rasmi katika Hospitali ya Kibweni.
Na Maryam Kidiko - Melezo Zanzibar. 
Watumishi wa afya ya Mama na Mtoto nchini wametakiwa kutanguliza utu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi na kuacha tabia ya kutumia lugha isiyonzuri wakati wanapotoa huduma kwa wananchi.
Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito huo Kibweni, Wilaya ya Magharibi ‘A’, alipokuwa akizinduwa jengo la Kituo cha Mama na Mtoto katika hospitali ya Kikosi cha KMKM ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kazi ya utowaji wa huduma ya afya ni kazi ya wito inayohitaji moyo wa huruma, upendo na Uvumilivu na kubwa zaidi ni kujitahidi katika kusaidia jamii na kutarajia ujira kutoka kwa Mwenyezi mungu.
Aliwashauri wataalamu wa afya kutumia utaalamu wao  kutekeleza wajibu mkubwa wa kuwahudumia wananchi na kusaidia kuokoa maisha ya Mama na Mtoto ili kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi.
“Ni wajibu wenu kutumia utaalamu wenu na jukumu mlilopewa na Taifa katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji na ufanisi katika Sekta ya afya Nchini,” alisema Makamo wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliwaahidi wataalamu wa huduma ya afya ya Mama na Mtoto kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kila fursa itakapopatikana ndani na nje ya Nchi kwa lengo la kuwaongezea utaalamu zaidi.
Aidha alisema uamuzi wa kuimarishwa kwa huduma ya Mama na Mtoto katika hospitali ya KMKM Kibweni ni jambo la faraja katika Sekta ya afya kwani itasaidia kupunguza msongomano katika hospitali ya Mnazi mmoja na Muembeladu.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa huduma ya mMama na Mtoto katika Hospitali ya KMKM Kibweni kitawapunguzia usumbufu Wananchi kufuatilia huduma hiyo hospitali za mbali na itapunguza idadi ya vifo vya Mama na Mtoto ambavyo ni vikubwa kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani WHO.
Aliwaomba watendaji na Wananchi watakaofika kwa ajili ya kupatiwa huduma kujenga utamaduni wa kuimarisha usafi wa jengo na kuvitunza vifaa vitakavyotumika ili viweze kudumu kwa muda mrefu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.